Lowassa kutinga kortini


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 22 September 2009

Printer-friendly version
Ni katika sakata la Richmond
Uswaiba na Kikwete majaribuni
MBUNGE wa Monduli, Edward Lowassa

MBUNGE wa Monduli, Edward Lowassa, aweza kufikishwa mahakamani kwa makosa ya kuingiza nchi katika mkataba wa kinyonyaji kati ya serikali na kampuni ya Richmond Development Company (LLC), MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa kutoka serikalini zinasema Lowassa aweza kufikishwa mahakamani kujibu, pamoja na mengine, tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.

Wiki mbili zilizopita, Rais Jakaya Kikwete alinukuliwa akisema serikali yake inataka kumaliza kabisa suala la Richmond kwa kuruhusu kufanyika uchunguzi wa kimataifa ili kubaini iwapo kulikuwa na vitendo vya rushwa wakati wa kupitisha mkataba huo.

Alisema katika vita dhidi ya rushwa, hana rafiki wala ndugu, na kwamba serikali yake iko tayari kuleta hata wapelelezi wa kimataifa kufanya kazi ya uchunguzi katika mradi wa Richmond ili kuweza kubaini ukweli.

Kwa mujibu wa kauli ya rais, watuhumiwa wa ufisadi katika Richmond waweza kufikishwa mahakamani. Hawa ni pamoja na Lowassa, aliyekuwa waziri mkuu; Nazir Karamagi, Dk. Ibrahim Msabaha waliokuwa mawaziri wa Nishati na Madini na baadhi ya watendaji serikalini.

Wenye uwezo wa kufanya hivyo ni pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) au wote wawili kwa ushirikiano wa wataalam kutoka nje ya nchi ambao Kikwete ameahidi.

Rais alimwambia muuliza swali kwa njia ya simu, “Chombo chetu kimeshindwa kubaini kama kulikuwa na vitendo vya rushwa ya moja kwa moja wakati wa zabuni ya Richmond.”

Alisema, “Nimetoa ruhusa kwa chombo chetu kushirikiana na taasisi nyingine za nje kuchunguza; nimemwagiza pia Katibu Mkuu Kiongozi, kufuatilia suala la maofisa waliohusika katika sakata hili.”

Hata hivyo, rais alisema katika mkutano ujao wa bunge (Novemba), serikali itakuwa na “majibu ya kuridhisha.” Hakuyataja.

Uchunguzi wa awali kwa Richmond, uliofanywa na Kamati Maalumu ya Bunge ya Nishati na Madini, ulibainisha kuwepo uzembe, utovu wa uadilifu na maadili.

Hata hivyo, TAKUKURU ambayo katika hatua za mwanzo za kufumuka kwa sakata la Richmond ilisema haikuwa imeona kosa la jinai ya rushwa, imekuwa ikikiri katika siku za karibuni kuwa kwa sheria ya sasa, inaweza kuanza upya uchunguzi na huenda ikapata matokeo tofauti.

“Chombo chetu kimeshindwa kubaini kama kulikuwa na vitendo vya rushwa ya moja kwa moja wakati wa zabuni ya Richmond.

Rais “Nimetoa ruhusa kwa chombo chetu kushirikiana na taasisi nyingine za nje kuchunguza; nimemwagiza pia Katibu Mkuu Kiongozi, kufuatilia suala la maofisa waliohusika katika sakata hili,” alisema rais.

Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza Richmond, ilitoa mapendekezo 23 kwa serikali, yakiwamo ya kuwachukulia hatua za kisheria waliohusika kuibeba Richmond ambayo haikuwa na fedha, utaalam wala hadhi ya kupewa kazi ya umma.

Lakini wakili wa Mahakama Kuu, Tundu Lissu ameliambia gazeti hili kuwa serikali inaweza kufungulia kesi watuhumiwa wa Richmond kupitia sheria zilizokuwapo kabla ya sheria mpya ya TAKUKURU.

Alisema, “Hata kama TAKUKURU haikuwa na meno wakati ule, lakini sheria ya uhujumu uchumi ilikuwapo. Hii ilitungwa mwaka 1984 na imekuwa ikitumika kwa miaka mingi sasa.”

Akiongea kwa kujiamini, Lissu alisema Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) anaweza kutumia sheria hiyo kufungua kesi ya uhujumu kwa watuhumiwa, iwapo atajiridhisha kuwa kilichofanyika ni jinai inayoangukia katika uhujumu uchumi.

Lissu amesema sheria hii imetungwa mwaka 1984 na inampa mamlaka DPP kufungua mashitaka ya aina hiyo.

Lakini anasema kwa upande wa TAKUKURU, kilichokosekana wakati huo ni kutokuwapo makosa ya kuhujumu uchumi katika sheria ya taasisi hiyo na “siyo kwamba serikali yote haikuwa na uwezo wa kushitaki.”

Kuhusu uwezekano wa watuhumiwa kushitakiwa sasa wakati makosa hayo yalitendeka mwaka 2006, sheria mpya ikiwa bado haijapitishwa, Lissu anasema, “Kilichokosekana wakati huo si sheria kuhusu jinai hiyo, bali TAKUKURU kutokuwa na nguvu ya kisheria ya kushitaki.”

Amesema kutokuwepo nguvu ya kisheria kwa TAKUKURU “hakuzuii vyombo vingine vya kisheria kuchukua mkondo wake” na kuongeza, “hakuna mashaka kwamba kilichofanyika katika Richmond ni jinai ya uhujumu wa uchumi.”

Richmond ambayo ilipewa zabuni ya kufua umeme wa dharura, ndiyo chanzo cha kujiuzulu kwa Lowassa, Karamagi na Msabaha.

Wakati Lowassa alijiuzuru waziwazi bungeni (hakustaafu kama anavyodai na anavyobebwa na vyombo vya habari), Msabaha na Karamagi walitoswa wakati Rais Kikwete alipovunja baraza la mawaziri na kutowarudishia nyadhifa zao.

Lakini siku nne baada ya Rais Kikwete kusema kuwa katika sualala Richmond hatakuwa na ndugu au rafiki, amebainisha kwamba kulikuwa na uzembe kwa baadhi ya wahusika.

Akijibu maswali ya moja kwa moja kupitia vyombo vya habari, Rais Kikwete alisema katika vita dhidi ya ufisadi hana rafiki wala ndugu.

Lakini siku nne baada ya Kikwete kusema kwamba katika vita dhidi ya ufisadi hatakuwa na ndugu wala rafiki, Lowassa aliibuka na kusema, “mimi na Kikwete hatukukutana barabarani.”

Alisema, “Huyu bwana mkubwa (Kikwete) hatukukutana barabarani. Hivyo watu hawawezi kutuvuruga barabarani.”

Kauli ya Lowassa ilibeba maana tatu kuu: Kumkumbusha Kikwete kuwa wametoka mbali; au baada ya kuona mwenzake amepania, basi naye akaamua kujibu mapigo kwa kuwa anajua mengi; au anahaha kujiokoa.

Kauli ya rais ilikuwa na kila sababu ya kumtikisa Lowassa. Aliliambia taifa kwa njia ya redio, televisheni na magazeti kuwa katika siku za karibuni, kesi tatu kubwa zitafikishwa mahakamani.

Ahadi hii na kauli kwamba hatakuwa na udugu na urafiki katika suala la Richmond, vinamkosesha Lowassa usingizi.

Baadhi ya wachambuzi wa kisiasa hata hivyo, wanasema kama kuna mpango wa kumfikisha Lowassa mahakamani, basi utakuwa ni mpango maalum wa “kumsafisha.”

Wanasema kama DPP alikataa kumtuhumu na kumfikisha mahakamani; TAKUKURU ilitumia visingizio na sasa rais anasema kuwa ataweza hata kutumia wataalam kutoka nje kushughulikia Richmond, basi “Lowassa ataachiwa tu.”

Hata hivyo, mpango wowote wa kumsafisha Lowassa kwa njia ya mahakama, sharti umhusishe mwenyewe, kwani unaweza kuzima, mara moja na milele, matamanio yake ya kisiasa.

“Lowassa anataka urais, ama mwaka 2010 au 2015; na kesi za mahakamani hazitabiliki. Kesi ikigota kwa miaka minane, kwa njia ya kumnusuru, basi muda wake wa kuwa anavyotaka utakuwa umeyoyoma,” ameeleza mbunge mmoja wa CCM.

Waziri wa Utawala Bora, Sophia Simba aliliambia gazeti hili juzi Jumatatu kuwa ni kweli TAKUKURU walisema hawakuona rushwa, lakini serikali inatafuta kufanya uchunguzi zaidi.

Amesema ni kweli pia kuwa waliohusika katika mradi wa Richmond hawakuwa waangalifu; “walichukua kampuni bila kuichunguza.”

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Edward Hoseah hakupatikana kwa maelezo kuwa yuko safarini China. Lakini ofisa uhusiano wa taasisi hiyo, Lilian Mashaka hakutaka kujibu maswali. Alisema, “Utaratibu wetu ni kutuandikia maswali ili tuwajibu. Basi.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: