Lowassa hasafishiki


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 06 April 2011

Printer-friendly version
Edward Lowassa

JUHUDI za waziri mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, kujisafisha mbele ya jamii, zimegonga mwamba baada ya kubainika kuwa ni serikali iliyoingiza kampuni ya Richmond katika mkataba wa kufua umeme.

Wakati huo, maelekezo yote kuhusiana na utoaji mkataba kwa Richmond yalikuwa yakifanyika chini ya Lowassa, kwa mujibu wa waziri wa nishati wakati huo, Dk. Ibrahim Msabaha.

Ilibainika katika kikao baina ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za serikali na makatibu wakuu wa Fedha na Nishati, kwamba TANESCO ililazimishwa na serikali kuingia mkataba na kampuni ya kitapeli ya Richmond.

Taarifa zimeeleza kuwa serikali ilitupilia mbali sheria zote za manunuzi na mikataba ili “kulazimisha na kulinda Richmond kupewa zabuni.”

Kamati teule ya bunge, katika uchunguzi wake wa kashfa hii, pamoja na kutaja wahusika wote na kutaka wawajibishwe, ilimwacha waziri mkuu “kuchukua uamuzi” anaoona unafaa. Lowassa alijiuluzu.

Taarifa zinaonyesha serikali iliingia mchakato wa kupata mzabuni, hata baada ya TANESCO kuona kuwa hakukuwepo mshindi kwa mujibu wa zabuni.

Kinyume na maoni ya TANESCO, wizara ya nishati, baada ya kupitia maombi ya zabuni, iliamuru bodi kukubali kuwa Richmond ndiye mshindi na Juni 19, 2009 wizara ikaagiza TANESCO kusaini mkataba na Richmond.

Katika uchunguzi wa bunge, ilibainika kuwa Richmond haikuwa na fedha, uwezo wa kiufundi, vitendea kazi wala uzoefu katika miradi kama hii.

Mkataba wa Richmond ulirithiwa na kampuni ya Dowans Holdings SA ya Costa Rica na Dowans Tanzania Limited (DTL).

Kwa mujibu wa Ibara ya 68 ya sheria ya manunuzi ya mwaka 2004, jukumu la kuamua mshindi wa zabuni ni la bodi ya zabuni ya shirika (TANESCO).

Kwa msingi huo, kamati iliyoteuliwa na serikali kushughulikia mkataba na zabuni, haikuwa na mamlaka ya kisheria ya kufanya uamuzi kuhusu zabuni.

Hiki ndicho chanzo cha kamati ya bunge ya hesabu za mashirika ya umma kufikia hitimisho wiki iliyopita kwamba ni serikali inayopaswa kubeba mzigo kwa vile TANESCO ilikuwa ikiamriwa tu.

Mahakama ya Kimataifa ya usuluhishi wa migogoro ya kibiashara (ICC) iliamua katika kesi ya madai, Novemba mwaka jama, kuwa TANESCO ilipe Dowans na Richmond dola 62.4 milioni (sawa na Sh. 94 bilioni) kwa kuvunja mkataba wake.

Tayari Dowans wamesajili uamuzi wa ICC mahakama kuu kama utaraibu wa kulipwa unayotakiwa.

Hata hivyo, TANESCO inapinga tozo hiyo. Katika utetezi wake, shirika hilo la umeme, pamoja na hoja nyingine, inawasilisha pia kuwa ililazimishwa na serikali kuingia katika mkataba.

Wachunguzi wa mambo ya utawala bora wanasema Lowassa, ambaye aliwahi kukiri kuwa alikuwa karibu sana na mchakato wa kupata mfua umeme na kwamba alikuwa akimpa rais taarifa mara kwa mara, hawezi kujinasua katika kashfa hii.

“Hilo siyo swali, hata wewe unaona na Lowassa mwenye aliliona ndiyo maana aliamua kujiuzulu kabla hajafukuzwa au kabla bunge halijataka achukuliwe hatua,” ameeleza kiongozi mmoja wa asasi ya kijamii inayofundisha masual ya utawala bora.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, alilithibitishia gazeti hili kuwa ni ni kweli serikali imefikia maamuzi hayo.

“Tumekaa na wenzetu wa Hazina na tukakubaliana kuwa TANESCO waandike mahesabu ya malipo haya kwenye vitabu vyao lakini kimsingi, kama uamuzi wa kulipa utafikiwa, serikali ndiyo itakayolipa,” alisema Jairo.

Jairo alisema serikali inafahamu kuwa ni yenyewe ndiyo iliyosimamia mchakato mzima uliotoa zabuni ya kuzalisha umeme kwa Richmond na Dowans, na ndiyo maana akasema itabeba jukumu la kulipa.

“Kama itafikia mahali tukatakiwa kulipa deni hilo, God Forbid (Mungu apishie mbali), basi serikali ndiyo itakayochukua jukumu hilo na si TANESCO,” alisema katibu huyo.

Alipoulizwa na MwanaHALISI ni hatua gani imechukuliwa na serikali dhidi ya wale watakaosababisha iingie katika hasara yote hiyo,  Jairo alijibu kwa ufupi, “Waliosababisha matatizo haya mnawajua.”

Huku Lowassa akiwa anajitahidi “kujisafisha” kwa kauli mbalimbali, imefahamika kuwa serikali ina mpango wa kumpa upendeleo katika ujenzi wa ofisi ya mbunge jimboni kwake.

Wakati bajeti ya serikali ya mwaka 2009/2010, ilipanga Lowassa ajengewe ofisi jimboni Monduli kwa Sh. 40 milioni, taarifa zinasemna ofisi yake itagharimu mara nne ya kiasi kilichopangwa.

Nyaraka ambazo MwanaHALISI imeona zinasema wakati kiasi cha awali cha fedha (Sh. 40 milioni) kilipokuwa tayari kimetumwa, ghafla serikali ikaja na mawazo mengine.

Hata hivyo, gazeti hili limeambiwa kuwa kutokana na kile kilichoitwa, “sababu za kiusalama,” serikali iliamuru “ofisi ya waziri mkuu mstaafu ambaye ni mbunge ijengwe tofauti na ofisi za wabunge wengine.”

Haikulezwa kama Lowassa ataendelea kuwa mbunge maisha yake yote, kwani ofisi hiyo yaweza kuwa chini ya mbunge mwingine wa CCM au wa upinzani.

Ikumbukwe pia kuwa mwaka 2006, serikali ilimjengea Lowassa nyumba ya mamilioni ya shilingi kwa kisingizio cha waziri mkuu mstaafu mtarajiwa, lakini hakuweza kumaliza hata kipindi cha kwanza cha uongozi.

Gazeti hili limefanikiwa kuona nakala za barua za mawasiliano miongoni mwa maofisa wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali na Ofisa Tawala wa Mkoa wa Arusha kuhusu ongezeko hilo la gharama ya ofisi ya Lowassa.

“Kwa taarifa tulizozipata kutoka kwa katibu tawala wa Arusha, ujenzi wa ofisi hiyo umeanza, lakini fedha iliyotolewa ni kidogo ikilinganishwa na mahitaji.”

“Ofisi ya Waziri Mkuu – OWM-TAMISEMI imeiandikia Hazina barua Na. CAB.2.317/01 ya tarehe 17 Februari 2011 juu ya kuomba fedha zaidi ambazo ni Sh. 131 milioni kwa ajili ya kujenga ofisi ya mheshimiwa mbunge wa Monduli,” inasema sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na T. Bangandashwa, Februari 24 mwaka huu.

Bangandashwa anasema, “Aidha, OWM-TAMISEMI imewasiliana na katibu tawala wa Arusha na amekubaliana na maelekezo ya kutenga Sh. 131 milioni kwenye bajeti ya 2011/12 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa ofisi hiyo iwapo Hazina haitatoa fedha hizo kwa mwaka wa fedha 2010/11.”

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: