Lowassa atuma shushushu CHADEMA


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 18 April 2012

Printer-friendly version

HATUA ya mfuasi mkuu wa Edward Lowassa kuhama CCM na kujiunga CHADEMA, imetafsiriwa kuwa njia ya Lowassa “kutuma shushushu” katika chama cha mageuzi.

Lakini Millya amejitetea akisema, “Sijatumwa kuchunguza wala kuua CHADEMA. Ndugu yangu nia yangu ni njema na ili kuthibitisha hilo ni kwamba kuona ni kuamini,” anasema Millya; “CHADEMA ni chama chenye matumaini mapya kwa maisha ya Watanzania.”

Naye Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigella alisema kujiondoa kwa Millya  ni hatua ya utekelezwaji wa maazimio ya NEC iliyoagiza baadhi ya wanachama wake kujipima na kama wakijiona kuwa ni mizigo wajiondoe mapema.

Mmoja wa viongozi wa ngazi za juu makao makuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jijini Dar es Salaam amesema,  “Si bure. Nani asiyemfahamu James ole Millya, kuwa ni kidole na pete na Lowassa? Kuna kitu wanatafuta.”

Millya amekuwa mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) mkoa wa Arusha. Alitangaza kujiunga na CHADEMA juzi Jumatatu.

Lowassa ni waziri mkuu aliyejiuzulu kutokana na kashfa ya mkataba wa kufua umeme wa kampuni ya Richmond.

“Imenishtua, imeniudhi na itakiweka chama chetu mahali pabaya. Ni hatua ya tata,” amesema ofisa mmoja wa ngazi za juu wa CHADEMA.

Amesema Millya amekuwa mfuasi mkubwa wa Lowassa; na Lowassa hivi sasa yumo katika mbio za “kusafisha jina lake” tayari kwa kugombea urais mwaka 2015.

“Jambo hili halina heri. Huu ni mtego na mpango mkakati wa kutudhoofisha. Wanajua CHADEMA ina nguvu na imejipanga kutwaa madaraka mwaka 2015,” ameongeza ofisa huyo ambaye ameomba asitajwe jina.

Hata hivyo, mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe amesema wanamkaribisha Millya wakiamini kwamba ni mpambanaji katika kutaka kuleta mageuzi ya kiuongozi nchini.

Hofu ya wanachama wengi wa CHADEMA waliopiga simu kwenye chumba cha habari MwanaHALISI, kuhusu suala hilo ni kwamba Millya ametumwa kama shushushu kwa ajili ya kujua mikakati ya chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Katika kipindi chote ambacho viongozi wa ngazi za juu wa CHADEMA wamekuwa wakishutumu mikataba ya kifisadi iliyoliingizia hasara taifa, ukiwemo mkataba wa kampuni ya kufua umeme wa Richmond, Millya siyo tu amekuwa kimya; amemganda Lowassa kama luba.

Aidha, Millya amekuwa mtiifu kwa Lowassa ambaye amekuwa akishutumiwa kwa kuhusika kuipa zabuni ya kufua umeme kampuni ya Richmond ambayo haikuwa na uwezo wala vifaa.

Hata Lowassa aliposhutumiwa pia kuhusika kuhamisha mkataba huo kwa kampuni ya Dowans, Millya alikaa kimya.

Tathmini iliyofanywa na wanachama wengi wa CCM juu ya kushindwa kwa chama hicho kung’ara katika uchaguzi mkuu mwaka 2010 ilionyesha kulitokana na kuwepo kwa watuhumiwa ufisadi ndani yake.

Watuhumiwa wa ufisadi ambao hata Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) iliazimia kuwang’oa kwenye chama ni waliohusika na mikataba ya Richmond na Dowans na ununuzi wa rada ya Jeshi la Wananchi.

Wanachama wa CCM waliokuwa wanatuhumiwa na kwamba lazima waondolewe kama magamba ni aliyekuwa mwanasheria mkuu na Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge; mfanyabiashara maarufu Rostam Aziz ambaye alikuwa mbunge wa Igunga, na Lowassa.

Tofauti na mawazo ya wana-CCM, Millya amesema, “Chama hiki kinavurugwa na Samuel Sitta na Dk. Harrison Mwakyembe kwa kueneza vitu vya uwongo dhidi ya Lowassa.”

Millya alikuwa akimshutumu Sitta aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa kwa kuunda Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza sakata la mkataba wa Richmond.

Kamati hiyo iliyokuwa chini ya Dk. Mwakyembe ndiyo iliweka wazi “ujasiri wa kifisadi” katika mradi huo na hatimaye Lowassa akajiuzulu pamoja na aliyekuwa Waziri wa Afrika Mashariki, Dk. Ibrahim Msabaha na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi.

Baada ya NEC kuazimia watuhumiwa wote wa ufisadi wajiondoe, Rostam Aziz alijiuzulu nyadhifa zake zote lakini si kwa ufisadi bali kwa kile alichoita siasa uchwara ndani ya CCM. Lakini Chenge aliwaambia wapigakura wake wasiwe na hofu kwani lile gamba “limeishia kiunoni.”

Millya alikaririwa akisema kuhusu kashfa ya Richmond na kujiuzulu kwa Lowassa kuwa, “Kama kuwajibika katika kashfa hiyo, aliyepaswa kuwajibika ni rais mwenyewe aliyekuwa mwenyekiti wa baraza la mawaziri.”

Historia ya Millya ndiyo inawafanya wanachama na wafuasi wa CHADEMA waamini huenda kijana huyo ametangulizwa kwa malengo maalum ambayo baadaye yanaweza kuwa na madhara makubwa kwa chama.

Akitangaza uamuzi wa kuvua fulana za njano, kofia za njano na kuvaa magandwa ya CHADEMA juzi, Millya alisema kuminywa kwa demokrasia ni sababu ya msingi ya yeye kujiondoa CCM.

“Mwenyekiti (Rais Jakaya Kikwete) ameendelea kupuuza mawazo ambayo sisi wengine tumeona kwamba yangeweza kuimarisha chama, lakini CCM imekuwa ni ya wachache,” alisema.

“Mwenyekiti ameshindwa kazi kwa sababu Kamati Kuu (CC) inayoongozwa na Rais Kikwete imeshindwa kusimamia serikali na kuleta matumaini mapya ndani CCM na kwa Watanzania.”

Pia alimtaja mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM, Ridhiwani Kikwete kwa “kushiriki” tamko la kibaguzi kwamba “Rais ajaye 2015 hatatoka Kaskazini.”

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: