Lowassa ashinikiza uwaziri


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 17 November 2010

Printer-friendly version
MBUNGE wa Monduli, Edward Lowassa

MBUNGE wa Monduli, Edward Lowassa anadaiwa kumshinikiza Rais Jakaya Kikwete amrejeshe katika baraza la mawaziri, imefahamika.

Lowassa ameomba kupatiwa nafasi ya kuongoza wizara ya mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimatifa, wizara ya ulinzi na jeshi la kujenga taifa, au wizara ya tawala za mikoa na serikali za mitaa. 

Habari zilizothibitishwa na mmoja wa viongozi wa ngazi ya juu katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ambaye yuko karibu na rais Kikwete na Lowassa, zinasema shinikizo la Lowassa limekuwa kubwa kiasi ambacho linamuweka rais njiapanda.

“Lowassa anataka kurejeshwa katika baraza la mawaziri. Ameomba apewe nafasi ya kuongoza wizara ya tawala za mikoa na serikali za mitaa, au wizara ya mambo ya nje,” ameeleza mtoa taarifa wa MwanaHALISI.

Amesema, “Mheshimiwa Lowassa anasema, iwapo hilo likishindakana, basi ateuliwe kuwa waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga taifa.”

Kigogo mwingine ambaye ameomba kurejeshwa katika baraza la mawaziri, ni Andrew Chenge ambaye anataka kuwa waziri wa miundombinu.

Chenge ambaye anakabiliwa na lundo la tuhuma za ufisadi ikwamo kashifa ya ununuzi wa rada, ameomba kupatiwa uwaziri katika wizara ya miundombinu au sheria na katiba.

Taarifa zinasema, Chenge ameshinikiza kuwa iwapo wizara ya miundombinu itagawanywa kwa kurejeshwa kama ilivyokuwa zamani, ambapo kulikuwa na wizara ya mawasiliano na uchukuzi na ile ya ujenzi, basi yeye akabidhiwe wizara ya ujenzi.

Chenge alijiuzulu wadhifa wa uwaziri wa miundombinu, Aprili mwaka 2008, miezi miwili baada ya kukabidhiwa nafasi hiyo. Kujiuzulu kwake kulitokana kuibuka kwa tuhuma nyingi za ufisadi.

Mpaka sasa, Chenge ameshindwa kujinasua kutoka katika tope la rushwa ya rada ambayo serikali ilinunua kwa bei kubwa na isiyohalali.

Anatuhumiwa kujipatia zaidi ya dola milioni moja, sawa na shilingi 2 bilioni, ambazo zimekutwa katika moja ya akaunti zake iliyopo nchini Uingereza.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ikulu, kuna uwezekano mkubwa Rais Kikwete kurejesha wizara hiyo kama ilivyokuwa wakati wa utawala wa awamu ya rais mstaafu, Benjamin Mkapa.

Katika kipindi cha utawala wa miaka 10 ya Mkapa, kulikuwa na wizara mbili – Ujenzi na Mawasiliamo na Uchukuzi.

Aidha, taarifa kutoka ndani ya serikali zinasema rais Kikwete amepanga kuacha mawaziri kadhaa katika baraza lake jipya.

Mawaziri ambao wanatarajiwa kuachwa ni wale waliokaa katika nafasi zao kwa zaidi ya miaka 10 na wale walioshindwa kutimiza wajibu wao. Majina ya mawaziri hao tunayahifadhi kwa sasa.

Tayari mawaziri kamili watano na manaibu waziri wanne wameshindwa katika uchaguzi. Baadhi yao ndani ya chama chao na wengine katika mbio na wagombea wa vyama vya upinzani.

Mawaziri walioshindwa katika uchaguzi ni Batilda Burian ambaye alikuwa waziri katika ofisi ya makamu wa rais (Mazingira), Lawrence Masha (Mambo ya Ndani), Philip Marmo (Sera, Uratibu na Bunge), Diodorus Kamala (Afrika Mashariki) na Shamsa Mwangunga (Maliasili na Utalii).

Katika orodha hiyo wamo naibu mawaziri, Aisha Kigoda (Afya na Ustawi wa Jamii), Mwamtumu Mahiza (Elimu na Mafunzo ya Ufundi), Joel Bendera (Habari, Utamaduni na Michezo) na James Wanyanche ambaye alikuwa naibu wizara ya uvuvi na mifugo. 

Mtoa taarifa anamtaja anayeshikia bango Kikwete kumrejesha Lowassa katika baraza la mawaziri, kuwa ni mfanyabiashara na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz.

Rostam amekuwa akitajwa kuwa anajitapa kwamba hatua ya chama hicho kufanikiwa kumuengua Samwel Sitta italeta amani katika chama na kwamba kwa sasa hakuna kizingiti kingine kinachomzuia Lowassa kurejea katika serikali. 

Hata hivyo, mbunge wa Simanjiro, Cristopher ole Sendeka alipoulizwa kama hatua ya kumuondoa Sitta inaweza kurejesha umoja katika chama, haraka alisema, “Vita haijaisha.”

Alisema, “Ugomvi wetu haukuwa ubinafsi. Ulihusu maslahi ya nchi na watu wake. Kama Rostam, Chenge na Lowassa wanadhani vita imekwisha kwa Sitta kutokuwa spika, basi hawajui kiini cha ugomvi. Hiki ni kicheko cha muda tu,” amesisitiza. 

Gazeti hili lishindwa kumpata Rostam kueleza iwapo ametumwa na Lowassa na Chenge kufanya kazi aliyojipa ya kuwapigia debe kwa Rais Kikwete. 

Habari zinasema Rostam amekuwa akishinikiza Kikwete, hasa baada ya kuwapo kwa taarifa kuwa rais anaweza kumuopoa aliyekuwa Spika wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta na kumkabidhi moja ya wizara katika serikali yake.

“Anayehangaika kila upande ni Rostam. Yeye ndiye anayemueleza rais na watu waliokaribu na rais, kwamba ni muhimu Lowassa akarejeshwa katika baraza la mawaziri, ili kuleta umoja na mshikamano kwa kuwa Sitta atapewa moja ya wizara,” mtoa taarifa amenukuliwa.

“Angalia hawa watu walivyo. Wanataka kurejeshwa serikalini na papohapo wanampangia rais nafasi za kuwapa. Hii ni hatari kwa mustakabali wa taifa,” anaeleza kiongozi mmoja wa ngazi ya juu wa CCM ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa huyo, mbali na Lowassa kutoa sharti la kutaka kurejeshwa katika baraza la mawaziri, anataka Kikwete kutenganisha wizara ya tawala za mikoa kutoka ofisi ya waziri mkuu na kuwa wizara inayojitegemea.

Inaelezwa kwamba Lowassa anataka kutumia wizara hiyo kujijenga kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kwa kuwa wizara hiyo ndiyo imetandawaa nchi nzima. 

“Unajua huyu bwana amepiga hesabu kubwa. Hii ndiyo wizara ambayo itamuwezesha kuwasiliana moja kwa moja na wakuu wa mikoa na wilaya. Ndipo atakapoweza kuwasiliana na wakurugenzi wa halmashauri, mameya na wenyeviti wa halmashauri za wilaya na miji. Lengo ni mwaka 2015,” kinaeleza chanzo cha taarifa.

Kwa upande wa Sitta, habari zinaeleza aliahidiwa na Rais Kikwete kuteuliwa kuwa waziri, ama wa miundombinu au mambo ya ndani.

Hata hivyo, awali taarifa zilisema Sitta alikataa ombi la rais la kumteua kushika nafasi hiyo, badala yake alitaka serikali iendelee kulipia pango la nyumba anayoishi na kumuachia gari la serikali na walinzi.

Lakini siku moja baadaye, taarifa zinasema Sitta aliomba kupatiwa nafasi hiyo. Hakuna sababu ambazo zimetajwa zilizomfanya Sitta kubadilisha uamuzi wake wa awali.

MwanaHALISI lilipomtafuta Sitta kutaka kuthibitisha madai hayo, alisema yuko kwenye mkutano wa wabunge wa chama chake. Aliahidi kupiga simu mara baada ya kutoka. Hakufanya hivyo.

0
Your rating: None Average: 3 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: