Lowassa atajwa tena


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 02 June 2010

Printer-friendly version
Edward Lowassa

KUNA ushahidi wa kutosha kwamba mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UV-CCM) aliyejiuzulu wazifa wake, Hamad Masauni Yusuf, amesulubiwa kutokana na kile kinachoitwa na wapinzani wake, “dhambi ya kumbeba Edward Lowassa.”

Taarifa kutoka ndani ya UV-CCM, marafiki wa mwanasiasa huyo na CCM yenyewe, zinasema kuwa Masauni ameondolewa katika nafasi yake baada ya kutofautiana na baadhi ya wajumbe wenzake waliotaka Lowassa aondolewe katika mwenuyekiti wa baraza la wadhamini ndani ya umoja huo.

MwanaHALISI limegundua kuwa Masauni alianza kutofautiana na wenzake ndani ya UV-CCM baada ya kukataa kupitisha azimio la kumuondoa Lowassa katika nafasi hiyo.

Masauni alikuwa mwenyekiti wa kikao cha Kamati ya Utekelezaji cha jumuiya hiyo, ambacho kilipokea pendekezo la kumtoa Lowassa katika anayoishikiria.

Katika mkutano huo, Masauni na baadhi ya wajumbe walipinga Lowassa kung’olewa kwa hoja kwamba kufanya hivyo kutawaingiza katika mtafaruku usiyokuwa na sababu.

“Ndani ya kikao, Masauni alijenga hoja kwamba iwapo Lowassa tutamtoa katika nafasi yake ya Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini, lazima tujiandae kujibu maswali. Kwamba tumemuondoa kwa nini,” amesema mtoa taarifa akimnukuu Masauni.

Taarifa zinasema msimamo wa Masauni wa kutaka Lowassa abakishwe katika nafasi yake haukufurahisha baadhi ya wenzake ndani ya UV-CCM. “Hapo ndipo chokochoko ilipoanzia. Masauni alitaka kuendeleza utamaduni wa kulinda wakubwa, kumbe wenzake walikuwa na ajenda yao,” alisema mtoa taarifa wetu.

Kwa mujibu wa taarifa aliyewasilisha hoja ya kumng’oa Lowassa katika nafasi yake ndani ya kikao cha Kamati ya Utekelezaji, ni Ridhiwani Kikwete.

Habari zinasema awali Ridhiwani alikutana na Masauni na kumueleza mkakati wa kubadilisha wajumbe wa baraza la wadhamini la UV-CCM, ambapo Masauni kwa sauti ya upole alijibu, “sawa, tusubiri vikao.”

Kwa mujibu wa Katiba ya UV-CCM, kikao cha Kamati ya Utekelezaji ndicho chenye mamlaka ya kupendekeza kwa Baraza Kuu la UV-CCM majina ya wajumbe wa Baraza la Wadhamini.

Aprili mwaka juzi, gazeti hili liliripoti Baraza la Wadhamini la UV-CCM chini ya uenyekiti wa Lowassa lilisaini kinyume na taratibu mkataba uliomuwezesha mbia kuanza utekelezaji wa mradi wa kitega uchumi cha UV-CCM.

Mradi huo ni Jengo la Vijana na ujenzi katika kiwanja Na. 108/2 barabara ya Morogoro jijini Dar es Salaam.

Siku moja baada ya taarifa hiyo kuchapishwa, karibu wajumbe wote wa Baraza la Wadhamini, ukiondoa Nazir Karamagi, walinukuliwa wakina kufahamu chochote kwenye mkataba wa Lowassa.

Waliomkana Lowassa walikuwa ni William Lukuvi, Mohammed Yusuf (Yusuf Mrefu) na Mery Nagu.

Kingine kinachodaiwa kimechangia kumtokomeza kisiasa, ni uamuzi wake wa kupinga mpango wa chama chake kuchangisha fedha kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu za mkononi sms.

“Ndani ya Kamati Kuu (CC), Masauni alisimama kupinga mpango wa chama kutumia sms kutafuta michango. Alisema mpango ule si endelefu na hauwezi kusaidia chama kujikwamua kiuchumi. Mle ndani ya CC, Masauni alitaka chama kifanye harambee kila mkoa kutokana na bajeti ya mkoa husika, badala ya utaratibu wa kutumia sms,” anasema mtoa taarifa wetua aliyekuwa ndani ya CC.

Inaelezwa kwamba Masauni alikiambia kikao cha CC, chini ya rais Jakaya Kikwete, kwamba kama chama chake kinataka kufanikiwa katika mpango huo, basi ni lazima uboreshwe kwa kuweka shindano litakalioambatana na zawadi.

“Yule bwana alisema ndani ya CC, kwamba wanachama wetu hawana utamaduni wa kuchangia chama chao. Alitoa mfano wa gazeti la chama Uhuru, kwamba kama wanaCCM wangekuwa na utamaduni wa kuchangia chama angalau kwa kununua gazeti hilo, basi Uhuru lingekuwa gazeti la kwanza kwa mauozo nchini,” mmoja wa marafiki wa karibu na Masauni alisema.

Masauni alijiuzulu uenyekiti wa UV-CCM katika mkutano wa Baraza Kuu la Vijana wiki mbili zilizopita, kutokana na kile kilichodaiwa, “kughushi umri wa kuzaliwa.”

Wakati nyaraka za ndani ya chama zikionyesha kuwa Masauni alizaliwa Oktoba 1979, zile za idara ya uhamiaji zilionyesha kuwa alizaliwa Oktoba 1973.

Taarifa za ndani ya CC iliyofanyika siku mbili baada ya Masauni kujiuzulu, zinanukuu Rais Jakaya Kikwete akisema, “kama Masauni anasema amezaliwa 1979, basi atakuwa alianza shule akiwa tumboni.”

Hii ni baada ya nyaraka za Masauni kuonyesha kuwa alianza elimu yake ya msingi mwaka 1979.

Hata hivyo, taarifa zinasema nyaraka ambazo zinadaiwa kuwa za kughushi ambazo inadaiwa kuwa zimetengezwa na Masauni, ziliandaliwa na viongozi wa UV-CCM Zanzibar kwa ushirikiano na mke wa kada mmoja wa chama hicho.

Aidha, habari zinasema mke wa kada huyo, ndiye aliyeibua hoja hiyo baada ya Masauni kutofautiana na mumewe katika harakati za kuwani kiti cha ubunge katika jimbo moja la uchaguzi visiwani Zanzibar.

Mbali na tafrani hilo, Masauni tayari alikuwa hapikiki chungu kimoja na wenzake katika UV-CCM hasa kutokana na msimamo wake wa kutaka umoja huo usiingilie mambo yasiyouhusu.

Vilevile, Masauni alikwaruzana na wenzake, Beno Malisa na Ridhiwani Kikwete, mara baada ya kumteuwa Hussen Bashe kuwa mjumbe wa Baraza Kuu la Vijana. Bashe alikuwa mmoja wa wagombea wa nafasi ya makamu mwenyekiti ambaye alishindwa na Malisa.

Taarifa zinasema hata uteuzi uliofanywa na Masuani wa wajumbe wa kamati ya utekelezaji ambao haukufuata matakwa ya Ridhiwani na wenzake, ulizidisha ufa kati yake na wenzake katika jumuiya na chama kwa jumla.

“Kaka yule Mzanzibari walidhani wataweza kumdhibiti. Kumbe wapi! Alikuwa anawaangalia, kisha anajibu tusubiri kikao. Jamaa wakaona hapa hakuna kitakachofanyika. Ndiyo sababu ya kumjengea zengwe,” amesema mjumbe mmoja wa baraza anayetajwa kuwa mfuasi wa Masauni.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba ametajwa kuwa ndiye aliyeshinikiza Masauni kuandika barua ya kujiuzulu kwa madai kuwa ametumwa na rais Kikwete.

“Kuanzia Iringa hadi ndani ya CC, Makamba alikuwa anasema ‘Mwenyekiti kazi uliyonituma nimeifanya kama ulivyoagiza,” chanzo cha taarifa kinasema.

Awali taarifa zinaeleza kuwa Makamba alimuita Masauni na kumtaka kuachia ngazi, vinginevyo kikao cha CC kitamuondoa katika nafasi yake kwa nguvu.

Alipoulizwa Makamba kuhusika kwake kushinikiza Masauni kujiuzulu alisema, “sina la kusema.”

Alipobanwa kuwa ni muhimu akajibu tuhuma zinazomkabili, Makamba alisema, “nashukuru, lakini sina la kusema.”

Aidha, Makamba anatuhumiwa kukoromea kwa njia ya simu, kada wa chama hicho, John Nchimbi na Bashe kwa madai kuwa walihusika katika kusmshawishi Masauni kutokuachia ngazi.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: