Lowassa: Demokrasia na utani


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 16 February 2011

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala
Edward Lowassa

MBUNGE wa Monduli na waziri mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa ameibuka na kutolea matamko masuala mazito ya kimataifa kabla ya wizara ya mambo ya nje kutoa msimamo wa serikali.

Lowassa ameunga mkono wananchi wa Misri waliomtimua rais wao, Hosni Mubarak. Ni siku chache tu tangu achaguliwe kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

Alisema mengi. Lakini kubwa alilozungumzia ni baadhi ya viongozi kushindwa kuhudumia wananchi wao, na kuishia kujilimbikizia mali.

Ninajilazimisha kuamini kuwa Bw. Lowassa alimaanisha kila neno na kila kauli aliyoitoa kuhusiana na masuala hayo ya Misri na mtazamo wake kuhusu masuala ya kiuongozi wa taifa.

Ninataka kuamini kuwa Lowassa alikusudia kutuma ujumbe wa kujionesha kuwa yeye ni tofauti na viongozi wa Misri na viongozi wengine wa Tanzania; yaani kauli yake ilikuwa inawahusu watu wengine wote isipokuwa yeye! Nimejishika mkono natikisa kichwa changu kwa kukataa.

Lowassa ni sehemu ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ni zao la mfumo uliowatengeneza viongozi wote wa CCM tunaowaona leo. Tangu Umoja wa Vijana (UV-CCM), Lowassa hajabadilika. Katika miaka yote ambayo amekuwa mbunge huku akishika nafasi mbalimbali ikiwemo ile ya waziri mkuu, Lowassa hajawahi kutuonesha kuwa  fikra zake ni kinyume na zile za chama chake.

Kwa muda mrefu wananchi wamekuwa wakilalamikia hoja ya Katiba Mpya; kwamba katiba yetu ya sasa ina matatizo mengi sana kiasi kwamba hayawezi kuondolewa kwa kuifanyia mabadiliko.

Sikumbuki (naweza kusahihishwa) wakati wowote ambapo Lowassa aliwahi kuunga mkono hoja ya Katiba Mpya, siyo wakati akiwa mbunge wa kawaida au akiwa waziri au waziri mkuu.  Hata wakati huu ambapo tunazungumzia suala la Katiba Mpya, bado hajatokea kiongozi yeyote wa CCM ambaye anaunga mkono kuwa na Katiba Mpya kabla ya 2015. Wote wanataka tukusanya maoni, tuzungumze, halafu tufikirie lini Katiba Mpya ije.

Hata suala la kuundwa upya kwa tume ya uchaguzi, hakuna wakati wowote ambapo Lowassa aliposimama nasi kudai tume ina matatizo. Na hata hivi sasa sidhani kama anaamini kuwa kuna tatizo katika sheria ya tume ya uchaguzi.

Leo hii, Lowassa anapongeza “wanaharakati wa Misri” ambao wamefanikiwa kuondoa chama tawala madarakani kutoka na kukithiri kwa ufisadi nchini humo, anataka watu waamini kuwa tatizo la Wamisri lilikuwa ni Hosni Mubarak peke yake?

Wananchi wa Misri walikuwa na tatizo la mfumo wa kifisadi uliojengwa kwa muda wa miaka thelathini. Wanaharakati wa Misri hawakuanza juzi kutaka mabadiliko; wamefanya hivyo kwa miongo kadhaa; kilichotokea juzi ni hitimisho la kile walichokuwa wakikidai.

Je, Lowassa yuko tayari kutoa pongezi kwa wanasiasa wa upinzani wanaojaribu kuondoa chama chake madarakani kutokana na kujenga, kuulinda na kuupepea mfumo wa kifisadi kwa zaidi ya miaka thelathini sasa?

Au Lowassa atakuwa kama Ahmedinajad wa Iran ambaye alipongeza wananchi wa Misiri “kutumia haki yao” kupinga serikali, lakini walipotaka wananchi wake kuandamana, amekimbilia kusema, “Ni kinyume na sheria?”

Kama Lowassa ni mkweli, mbona hajaungana na wananchi wa Arusha wanaopinga uchaguzi wa meya na umwagikaji wa damu? Maandamano ya Misri yalipigwa marufuku na polisi kwa madai kuwa taarifa za “intelligensia” zinaonyesha kuwa yataleta vurugu.

Kama Lowassa anaamini alichokisema, basi angefika mbali zaidi. Angesema kwa kuwa mimi sasa, ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, niko tayari kuchunguza kilichotokea kule Arusha. Angesema bila kutafuna maneno, kwamba “Bunge litachunguza na majibu yote, bila kuchakachuliwa yatawasilishwa bungeni.”

Lowassa anaamini tatizo kubwa la Misri ni Mubarak kukaa madarakani kwa muda mrefu. Amejaribu kuhusisha kukataliwa kwake na wananchi na muda wake wa kukaa madarakani. Kama hili ni kweli, anaonaje kama atakuja na pendekezo la kuweka kikomo cha kipindi cha ubunge?

Hivi anafikiri wananchi wanaridhika na mtindo wa wabunge kutokuwa na ukomo kiasi kwamba tuna wabunge ambao wengine wamewahi kuwepo tangu enzi za vita baridi?

Kama kweli anafikiri kuna tatizo la viongozi kukaa madarakani muda mrefu aje na mswada wa ukomo wa ubunge. Lakini hata asipofanya hivyo, mjadala wa Katiba Mpya ambao tumeupigia debe sisi wengine tutawawekea kikomo hicho. Kama rais amewekewa kikomo, basi wabunge nao wajiandae.

Na kwa vile katiba mpya inatakiwa kabla ya uchaguzi wa 2015, basi wale wote waliokwisha kutumikia bunge miaka 10 mfululizo, kikomo chao kitakuwa mwaka 2015. Je, Lowassa yuko tayari kutuunga mkono?

Lakini Lowassa alienda mbele vile vile na kutaka viongozi “wasijilimbikizie mali” akihusisha hilo na kung’olewa madarakani kwa rais Mubaraka ambaye inadaiwa amejikusanyia utajiri kumshinda hata Bill Gates.

Angalizo lake la viongozi kutokujilimbikizia mali linanishangaza! Kwa miaka karibu 15 chama chake kimekuwa kikiimba wimbo huu na kuurudia wakati mwingine bila ya kuwa na viitikio. Leo hii wanatuambia viongozi wasijilimbikizie mali. Lowassa anazungumzia viongozi gani? Makatibu kata na wenyeviti wa vijiji? Yumkini wengine ni wabunge kama yeye? Je, na yeye yumo?

Katika kauli hiyo kuna jambo jingine pia ambalo ni lazima waopinga “viongozi kujilimbikizia mali” hawe tayari kuliangalia. Wananchi hatuna tatizo na viongozi kujilimbikizia mali. Tatizo ni jingi gani viongozi wetu walivyopata hiyo mali; yaani wanapata utajiri usio na kikomo wakiwa katika nafasi za uongozi, tena kwa njia haramu.

Tatizo siyo mtu anayefanya kazi kwa uhalali, akafanya biashara zake za pembeni kwa uhalali na kupata utajiri. Hatuna ugomvi na utajiri wa mtu. Tatizo letu ni jinsi gani utajiri huo ulivyopatikana. Hilo ndilo tatizo na ndiyo sababu ya vita dhidi ya ufisadi.

Angalia mafao ya wabunge wanavyolipwa mishahara minono. Angalia hata Lowassa mwenye anavyochota katika hazina ya taifa, asilimia themanini ya mshahara wa waziri mkuu wa sasa wakati hajawahi kustaafu?

Mgogoro wa Misri si kwa sababu Mubarak alikuwa tajiri! Bali, kwa sababu aliupata vipi utajiri huo katika nchi ambayo wananchi wake ni maskini wa kutupwa.

Wakati wa vita ya Kagera mmoja wa makamanda waliokwenda kumng’oa nduli Iddi Amini, “Tunachogombania ni ardhi yetu.”

Tunachogombania ni utu wetu, ni heshima yetu, ni hadhi yetu kama wananchi na kama wanadamu. Hatugombanii vyeo vyao, na wala hatugombanii saluti wanazopigiwa na bendera wanazopeperushiwa. Tunachogombania ni nafasi ya Watanzania kufanikiwa katika nchi yao. Viongozi wote wanaotuchezea akili na wanaojaribu kutuuzia uongo kama ukweli, ni lazima tuwakatae.

Kwa mawasiliano na Mwanakijiji andika katika Facebook: "mimi mwanakijiji"
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: