Lowassa: Hii ni furaha ya muda


Mayage S. Mayage's picture

Na Mayage S. Mayage - Imechapwa 30 November 2011

Printer-friendly version
Jamvi la Weledi

VIKAO vikuu vya maamuzi vya Chama cha Mapinduzi (CCM) – Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC) vilivyofanyika wiki iliyopita, vimekubaliana kulirejesha suala zima la kuleta mageuzi ya kisiasa ndani ya chama hicho, maarufu kwa msemo wa kujivua gamba, katika kamati za usalama na maadili za ngazi ya tawi hadi taifa.

Huo umeelezwa ni uamuzi unaolenga kuchukua hatua dhidi ya wote waliohusika kukishushia hadhi chama hicho mbele ya jamii, kwa kujihusisha na mambo yanayokwenda kinyume na maadili ya uongozi, vikiwamo vitendo vya ufisadi, kwa kufuata taratibu na kanuni zilizowekwa na chama hicho tawala.

Kwa uamuzi huo, ni watuhumiwa wote, kuanzia ngazi ya tawi hadi taifa, wataitwa mbele ya kamati hizo katika ngazi husika kujieleza kabla ya hatua stahiki kuchukuliwa dhidi yao.

Wachambuzi wengi wa mambo, katika maoni yao, wamebeza maamuzi hayo ya NEC ya sasa, wakisema chama kimeshindwa au kimewaogopa kuwachukulia hatua wahusika.

Baadhi yao wamekwenda mbali zaidi kwa kusema, CCM na hasa mwenyekiti wake, Jakaya Kikwete, alikurupuka kwa kuasisi dhana hiyo na utekelezaji wake pasipo kufanya utafiti na kujiridhisha.

Katika nchi yenye demokrasia na uhuru wa kila mtu kutoa maoni yake, naamini yataendelea kusemwa mengi juu ya hicho kinachoitwa udhaifu wa CCM au wa mwenyekiti Kikwete katika kusimamia suala hili la kuleta mageuzi ndani ya chama kwa lengo la kukipatia uhai mpya na hivyo kuendelea kuaminiwa na umma.

Nimejifunza na kuelewa mambo kadhaa ya msingi, ambayo bila shaka kila mwana CCM anayetuhumiwa kwa tuhuma mbalimbali za kimaadili na yule mwenye ndoto za kumrithi Rais Kikwete mwaka 2015 anapaswa kutoyapuuzia, kwani kwa kufanya hivyo anaweza akajikuta anatwanga maji ndani ya kinu.

KUJIVUA GAMBA

Moja ya maazimio ya NEC ya CCM iliyokutana Aprili 10-11 mwaka huu, ilikuwa kwamba NEC imetakari na kukiri kuwa ndani ya chama hicho kuna mafisadi, na kwamba hao wamechangia kushusha haiba ya chama mbele ya umma wa Watanzania.

Kwa hiyo, kwa kutambua kuwapo kwa mafisadi, NEC ilitoa fulsa, kwanza kwa kila mtuhumiwa kujitathimini na hatimaye kuamua mwenyewe kujiondoa katika nafasi ya uongozi wa chama kwa hiyari yake.

Pili, iwapo watuhumiwa hawatachukua hatua kwa hiyari yao, chama kimlazimishe kwa kumvua uongozi.

NEC ya sasa imekiri kwamba mwitikio katika azimio hilo la Aprili, ulikuwa mdogo. Kimsingi, ni sawa na kusema hakuna lolote lililofanyika, watuhumiwa wote wameligomea azimio hilo.

Agizo la NEC ya sasa ni kwamba hatua zichukuliwe bila kuchelewa, kwa wathumiwa wote kuitwa mbele ya kamati za usalama na maadili ili kuwapa nafasi ya kujitetea kama kanuni na taratibu za chama zinavyoelekeza ili mwisho wa siku atakayepatikana na hatia, asilaumu utaratibu kwamba haukutoa haki hiyo.

Mpaka hapa siuoni ushindi wala ushujaa wa mmoja wa watuhumiwa wa ufisadi, ambaye wapambe wake walijazana Dodoma, wakakesha wakisherehekea kwa kula na kunywa kwa madai kwamba CCM ‘kimemgwaya’ kwa hatua yake ya kuamua kurejesha suala lake kwenye Kamati ya Usalama na Maadili ya chama na baadaye CC kwa utekelezaji.

Ni kweli CCM ya sasa, ni tofauti kabisa kwa udhaifu, tena kwa mbali na iliyokuwa chini ya Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi na hata ya Benjamin Mkapa.

CCM ya sasa, imejaa wasanii wengi wanaosema ndicho sicho. Ni vikao vyenye wajumbe ambao ni mateka wa dhambi ya ufisadi na kwa hiyo kila azimio jema kwa maslahi ya chama, linagusa mnyororo (chain) wa ufisadi.

Lakini pamoja na udhaifu huo, itakuwa ni makosa makubwa ya kisiasa kwa mwanasiasa yeyote ambaye kuwapo kwake, maslahi yake binafsi, maisha yake binafsi na familia yake, yanategemea chama hicho.

Mtu mweledi na makini, akifanya jambo la ovyo, watu watamshangaa, lakini mtu mjinga akifanya jambo la ovyo hakuna atakayeshangaa kwa sababu jambo lenyewe hilo limo ndani ya ujinga wake.

Maamuzi yoyote makubwa ya kisiasa huzingatia mazingira na muda. Mambo muhimu ya kisiasa, yasipofanyika katika mazingira stahiki na muda stahiki, matokeo yake yanaweza yasiwe mazuri.

Suala la utekelezaji wa kujivua gamba ndani ya CCM, lilikosewa tangu mwanzo. Utekelezaji wake ulipaswa kufanyika mara moja – pale ilipovunjwa sekretarieti na CC – hatua ambayo isingeweza mtafaruku wowote mkubwa ndani ya chama.

Kwa kutoa muda wa watuhumiwa wa ufisadi kujitathini na kujihukumu wenyewe, CCM ilikosea na inajua ilikosea. Ni kutokana na kukiri kosa hilo, ndiyo maana ya uamuzi wa sasa.

Inawezekana mbele ya kamati hizo, Kikwete anayeonekana dhaifu anaweza kuchukua hatua na kuvunja gamba lake. Anaweza kutumia kamati hizo kuwatimia wanaoitwa vigogo wasiogusika. Kamati hizi ni tofauti na mkusanyiko wa wajumbe wa NEC.

Lakini kuna jingine pia: Kwa mara ya kwanza katika historia ya vikao vya NEC ya CCM, maoni ya Edward Lowassa na wote waliomfuatia, yalikuwa yakisikika kila kona ya nchi na dunia kwa ujumla wake. Ni kutokana na kukuwa kwa tekronojia ya mawasiliano na habari.

Upo ushahidi usiotia shaka, kwamba baadhi ya wahariri katika vyumba vya habari jijini Dar es Salaam, walijua neno kwa neno aliloongea Lowassa kuliko mwandishi aliyetumwa na vyombo hivyo kufuatilia mkutano huo.

Ushahidi wa hili unaweza kuonekana katika baadhi ya magazeti yaliyotoka kesho yake, Ijumaa 25 Novemba 2011. Baadhi ya yamemnukuu Lowassa neno kwa neno mithiri ya mwandishi aliyemrekodi mtu aliyekuwa akihojiana naye katika tukio fulani.

Siku zote, katika vikao kama hivi vya NEC, tulizoea kupata habari za kunusanusa na nusu nusu, lakini siyo hotuba nzima kwa ukamilifu kama ilivyotokea kwa hili la Lowassa.

Sitaki kumhukumu Lowassa katika hili. Lakini niseme jambo moja: Kusikika “live” maoni yake aliyoyatoa NEC, ni kosa la kimaadili kwa chama chake; haliwezi kuwa lilitokea kwa bahati mbaya.

Kwa kifupi kabisa, haya ndiyo mambo niliyoona Dodoma. Kwamba ili CCM ipone hasira za wananchi mwaka 2015, lazima wanaowaita mafisadi wavuliwe gamba. Ikishindwa, itakumbana na hasira za wananchi. Je, wako tayari? Tusubiri tuone.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: