Lowassa kuibukia bungeni


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 01 November 2009

Printer-friendly version
'Majemedari' wake wajipanga
Kikwete huenda akahusishwa

EDWARD Lowassa, aliyekuwa waziri mkuu, anatarajiwa kuibukia katika mkutano ujao wa Bunge na kupasua kile kinachoitwa "ukweli kuhusu utata wa mkataba wa Richmond," imefahamika.

Taarifa kutoka vyanzo vya kuaminika ndani ya kambi yake na katika serikali zinasema Lowassa amekuwa akishinikizwa na marafiki zake kuweka “mambo hadharani” kwa lengo la kujinasua kwenye kitanzi cha Richmond.

Mkutano huo wa Bunge la Muungano, unaoanza Jumanne ijayo mjini Dodoma, unakuwa muhimu kwa kuwa ndimo serikali iliahidi kuwasilisha ripoti ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge juu ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond Development Company (LLC).

Suala la Lowassa kupasua ukweli linakuja karibu mwezi tangu atamke kuwa yeye na Rais Jakaya Kikwete ni marafiki wa kweli, ambao hawakukutana njiani na kwamba hakuna wa kuwatenganisha.

Alisema yeye na Kikwete wametoka mbali na urafiki wao, “hauwezi kuvurugwa na kikundi kidogo cha watu.”

Hata hivyo, kauli ya Lowassa ilitolewa siku mbili tangu Rais Kikwete aseme, mapema mwezi uliopita, kwamba, “sina ndugu wala rafiki” katika vita dhidi ya rushwa na ufisadi.

Rais alikuwa akijibu swali la mmoja wa wananchi, katika kipindi cha maswali na majibu ya papo kwa papo kwenye televisheni, ambaye alimtuhumu kulinda marafiki zake wanaotuhumiwa kwa ufisadi.

Rais Kikwete alinukuliwa pia akisema serikali yake ina mpango wa kutafuta msaada wa kitaalamu kutoka vyombo vya kimataifa ili kujiridhisha kuhusu utata wa zabuni iliyotolewa kwa kampuni ya Richmond.

Kampuni ya Richmond ambayo ilipewa zabuni ya kuagiza mitambo ya kufua umeme wa dharura mwaka 2006, ndiyo chanzo cha kujiuzulu kwa Lowassa na mawaziri wengine wawili.

Mawaziri waliojiuzulu ni Nazir Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha kutokana na kuhusika kwao katika mchakato wa mkataba wa Richmond ambao Rais Kikwete amebainisha kuwa ulijaa uzembe na ubabaishaji.

Wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema kauli ya Lowassa ilikuwa “inatoa salamu” kwa Kikwete, kwamba siku atakayopata nafasi ya kuzungumza, hatakuwa na simile – ataanika kila kitu hadharani.

Haikufahamika iwapo “kuanika kila kitu” kunamaanisha kumhusisha Rais Kikwete katika kashfa ambayo tayari bunge limeitolea maamuzi.

MwanaHALISI linaweza kuthibitisha kwamba Lowassa na wapambe wake wako mbioni kukamilisha wanachoita, “mkakati wa kusafisha njia kuelekea kilele cha uongozi.”

Chanzo cha habari cha gazeti hili kimemnukuu mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba akisema, “Ni lazima Lowassa apasue jipu katika mkutano huu.”

Serukamba, mmoja wa wabunge wanaotajwa kuwa ni watetezi wakubwa wa Lowassa ndani na nje ya bunge, anasema katika mahojiano hayo, “Tunategemea hivyo na kila kitu kitakwenda kama tulivyopanga.”

Mbunge Serukamba alikuwa akijibu swali aliloulizwa juu ya hatua waliyofikia kuhusu mpango wa Lowassa kuzungumza “kutoboa kila kitu bungeni.”

Kambi ya Lowassa inasemekana kupata nguvu mpya baada ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumsulubu Spika wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta kwa madai kuwa anasababisha “kuchafuka kwa hali ya hewa” bungeni na kudhoofisha serikali.

Uchunguzi wa awali wa mkataba wa Richmond ulibainisha kuwapo kwa uzembe, jambo ambalo lilibainishwa na Kamati Maalumu ya Bunge ya Nishati na Madini, iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela (CCM), Dk. Harrison Mwakyembe.

Wakati Lowassa akipanga kujisafisha, mmoja wa wajumbe wa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mkataba huo amesema wanasubiri kauli yake “kwa hamu kubwa.”

“Unasema amepanga kulipuka bungeni? Ha, ha! Tunamsubiri. Nakuhakikishia hapatatosha,” alisema akitoa kicheko chembamba.

Alisema, “Kwa kweli mdogo wangu, nakwambia ataumbuka; maana hata zile taarifa za ndani, ambazo hazikuwa zimepata mwanya wa kutoka, zitawekwa kwenye paa la nyumba.”

Sakata la Richmond linatarajiwa kuchukua sura mpya katika mkutano huu wa bunge iwapo serikali itatoa taarifa ya utekelezaji, kama ilivyoahidi na baadaye kujadiliwa na wabunge.

Ni katika hatua hiyo, taarifa zinaeleza, wapambe wa Lowassa wanataka kujipanga ili kushawishi wabunge kuwa kigogo huyo “hakuhusika” katika kashfa ya Richmond.

Mkataba wa Richmond ndio ulisukuma Lowassa nje ya uwaziri mkuu hapo Februari mwaka 2008. Tangu hapo, Lowassa na wapambe wake wamekuwa wakijitahidi bila mafanikio kutaka kurejesha hadhi hiyo ya kisiasa.

Taarifa zinasema tayari kuna mkakati wa kupanga “idadi nzuri” ya wabunge ili wakati Lowassa anazungumza, waweze kumshangilia kwa kupiga makofi ili kuzima nguvu ya “wapinzani wake.”

“Ndiyo, tumeshapata zaidi ya wabunge 100 wanaotuunga mkono. Tunataka pale Lowassa anapozungumza asitokee mtu wa kutujibu. Na kila anayetaka kujibu akutane na kishindo chetu,” mbunge mmoja alimueleza mtoa taarifa.

Kuna taarifa kuwa kundi la Lowassa limepanga kutumia mbinu iliyotumika katika NEC kuzima sauti na ushawishi wa wabunge wanaopinga mkataba huo wa Richmond.

Hata hivyo, mjumbe mmoja wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini aliliambia MwanaHALISI kwamba ni lazima Lowassa aje na utetezi wa nguvu, vinginevyo anaweza kujikuta anazama badala ya kuibuka.

Kamati Teule iliyochunguza Richmond, ilitoa mapendekezo 23, yakiwamo ya kuwachukulia hatua waliohusika kuibeba kampuni hiyo kinyume cha taratibu na hata sheria za nchini.

Iwapo Lowassa atapata fursa ya kutimiza azma yake, kuna uwezekano wa kuchafuka tena kwa hali ya hewa bungeni kutokana na kile ambacho baadhi ya wabunge wanadai “kutokubali kusafisha watuhumiwa.”

Kundi la Lowassa linataka kutumia kauli ya Rais Kikwete kwamba alizuia waziri wake mmoja kufanya malipo ya awali kwa Richmond akihofia “inaweza kuwa kampuni ya mfukoni.”

Kwa mujibu wa mtoa taarifa, kauli hiyo ya rais inatafsiriwa kusema kuwa Lowassa alishirikisha kiongozi huyo wa nchi katika “hatua zote za kufikia mkataba” ambao ulikuja kufahamika kuwa wa upendeleo na unaovunja kanuni na sheria.

“Sisi hatujali nani anaumia na nani ananufaika. Tulichopanga ni kupasua jipu,” anasema mbunge huyo kutoka kambi ya Lowassa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: