Lowassa, Rostam kumzima Kikwete


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 08 June 2011

Printer-friendly version
Waahidi kumlipua vikaoni
CCM hatihati kuvunjika
Rostam Aziz

HATUA yoyote ya Rais Jakaya Kikwete kutaka kuwafukuza ndani ya Chama Chaa Mapinduzi (CCM) wanaowaita “watuhumiwa wakuu wa ufisadi nchini,” yaweza kumuumiza mwenyewe, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa kutoka ndani ya serikali na chama hicho zinasema watuhumiwa hao ambao Kikwete wiki mbili zilizopita waliitwa mbele ya makamu mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa na kuhojiwa, wamejipanga kuzuia mpango huo na ikibidi watamgeuzia kibao kwa hoja kuwa yeye “ndiye tatizo kuu” katika chama na “chanzo cha serikali kuzorota.”

Wanaotakiwa kuondolewa kwenye uongozi ndani ya chama kwa hoja kwamba “wamechafua sura” ya chama hicho mbele ya wanachama na wananchi, ni Edward Lowassa, Rostam Aziz na Andrew Chenge.

Lowassa anatuhumiwa kufanya upendeleo katika kuipa zabuni ya kuzalisha umeme kampuni ya kitapeli ya Richmond Development Company (LLC), ambayo imethibitika kuwa haikuwa na uwezo, sifa wala fedha za kufanya kazi iliyoomba.

Rostam ametajwa mara kadhaa katika ufanikishaji wa mikataba tata ya kufua umeme ya Richmond/Dowans, pamoja na wizi wa mabilioni ya shilingi uliofanywa na kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd., katika akaunti ya madeni ya nje (EPA) iliyoko Benki Kuu ya Taifa (BoT).

Chenge, aliyelazimika kujiuzulu uwaziri, anatuhumiwa kuingiza nchi katika mikataba mbalimbali ya madini, ununuzi wa ndege ya rais na kujipatia mlungula katika ununuzi wa rada kama ilivyothibitishwa na shirika la uchunguzi wa makosa makubwa la Uingereza (SFO).

Mtoa habari wa gazeti hili ambaye yuko karibu na viongozi hao watatu anasema, “Lowassa, Rostam na Chenge wameapa kutoondoka CCM.” Anasema wameapa kukabiliana na yeyote anayetaka kuwaondoa.

Anasema, “Wewe unajua kwamba Rostam ametoa fedha nyingi sana kwa chama hiki. Sasa anasema wanaotaka aondoke lazima waseme aende wapi. Anasema lolote na liwe, lakini hakuna atakayejiuzulu wala atakayekubali kufukuzwa.”

Mtoa taarifa hizi ni mmoja wa mawaziri katika serikali ya Rais Kikwete.

Kuvuja kwa taarifa kwamba Lowassa, Rostam na Chenge wameapa “kufa na Kikwete” iwapo ataendelea na kinachoitwa msimamo wake wa kutaka kuwaondoa ndani ya uongozi wa juu wa CCM, kumekuja wiki moja baada ya gazeti hili kuripoti kuwa watuhumiwa hao wa ufisadi walikutana kwa faragha na makamu mwenyekiti wa chama hicho, Msekwa na kugoma kujiuzulu.

Katika mkutano huo, Rostam alisisitiza kuwa hawezi kujiuzulu kwa kuwa hana hatia. Hakukuwa na habari yoyote kuhusiana na mazungumzo kati ya Chenge na Msekwa.

Bali Lowassa alihoji sababu ya kutakiwa kujiuzulu na baada ya kuelezwa kuwa ni tuhuma za mkataba tata wa Richmond, haraka alijibu, “Kuhusu Richmond, ukweli unafahamika… Rais anafahamu hilo na kila mmoja anajua hilo.”
Mtoa taarifa anasema Lowassa katika kuhakikisha anabaki ndani ya chama hicho amepanga kueleza mkutano wa NEC, hatua kwa hatua, jinsi kampuni ya Richmond na Dowans zilivyoingia nchini na jinsi zilivyopewa mkataba.

Inadaiwa kuwa hatua hiyo ya Lowassa inatokana na Kikwete kuvunja kinachoitwa “makubaliano ya awali” ya kumsafisha kuhusiana na sakata hilo.

“Unajua Kikwete na Lowassa walikuwa na makubaliano, kwamba yeye ajiuzulu (uwaziri mkuu Februari 2008) ili kulinda serikali na chama. Kisha wakakubaliana kuwa Kikwete atafanya kazi ya kumsafisha kupitia chama na Bunge.

“Lakini Kikwete hakutekeleza makubaliano hayo kwa kisingizio kuwa ni kazi ngumu kumsafisha Lowassa. Sasa yeye ameamua kujisafisha mwenyewe,” taarifa zinaeleza.

Bali si siri kwamba Rais Kikwete, wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu, alifika Monduli, katika jimbo la Lowassa, kumshika mkono, kuuinua na kumtangaza mkutanoni kuwa ni kiongozi shupavu anayestahili kupigiwa kura.

Lowassa anasemekana kutoridhishwa na kauli hiyo katika harakati zake za kurejea ulingo wa juu wa siasa nchini.

Katika mkutano kati ya Lowassa na Msekwa, habari zilinukuu viongozi hao, kila mmoja akishupalia mwenzake.

Wakati imeripotiwa Msekwa akisema, “Lowassa acha mbio za urais,” Lowassa yeye alijibu mapigo kwa kusema, “Lini nimetangaza kugombea urais? Je, (kama nilitangaza) haramu kufanya hivyo, au kuna mliowaandaa?”

Imeelezwa kuwa Msekwa alikana kuwapo mtu aliyeandaliwa, lakini akasema, “ndivyo wanavyosema, kwamba wewe unataka urais,” na kwamba “…haya mambo ya urais yatatuvuruga.”

Wakati Lowassa akipanga kujisafisha kwenye NEC, taarifa zinasema Rais Kikwete amepanga kuitumia Kamati Kuu (CC), “kuwafukuza watuhumiwa” ili kujenga sura ya uwajibikaji.

Ni ndani ya kikao hicho maalum cha CC, ambamo inadaiwa Rais Kikwete amepanga kupeleka hoja ya kuwafukuza watuhumiwa hao, halafu kuijulisha NEC kwa njia ya taarifa.

Inadaiwa mara hoja hiyo itakapoingia NEC, Kikwete atawaeleza wajumbe kuwa CC imetekeleza maagizo ya NEC iliyopita ambayo inadaiwa iliagiza kufukuzwa chama watuhumiwa wote wa ufisadi.

Hata hivyo, kiongozi mmoja wa ngazi ya juu ndani ya CCM amesema, iwapo Kikwete ataamua kutumia njia hiyo, basi ajiandae kukabiliana na upinzani mkali kutoka kwa kundi la Lowassa na wafuasi wake; jambo ambalo linaweza kusababisha kugeuziwa kibao na kuishia kujadiliwa utendaji wake ndani ya chama na serikali.

“Hapo ndipo hata ile hoja ya kutenganisha kofia mbili inaweza kuibuka. Unajua ndani ya CCM kuna viongozi wengi wanaomuona Kikwete ni dhaifu na hivyo wanataka kutenganisha kofia ya mwenyekiti wa chama na rais wa nchi. Sasa akifanya mchezo hapa kunaweza kutokea makubwa,” ameeleza mmoja wa viongozi wa CCM ambaye ni mwanasheria.

Anasema, “Kamati Kuu ya chama haina uwezo wa kuwafukuza wale jamaa. Ni lazima kama wanataka kuwafukuza, hoja iletwe NEC, kwani hiyo ndiyo inayofanya kazi kwa idhini ya mkutano mkuu. Sasa mle NEC, hawa jamaa wako vizuri. Kikwete akileta hoja hiyo, anaweza kujikuta anaingia katika mgogoro na pengine chama kugawanyika.”

Nguvu ya Lowassa inatarajiwa kuegemea viongozi wastaafu, hasa Rais Benjamin Mkapa ambaye wachambuzi wa mambo wanamchukulia kuwa hawezi kukubaliana na mpango wa Rais Kikwete wa kufukuza wenzake katika chama.

Mkapa ambaye amejitosa katika kesi ya aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu, anachukuliwa na wengi kuwa hafurahishwi na hali ya mambo inavyokwenda ndani ya chama na hata serikali chini ya Rais Kikwete.

Kwa mujibu wa watu waliokaribu na viongozi wa juu CCM, hoja ya kumfukuza Lowassa na wenzake tayari imeiva na kwamba azimio la kuwafukuza litafikishwa CC “kwa ajili ya kubarikiwa tu.”

0
Your rating: None Average: 4.5 (22 votes)
Soma zaidi kuhusu: