Lowassa naye amewaonea wengi


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 04 August 2010

Printer-friendly version
Gumzo
Edward Lowassa

NIMEBAHATIKA kusoma makala mbili katika gazeti lako zinazomzungumzia mwanasiasa aliyekamilisha kutumikia ubunge jimboni Monduli, Edward Lowasa kuhusiana na kile kinachoitwa, “Lowassa na sakata la Richmond."

Sitaki kurudia hoja kuu zinazothibitisha kwamba Lowassa hakuonewa. Hii ni kwa sababu, Lowassa mwenyewe anafahamu fika hakuonewa.

Lowassa anasema, "hakufanya kosa hata moja kwenye suala la Richmond na kuwa hata tukimwamsha leo usingizini atarudia maamuzi yaleyale kwa namna ile ile.”

Mimi si msomi, lakini kwa uelewa wangu mdogo, hii ni jinai. Kwamba alifanya vile alivyofanya kwa makusudi; alielewa alichokuwa anakifanya – kuliingiza taifa kwenye hasara ya Sh. 152 milioni kwa siku. Kwa mwaka na nusu, sijui ni bilioni ngapi!

Kwamba haikuwa ajali, kama Rais Jakaya Kikwete alivyotuaminisha Watanzania! Kibaya zaidi, hata akipewa tena nafasi ya waziri mkuu na kukatokea tatizo kama lile, atatufanya ‘kitu mbaya’ kwa staili ileile! Jamani, hii si jinai?

Huyu mtu hapaswi kukamatwa? Tafadhali wanasheria nisaidieni. Mchungaji Mtikila na wengine mko wapi katika hili? Huyu si wa kufunguliwa mashtaka kweli? Watanzania tutaendelea kuwa "kichwa cha mwenda wazimu" mpaka lini?

Lowassa bado anadai na anaendelea kusisitiza kuwa amedhalilishwa sana, amefadhaika sana, ameonewa sana, na hakutendewa haki.

Yote haya hayana chembe ya ukweli kama ulivyothibitisha kwenye makala zako; pamoja na ilivyothibitishwa na Bunge lenyewe – kwamba hakuonewa kwani alipewa nafasi, tena nzuri tu; na ni uungwana kabisa.

Lakini hebu tujiulize ni kweli "alionewa, alidhalilishwa, na hakutendewa haki", kama machozi yake ya damu yanavyotiririshwa?

Je, yeye mwenyewe amewafanyia wangapi vivyo hivyo?

Tangu aanze kazi CCM akiwa Shinyanga na Arusha; alipokuwa Mkurugenzi wa AICC; Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Mzee John Malecela ni shahidi); Waziri wa Ardhi; Waziri wa Maji; na hatimaye kipindi chake kifupi cha Uwaziri Mkuu; amedhalilisha, kuwaonea, kuwafedhehesha na kutowatendea haki wangapi?

Leo hii tukisema wajitokeze, mbona itakuwa aibu na fedheha kubwa.

Nitaonyesha maeneo machache ya vitendo hivyo vya aibu na manyanyaso aliyofanya Lowassa.

Ukianzia watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, nenda kwa aliyekuwa DC wa Nyamagana, mama aliyekuwa DED wa Same, Mhandisi wa Manispaa ya Temeke, wakuu wa idara na watumishi wa ngazi za juu, kati na za chini – wote hawa waliathirika kupindukia.

Lakini hata wakuu wengine wa wilaya na mikoa; mawaziri na manaibu wao; makatibu wakuu na wakurugenzi mbalimbali; na hata watumishi ofisini kwake mwenyewe – aliwafanyia hivyo anavyolalamika kufanyiwa. Ah, mkuki kwa nguruwe!

Lakini huyo Rais wa kumpa tena Lowassa uwaziri mkuu ni nani? Hajitakii mema? Atafanya tena "majaribio?" Atasimulia tena kuwa "ajali ya kisiasa"? Ataendelea kupuuza maoni ya Mwalimu Nyerere?

Ataendelea kudharau ushauri wa Benjamin Mkapa, Mzee Ali Hassan Mwinyi, marehemu Rashid Mfaume Kawawa, Kingunge Ngombale-Mwiru kuhusu uteuzi huo mbovu?

Bunge gani litakalopitisha jina hilo? Bado watakuwepo maswahiba kama "Bangusilo" yaani Dk. Ibrahim Msabaha, Nazir Karamagi, Arthur Mwakapugi, na mwenyekiti wa bodi ya Tanesco? Je, Dk. Edward Hoseah atakubali tena kuandika ripoti tata kama ile ya awali kuhusu mkataba wa Richmond?

Lowassa anadai kuwa kuna watu (sijui ni kina Dk. Harrison Mwakyembe, Mizengo Pinda, Samwel Sitta au nani?) walikuwa wanautaka uwaziri mkuu wake. Hivi waziri mkuu anapatikanaje, kwa kuutaka?

Naomba waliowahi kushika nafasi hizo waeleze Watanzania; Dk. Salim Ahmed Salim, Joseph Sinde Warioba, Malecela, Cleopa Msuya na Frederick Sumaye.

Pia marais Mwinyi, Mkapa na Jakaya Kikwete watueleze jinsi anavyopatikana waziri mkuu ili waziri mkuu mtarajiwa wa Novemba aanze "kushughulika."

Kinachonikera zaidi mimi ni pale kila Lowassa akiwa Monduli, wakati wote mbaya wake ni Mwakyembe; kwenye Bar, mikahawa, vijiweni kote, anamlaumu Dk. Mwakyembe!

Inaelekea mpaka leo haamini kuwa alifukuzwa na Bunge siyo Dk. Mwakyembe. Sijui bwana huyu yukoje, mtu mmoja, tena si yule aliyekuteua, atakufukuzaje uwaziri mkuu?

Kwa kumbukumbu zangu, siku ile ya Lowassa kuachia ngazi – ukiacha wabunge wachache sana kama kina Andrew Chenge, Peter Serukamba, Karamagi, Dk. Msabaha na Spika Sitta aliyeonekana kuchanganyikiwa (mkanda unaonyesha hata leo) – Bunge zima lilishangilia.

Pale Dodoma, Dar es Salaam, na nchi yote ilizizima kwa vifijo, shangwe na vigelegele. Lowassa hajiulizi kulikoni? Wote hao waliutaka uwaziri mkuu wake?

Kuna maelezo yanayotolewa kwamba Lowassa hana mtu wa kumlaumu isipokuwa yeye mwenyewe. Sikubaliani na "shule" hii.

Naona hata yeye mwenyewe hapaswi kujilaumu wala kulaumiwa na mtu yeyote. Kwa nini? Kwa kuwa, kwa sisi tunaomfahamu kiuongozi, Lowassa hakarabatiki. Ukilazimisha mtafedheheka wote. Ndiyo maana aliingia kirahisi mno kwenye tope la Richmond lililomuua kabisa katika medani za siasa.

Mwisho, viongozi wa CHADEMA walimtaja kwamba yeye ni FISADI kwenye "List of shame" sijaona akichukua hatua zozote kwa miaka mitatu sasa. Maana yake nini?

Maneno ya Mwalimu Nyerere baada ya kuonana na Nelson Mandela kwenye Ubalozi wa Afrika Kusini mjini Dar es Salaam, "wewe tumekutoa juzi tu toka Umoja wa Vijana. Ghafla una mali kupindukia, umezitoa wapi?

“Wewe ni mchafu, ondoa jina lako kwenye wagombea" ni ya kweli? Je, anaweza kuwaeleza Watanzania mali alizochuma katika kipindi kifupi cha uwaziri mkuu na jinsi alivyozipata?

Jambo moja ni wazi, endapo itatokea kwamba licha ya tahadhari zote nilizozionyesha hapo juu, bado huyu bwana atateuliwa kuwa PM – au wadhifa mwingine – na bado akawapata walamba viatu na wakavunja na kupindisha sheria ya manunuzi serikalini, hakika wote hawa wataishia LUPANGO.

Hii ni kwa kuwa wakati umebadilika. Kama Rais hatachukua hatua, naamini wapo Watanzania watakaokwenda mahakamani.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: