Lowassa, Msabaha hapatoshi


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 28 October 2009

Printer-friendly version
Ni katika sakata la Richmond
Kila mmoja apanga kujinasua
Ibahim Msabaha

HATMA ya Edward Lowassa kujinasua kwenye kashfa ya mkataba tata wa kampuni ya Richmond, ipo mikononi mwa Dk. Ibrahim Msabaha, MwanaHALISI limeelezwa.

Dk. Msabaha ametajwa kuwa mwenye taarifa juu ya kila hatua na tukio katika kukamilisha mkataba wa Richmond; kampuni ambayo ilipewa tenda ya kuzalisha umeme huku ikiwa haina fedha, wataalam wala ofisi.

Taarifa za ndani zilizopatikana wiki moja baada ya gazeti hili kufichua mpango wa Lowassa kutumia mkutano wa sasa wa Bunge kujisafisha na ikibidi kumhusisha hata Rais Jakaya Kikwete, zinasema “mwokozi au mwangamizaji wa Lowassa ni Dk. Msabaha.”

“Ndiye mwenye uamuzi. Lazima wamshike kama mboni ya jicho. Aweza kuamua kumuopoa au kumtosa. Itategemea uhusiano wao wa sasa,” ameeleza mtu wa karibu wa Lowassa.

Mjadala juu ya kampuni ya Richmond Development Company (LLC), unatarajiwa kufanywa wiki ijayo mara baada ya serikali kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya bunge.

Dk. Msabaha, waziri wa zamani wa nishati na madini aliyejiuzulu nafasi yake kutokana na kashfa ya Richmond, ni mtu muhimu pia hata kwa upande wa serikali.

Aidha, mawasiliano ya siri miongoni mwa watendaji wa serikali ambayo yamevujishwa katika baadhi ya vyombo vya habari nchini, tayari yamewaweka Lowassa na Msabaha katika hali ya “urafiki wa mashaka.”

Wakati Lowassa alimwitaji Msabaha kuficha kila alichokijua juu ya mkataba, upande wa serikali ambao unatishiwa kuingizwa kwenye kashfa, unataka aiokoe kwenye sakata hili.

Tayari taarifa zimeonyesha jinsi Msabaha alivyokuwa “mesenja” kati ya waziri mkuu, wizara yake ya nishati, Shirika la Umeme (Tanesco) na bodi ya wakurugenzi ya shirika hilo.

Nyaraka zipatazo saba ambazo zimewekwa saini na Msabaha, zinaonyesha kitu kimoja; kwamba alikuwa anaagizwa na Lowassa na anasisitiza msimamo wa “waziri mkuu” bila kutetereka.

Kwa mfano, katika barua ya 12 Aprili  2006 yenye Kumb. CDB 88/286/01 kuhusu mashine za kukodi, Msabaha anaelekeza kwa Balozi Fulgence Kazaura, mwenyekiti wa bodi ya Tanesco kufuata maamuzi ya waziri mkuu.

“…Pasiwe tena na picha kama vile menejementi ya Tanesco imerejeshewa kazi hiyo, maana huko kutakuwa kukiuka maagizo ya mheshimiwa waziri mkuu,” anaandika Msabaha.

Alikuwa akionya juu ya kuingiliwa kwa Kamati ya waziri mkuu iliyoteuliwa kushughulikia suala la Richmond na kueleza kuwa yote yanapaswa kufanywa “kwa kadri Kamati inavyoona inafaa.”

Kamati ya waziri mkuu ya kushughulikia suala la mashine za umeme za Richmond ilihusisha katibu mkuu wa hazina; katibu mkuu wizara ya nishati na Madini na mwanasheria mkuu wa serikali.

“Nadhani hatukuelewana vizuri,” anaandika Msabaha na kuongeza akimwandikia Kazaura, “Suala la kushughulikia gas turbines za kukodisha lilishashughulikiwa na mheshimiwa waziri mkuu.” Yeye aliliona kama “baba mkwe.”

Imedhihirika kuwa kuanzia pale ilipoanza kunong’onwa kuwa Richmond yaweza kuwa bomu, Msabaha alianza kupeleka nakala za mawasiliano yake kwa rais.

Haikufahamika mara moja rais alikuwa anatoa maoni gani juu ya kile alichokuwa akipelekewa taarifa juu yake.

Hata hivyo, Rais Kikwete akijibu swali na mwananchi kwa njia ya televisheni, miezi miwili iliyopita, alisema alizuia waziri wake kulipa Richmond kwa kuwa “inaweza kuwa kampuni ya mfukoni.”

Taarifa zinasema ni kwa uzito huu wa Msabaha, kambi ya Lowassa imekuwa ikimpigia magoti ili asiweze kutoa siri ya jinsi Lowassa alivyoshiriki katika mkataba huo.  

“Nakuambia, kina Lowassa wanahaha ili kumzuia Msabaha asizungumze. Maana Msabaha anajua kila kitu na hivyo siku akiamua kutoka hadharani, itabidi Lowassa afiche sura yake,” kimesema chanzo cha habari ndani ya serikali.

Mjadala juu ya Msabaha kuokoa au kuzamisha Lowassa pale (Lowassa) atakapoibuka kujitetea, umekuja mwaka mmoja tangu mbunge huyo wa Kibaha Mjini atishie kuweka hadharani kile kinachoitwa, “Siri ya Richmond.”

Taarifa za Msabaha kutishia kuanika kilichotendeka zilisikika kwa mara ya kwanza wiki moja baada ya Lowassa kukana kuhusika na mkataba wa Richmond.

Kanusho la Lowassa lilitolewa jimboni kwake, Monduli mkoani Arusha, wiki moja baada ya kujizulu nafasi ya waziri mkuu. Alinukuliwa akisema ameponzwa na Msabaha na watendaji wengine serikalini.

“Kama siyo busara za mmoja wao katika kambi ya Lowassa; kuingilia kati na kumtuliza Msabaha, angekuwa amelipuka zamani,” ameeleza mtoa habari.

Taarifa za ndani ya serikali zinadai hata kuondolewa kwa Msabaha katika wizara ya nishati na madini, na nafasi yake kuchukuliwa na Nazir Karamagi, kulitokana na tabia yake hasa alipoanza kutilia mashaka mkataba wa Richmond.

Hata hivyo, nyaraka mbalimbali ambazo MwanaHALISI imeona, zinaonyesha kazi yote ya kusimamia, kuidhinisha na kupitisha mkataba wa Richmond ilifanywa chini ya uangalizi wa waziri mkuu.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, kile kinachoelezwa kuwa tahadhari ya Lowassa juu ya mkataba huo, kinavunjwa na barua iliyoandikwa na Lowassa mwenyewe.

Wakati Lowassa anamwandikia Msabaha ajiridhishe kuwa Richmond itaweza kutekeleza kazi zake, tayari kampuni hiyo ilikuwa imepewa mkataba.

Katika barua hiyo ya 21 Septemba 2006, waziri mkuu anaonyesha kumpa Msabaha kazi nje ya ofisi ya serikali kwa kumtaka “kufuatilia kwa karibu” ili kuhakikisha walioomba mkataba na wakapewa kwa nguvu ya serikali, wanaingiza mitambo ya umeme nchini.

Mkataba kati ya serikali na Richmond ulisainiwa 23 Juni 2006, wakati barua ya Lowassa iliandikwa miezi mitatu baadaye.

Kwa kipindi chote cha kusubiri mashine za umeme, mawaziri wa nishati, Msabaha na Karamagi walifanya kazi kama ya “maofisa uhusiano” wa Richmond, kwa kuisemea hata ilipokuwa haina la kujitetea kuhusu kuchelewa kuzalisha umeme.

“Barua hii ya Lowassa ni feki. Aliiandika wakati tayari serikali imeshafunga mkataba na Richmond na baada ya kuona mambo yameanza kuharibika,” ameeleza waziri anayejua vema mkondo wa mkataba wa Richmond.

Amesema Msabaha anayajua yote haya na kuongeza, “Mtafute akueleze.” Msabaha hakuweza kupatikana kwa simu yake ya mkononi. Iliita bila kupokelewa.

Madai kwamba Lowassa alikuwa akipeleka taarifa kwa rais kwa kila hatua, haikuweza kuthibitishwa, kwani hata barua ya kutaka Msabaha achukue tahadhari, ambayo uhalali wake unatiliwa mashaka, haikunakiliwa kwa rais.

Hata hivyo, barua ya Lowassa imejaa kila aina ya utata, kuanzia tarehe iliyoandikwa, mahali ilipoandikwa na ilipopatikana.

Wakati andishi hilo linaonekana lilitoka Dodoma, S.L.P. 981, lilipokelewa hukohuko Dodoma kupitia Fax Na. +255 026 2331955.

Uthibitisho mwingine wa nafasi ya Lowassa katika sakata la Richmond ni barua ya Msabaha ya 13 Julai 2006 ambayo inamsisitiza katibu mkuu wa wizara ya nisahati na madini “kuheshimu maagizo ya waziri mkuu” Lowassa.

Lakini kuzagaa kwa taarifa hizi mpya na kuwapo kwa taarifa kwamba Msabaha anaweza kuibukia bungeni ili “kuanika ukweli,” kunaweza kuvuruga kabisa mipango yake.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: