Lowassa, Rostam, wamvaa Makamba


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 06 October 2009

Printer-friendly version
Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba

HATUA ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Yusuph Makamba kwenda nyumbani kwa Spika wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta, imeudhi baadhi ya vigogo waandamizi wa chama hicho, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa za kuaminika kutoka ndani ya CCM zinataja mbunge wa Igunga, Rostam Aziz na mwenzake wa Monduli, Edward Lowassa kuwa hawakufurahishwa na hatua ya Makamba kwenda jimboni kwa Sitta na kauli alizotoa.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari vya kuaminika, mara baada ya Makamba kurejea Dar es Salaam kutoka Urambo aliitwa na washirika wake hao wawili, Lowassa na Rostam na “kukaripiwa” kwa kauli alizotoa akiwa Urambo.

Wiki mbili zilizopita, Makamba alikwenda jimboni Urambo, mkoani Tabora na kuwaeleza viongozi wa chama hicho mkoani humo kwamba, “Sitta anafanya kazi nzuri ya kujenga CCM.”

Makamba alitoa kauli hiyo wiki mbili baada ya kudhihirisha kuwa alikuwa upande wa waliomsulubu Sitta kwenye vikao vya juu vya CCM mjini Dodoma ambako spika alitishiwa hata kufukuzwa kwenye chama.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, Makamba alirejea tena kauli hiyo mara kadhaa ikiwamo katika mkutano wa hadhara na alipokwenda kumjulia hali mama mzazi wa Sitta.

Inaelezwa kwamba ni “msimamo huo mpya” wa Makamba ulioudhi washirika wake wa kisiasa hadi kufikia hatua ya kumuita nyumbani kwa Lowassa, Dar es Salaam na kumkaripia.

“Ndugu yangu, nakuhakikishia kwamba hatua ile ya Makamba kwenda kwa Sitta, haikuwafurahisha hawa jamaa (Edward Lowassa na Rostam). Ilibidi mzee aitwe na kuonywa,” alisema mtoa taarifa.

Ndani ya kikao kilichochukua zaidi ya saa mbili, taarifa zinasema Lowassa na Rostam walikuwa mbogo wakimuonya Makamba kuwa uamuzi wake utaathiri kambi yao.

“He! Ile safari ya Tabora imemtokea puani. Wale marafiki zake wawili walimjia juu na kumuonya kuwa amefanya jambo baya sana linaloweza kuhatarisha mustakabali wao kisiasa,” alisema mtoa taarifa.

Alisema Lowassa na Rostam walimweleza SG (katibu mkuu) kwamba hatua yake itaufanya umma uamini kuwa Sitta ni “jemedari aliyeshinda vita.”

Rostam na Lowassa wamekuwa katika mvutano mkubwa na Sitta tokea Bunge liunde Kamati Teule kuchunguza mkataba wa kitapeli wa Ricmond uliosababisha Lowassa kujiuzulu nafasi yake ya waziri mkuu.

Kwa muda wa zaidi ya miaka miwili sasa, kumekuwa na minyukano ndani ya Bunge na katika chama huku kambi hizo zikitajwa kuwa ni kama chui na mbwa.

Makamba alipoulizwa juu ya kukaripiwa na Lowassa na Rostam, kwanza alisita, kisha akasema, “Hakuna kitu kama hicho.”

Alisema, “Mimi sikwenda kwa Lowassa. Silijui jambo hilo. Mambo ya Urambo yalishaisha nami nimesharejea Dar es Salaam.”

Akiongea kwa sauti iliyosikika kujaa hasira, Makamba alisema, “Tena nakuagiza usitaje kabisa jina la Lowassa na Rostam katika gazeti lako. Unasikia? Sitaki gazeti lako litaje jina la Lowassa wala Rostam.”

Huku Makamba akiwa tayari amemaliza mahojiano na mwandishi, lakini kabla ya kuzima simu yake ya mkononi, ilisikika sauti ya mtu mwingine ikiuliza, “Lakini wewe si ulikwenda kwa Lowassa?”

Naye Makamba alisikika akijibu, “Ndiyo nilikwenda. Kwani nikienda kuna ubaya gani? Si Lowassa ni ndugu yangu?” Makamba alihoji.

Haikuweza kufahamika mara moja ni nani ambaye Makamba alikuwa akimweleza maneno hayo, lakini sauti hiyo iliyokuwa ikihoji kwa upande wa pili ilikuwa ya mwanamke.

Aidha, taarifa zinasema Makamba alinukuliwa akieleza wenzake hao wawili kuwa hakujua kama safari yake ya Urambo ingeleta utata.

“Mimi sikujua bwana kama nilichokieleza kule Urambo kinaweza kumjenga Sitta. Nimewasikia, nashukuru. Tutakutana baada ya sikukuu (Idd el Fitri),” ameripoti mtoa taarifa akimnukuu Makamba.

Naye Lowassa alipoulizwa na gazeti hili kwamba yeye na Rostam wamekaripia Makamba, haraka alikata simu.

Alipopigiwa tena na kuelezwa kwamba anaongea na mwandishi wa MwanaHALISI, Lowassa alijibu, “Sitaki kuzungumza na waandishi wa habari.”

Alipong’ang’anizwa kwamba gazeti linataka kupata kauli yake juu ya kinachoelezwa kuwamba yeye na Rostam walimkaripia Makamba, Lowassa alisema, “Sizungumzi na waandishi wa habari.” Alikata simu.

Tokea Bunge lipokee ripoti ya mkataba kati ya serikali na kampuni ya Richmond Development Company (LLC) na Lowassa kujiuzulu, kumeibuka kambi mbili miongoni mwa wabunge wa CCM – wanaounga mkono upande wa akina Lowassa na wale wanaopinga.

Minyukano miongoni mwa wabunge imekuwa ikikua na kuchukua sura mpya nje ya bunge ambako pia kambi mbili zimedhihirika.

Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete alinukuliwa hivi karibuni, wakati akijibu maswali ya “papo kwa papo” kwa njia ya televisheni, kuwa uhasana miongoni mwa wabunge umefikia viwango vya kutoaminiana na kuogopa “hata kuachiana glasi.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: