Lowassa na Kanisa Katoliki: Nani anamchafua huyu na kumtakasa yule?


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 29 February 2012

Printer-friendly version

SASA imeripotiwa rasmi kuwa waziri mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa atakuwa mgeni “maalum” katika harambee ya kuchagisha fedha kwa ajili ya Jimbo jipya la Katoliki la Ifakara. Harambee hiyo itafanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee.

Imeripotiwa pia kuwa harambee hiyo itahudhuriwa na maaskofu kadhaa wa kanisa hilo kubwa nchini. Hii yaonyesha umuhimu wa tukio hilo.

Kimsingi, umuhimu wa tukio huonekana kwa waliohudhuria. Mgeni rasmi ni kikolezo muhimu katika hafla yoyote.

Edward Lowasa ni jina kubwa na kwa hiyo kila likitajwa, lazima mijadala ianze. Mimi ni mmoja wa waathirika wa mijadala hiyo. Nimejiuliza, kati ya Lowassa na kanisa Katoliki, nani anamchafua mwingine na nani anamtakasa mwingine?

Taifa hili limo katika mgogoro mkubwa wa uongozi. Wanaojadili kama mimi wanaliita ombwe la uongozi. Kwa kuonyesha heshima kwa mkuu wa nchi, watu wengi wanajificha nyuma ya neno ombwe kueleza udhaifu wa kiongozi wetu wa nchi.

Wengine kwa kumstahi wanajilazimisha kuwalaumu wasaidizi na washauri wake, lakini kimsingi tuna rais mdhaifu kiuongozi na ambaye ameifanya taasisi ya urais iwe dhaifu na kupoteza heshima yake.

Rais huyu na udhaifu wake kwa sehemu kubwa alijengwa na kanisa Katoliki pale lilipomtangaza kuwa ni “chaguo la Mungu.”

Alikuwa ni Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Dk. Methodius Kilaini aliyetamka kuwa “Jakaya Kikwete ni chaguo la Mungu.”

Wakati huo Lowasa ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa mtandao uliomwingiza Kikwete madarakani mwaka 2005.

Kwa hiyo, Lowassa si mgeni sana katika siasa za ndani na nje ya kanisa Katoliki. Ninaamini ndiyo maana hakai mbali nalo kwa sababu anajua tamko la kanisa hilo linaweza kumfikisha mbali katika harakati zake za kuwa rais ajaye wa taifa hili.

Ni Lowasa aliyeonekana hivi karibuni katika harambee ya Kanisa Katoliki jijini Mwanza.

Maneno mengi yalisemwa baada ya harambee hiyo na watu wengi walidhani baada ya maneno yale, ama Lowasa angekuwa mwangalifu kutumia makanisa, au makanisa yangekuwa na uangalifu kumtumia Lowasa. Yote mawili hayajatokea, labda ujumbe haujafika sawa sawa.

Sehemu zote mbili zinahitajiana. Lowassa ana fedha – chafu na safi. Kanisa Katoliki lina ushawishi – mzuri na mbaya. Magwiji hawa wawili yaonekana wameamua kwa mara nyingine kutumiana ili kujinufaisha kwanza bila kujali maslahi mapana ya taifa letu.

Nina maana kuwa, Kanisa katoliki lipate fedha na kujenga majengo na Lowassa asafishwe na apate madaraka ya urais anaoulilia sana. Ebu turudie tena kuangalia sehemu zote mbili.

Lowasa ni “fisadi” pasipo shaka. Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanamwita fisadi, wapinzani wanamwita fisadi, bungeni anaitwa fisadi, yeye mwenyewe hajajiita fisadi lakini pia hajakana kama si fisadi.

Rais Kikwete hajamwita fisadi hadharani na pengine hawezi, lakini walio karibu naye wanasema anakosa usingizi kwa sababu ya Lowassa. Alimruhusu ajiuzuru kwa ahadi ya kumsafisha. Aliposhindwa kumsafisha, Lowassa akaamua kujisafisha na kutafuta namna ya kutimiza ndoto zake. Katika hili, hakuna anayemlaumu Lowasa kwa sababu ana haki ya kujisafisha kwa njia yoyote.

Rekodi ya Kanisa Katoliki katika vita dhidi ya ufisadi ina utata, sawa tu na rekodi za makanisa mengine. Ni kanisa lenye viongozi wanaokemea ufisadi hadharani bila woga.

Tumemshuhudia Mwadhama Kardinali Pengo akifikia hatua ya kusema yuko tayari kufa kwa kutetea ukweli. Amepokea vitisho kadha wa kadha na kwa hakika tumeshuhudia akisifiwa hata na viongozi wa serikali.

Rais Kikwete katika hafla ya kumpongeza Mwadhama Kardinali Pengo kutimiza miaka 25 ya uaskofu alimsifia sana kuwa ni mtu “asiyekurupuka” na anayejua kitu gani cha kusema kabla ya kukisema. Ni vigumu kuamini kuwa kualikwa kwa Lowasa katika harambee hii hakuna baraka za Mwadhama Pengo.

Tumeshuhudia pia baadhi ya mapadre wa kanisa Katoliki wakiwafungia sakramenti baadhi ya waumini wake kwa kuwaalika viongozi wa kisiasa katika matukio kadhaa kwenye parokia zao.

Viongozi wa kisiasa hasa wasiotoka katika chama tawala hawaruhusiwi kualikwa kama wageni rasmi katika halfa za kanisa katoliki. Sababu zinazotolewa na mapadre wanaowaadhibu waumini wao ni kuwa “wasichanganye dini na siasa.” Kwa hili la kumwalika Lowasa ni vigumu kuamini kuwa si kuchanganya dini na siasa.

Labda tufikiri zaidi. Kuna ubia gani kati ya CCM na kanisa Katoliki katika vita dhidi ya ufisadi nchini?

Kanisa Katoliki linajua wazi kuwa utajiri wa watu wanaowakaribisha kuongoza harambee umejaa damu na jasho la watu maskini. Utetezi ambao kanisa hilo limekuwa likiutoa kuwa mafisadi kama waumini wana haki ya kuja kanisani na kuwa haliwezi kuwatenga hauna mantiki.

Mbona kanisa linawatenga wazinzi, vibaka na hata waumini safi kwa kosa la kuwakaribisha parokiani baadhi ya wanasiasa wasio na hela nyingi?

Mradi huu kati ya Lowasa na makanisa una maana moja kuu tu. Ni mradi wa kusafishana. Kanisa linamsafisha Lowasa au watuhumiwa wa ufisadi wengine ili lipate fedha; na mafisadi wenye madaraka wanalisafisha kanisa hilo lenye historia na matendo mengine mengi ya aibu.

Vinginevyo haingii akilini, kanisa hilo hilo kupitia maandiko yake na mafundisho lipige vita ufisadi na hapo hapo liwakumbatie mafisadi na kutamani fedha zao.

Kama ingekuwa kuwa fedha ya mafisadi inaingia kanisani kwa njia ya zaka, tungesitisha malalamiko yetu, lakini sasa kanisa limeamua mchana kweupe kuwaibia Watanzania kupitia fedha za harambee za mafisadi. Mafisadi wanajaribu kutakasa fedha zao chafu kupitia makanisa.

Niliwahi kusema huko nyuma kuwa CCM inawachukia mafisadi lakini inapenda fedha zao; sasa kanisa katoliki linajitangaza  kuwachukia mafisadi na ufisadi, lakini linatamani matunda ya ufisadi.

Inawezekana fedha za Lowasa ni zile zile za Richmond, Dowans, EPA na nyinginezo ambazo zimekosesha huduma za jamii kama vile madawa hospitalini.

Kuibwa kwa fedha hizo ndiko kulikosababisha migomo vyuoni, ndiko kulikosababisha mahakama kukosa fedha za kutosha za kutoa haki kwa wanyonge; kumepandisha bei ya umeme, kumewanyima maji safi mamilioni ya wananchi na kupandisha gharama za maisha kwa walalahoi.

Fedha za Lowasa atakazotoa katika harambee ni hizo hizo zinazokosekana katika hazina ya taifa; yaani ni kama Edward Lowasa kaiba hazina kupeleka katika harambee ya kanisa Katoliki na kanisa linapokea na kutakasa uovu huo.

Yawezekana hukumu yangu hii ikawa na makosa, lakini kanisa Katoliki likumbuke kwa makini kuwa siku za karibuni limelazimika kulipa mabilioni ya fedha kufidia maamuzi yake ya zamani ya kukumbatia uovu wa kashfa za ngono.

Kukumbatia uovu kwa kujua ni dhambi inayoweza kulitafuna kanisa hili kwa muda mrefu.

Kwanza, kitendo hicho kinalinyima kanisa nguvu ya ujasiri ya kukemea uovu, na pili kunalifanya kanisa kuwa mtumwa wa uovu huo.

Madhara yanayosababishwa na ufisadi hapa nchini hayana tofauti na madhara ya kashfa za ngono zilizofanywa na mapadre huko nyuma na kuligharimu kanisa fedha nyingi.

Kuna siku wahanga wa ufisadi hapa nchini, wajukuu na vitukuu, watasimama na kudai fidia si kutoka kwa serikali tu, bali hata mashirika na madhehebu yanayokumbatia vitendo hivyo.

Kwa kumtakasa Lowasa, kanisa linajichafua kwa gharama ndogo ya harambee kupitia chakula cha hisani.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: