Lowassa, Rostam waumbuana


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 05 May 2009

Printer-friendly version
Edward Lowassa

SIRI imefichuka. Vigogo waliojaribu kuiba ripoti ya Kamati Teule ya Bunge kuhusu kashfa ya Richmond kabla ya kuwasilishwa bungeni, waliiba “kanyaboya,” MwanaHALISI limegundua.

Taarifa mikononi mwa gazeti hili na ambazo zimethibitishwa na gazeti la Rai toleo Na. 814 la Alhamisi iliyopita, zinasema kuna tofauti kubwa kati ya taarifa iliyokwapuliwa mapema na taarifa halisi iliyowasilishwa bungeni.

Gazeti la Rai linalomilikiwa na Rostam Aziz, limeandika kwa mshangao na kulalama, kuwa “…Sehemu ya 7.0 ya taarifa zote mbili inazungumzia ‘HITIMISHO NA MAPENDEKEZO,’ (lakini) taarifa ya kwanza haina mapendekezo yoyote wakati ile ya pili ilikuwa na mapendekezo.”

“Shabaha kuu ya kutaka kuiba taarifa ilikuwa kuona iwapo wanatajwa kwa majina ili waweze kujiandaa kukabiliana na tuhuma. Lakini katika haraka waliiba kanyaboya na kuanza kujigamba kuwa hawahusiki,” ameeleza mtoa habari kwa gazeti hili.

Toleo la Rai lililochapisha habari za kuhitilafiana kwa taarifa, lenye kichwa cha habari “Siri nzito Richmond” na kuuzwa katika baadhi ya mikoa ikiwemo Iringa, Lindi na Ruvuma, limelalama kuwa aliyekuwa waziri mkuu, Edward Lowassa hayumo katika ripoti ya kwanza lakini anatajwa katika ripoti iliyowasilishwa bungeni.

Wachunguzi wanasema kuchapisha taarifa zinazolenga kusafisha Rostam na Lowassa, katika gazeti linalomilikiwa na mmoja wao (Rostam), kunaonyesha kuwatuhumu watu hao kuwa ndio wahusika wakuu katika kupatikana kwa nyaraka ambazo zilikuwa siri hadi zilipowasilishwa bungeni.

Bunge liliteua Kamati maalum kuchunguza mazingira ya rushwa na upendeleo katika mkataba wa kampuni ya kufua umeme ya Richmond Development Company LLC. Kamati ilikabidhi ripoti yake Februari 2008.

Kamati ilitaarifu katika hitimisho kuwa Richmond ilikuwa kampuni feki, isiyo na uwezo kifedha wala kitaaluma na kwamba ilibebwa na ubabe wa Lowassa katika kushinikiza wizara ya nishati na madini.

Habari ya gazeti hilo iliyochukua ukurasa wa mbele na wa pili – ikibeba picha za Lowassa na Harrison Mwakyembe – inatafuta kujenga utetezi kwamba, kwa vile Lowassa na Rostam hawakutajwa katika ripoti iliyoibwa, basi hawakustahili kuwa katika ripoti ya mwisho na sahihi iliyowasilishwa bungeni.

Wakati Lowassa alihusishwa na shinikizo kwa wizara, Rostam alituhumiwa kuwa na uhusiano na Richmond na baadaye kampuni ya Dowans ambayo baadaye ilichukua mkataba wa Richmond.

Zaidi ya mashahidi watano kwenye Kamati teule ya Bunge walitaja Rostam kuwa na uhusiano na Richmond na Dowans kwa vile makampuni hayo yalikuwa yakitumia anwani ya posta na anwani ya barua pepe ya kampuni yake ya Caspian Construction Company Ltd.

Kamati Teule ilipata pia majina ya baadhi ya wafanyakazi wa Caspian ambao pia walikuwa wanaitumikia Dowans Holdings A.A.

Kuna taarifa kuwa nakala ya taarifa kanyaboya iliangukia mikononi mwa Rai katika mbinu na juhudi maalum za kujaribu “kusafisha majina ya Lowassa na Rostam.”

Tayari Rostam ametajwa na Mwenyekiti wa IPP Reginald Mengi na Katibu Mkuu wa Chadema, Willibrod Slaam kuwa mmoja wa watuhumiwa wakuu wa ufisadi nchini.

Ni Rostam ambaye inadaiwa akaunti yake katika benki ya Exim jijini Dar es Salaam ndiyo iliyohamisha fedha kwenda nje kununua mitambo ya kufua umeme ya Richmond na dada yake Dowans.

Aidha, Rostam amekuwa akituhumiwa kuhusika na kampuni tata ya Kagoda Agriculture Limited ambayo ilikwapua zaidi ya Sh. 40 bilioni kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) lakini serikali haijamchukulia hatua.

Chanzo cha habari kinasema wizi wa taarifa isiyokamilika ulifanywa kabla ya mke wa Lowassa, Regina kwenda kwa mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge, Dk. Mwakyembe na kumpigia magoti akimsihi kumuokoa mume wake na zahama ya Richmond. Dk. Mwakyembe ndiye aliwasilisha ripoti bungeni.

Naye Spika Samwel Sitta alipoonyeshwa gazeti lenye madai dhidi ta kamati teule, alisema huku akitabasamu, “Ripoti kamili ni ile iliyowasilishwa bungeni.”

Sitta alisema kuwa alipokea ripoti ya kwanza ya mahali walipofikia na “baadaye wakaniambia hawajamaliza na kuwa wanaomba muda zaidi. Nikawapa muda wakamalizia, na ripoti ya mwisho ndiyo hiyo iliyowasilishwa bungeni. Tatizo liko wapi?”

Taarifa za ndani ya kampuni ya New Habari Corporation inayochapisha gazeti la Rai zinasema toleo lililojaa malalamiko ya Lowassa na Rostam, lilisitishwa kusambazwa baada ya mmiliki (Rostam) kuhofia Mwakyembe kujibu mapigo.

Rostam amenukuliwa akimwambia mmoja wa wahariri wa gazeti lake, “Msisambaze toleo hili. Mwakyembe anajua mambo mengi na bado hajayasema. Mkilisambaza Mwakyembe atalipuka na mtakuwa mmenimaliza,” ameeleza mtoa habari akimnukuu Rostam.

Mwakyembe aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwezi uliopita kuwa “kuna siku nitalipuka na tusiheshimiane kabisa,” akimlenga Rostam ambaye alidai ametumia vyombo vyake vya habari kumchafua.

Woga mwingine wa Rostam unatokana na taarifa ya gazeti kudai kuwa wabunge waliokuwa wajumbe wa Kamati teule hawakuwa waadilifu, jambo ambalo lingeonekana ni kufufua hoja iliyohitimishwa rasmi ambayo ni kinyume cha kanuni; kuvunja heshima ya Bunge na Spika.

Hata hivyo taarifa zinasema amri ya kuzuia gazeti kuuzwa haikufika sehemu zote nchini kiasi kwamba MwanaHALISI liliweza kuagiza nakala za toleo hilo kutoka Iringa.

Badala ya toleo lililozuiliwa na mmiliki, kampuni ilichapisha toleo jingine la tarehe hiyohiyo na namba ileile ya toleo lenye kichwa kisemacho “ Reginald Mengi aivuruga taaluma ya habari nchini.”

Wachunguzi wa mwenendo wa vyombo vya habari wanasema kitendo cha Habari Corporation kutoa matoleo mawili, kwa tarehe moja na namba ileile ya toleo, kingekuwa kimefanywa na MwanaHALISI, basi gazeti lingekuwa linatishiwa kufungiwa na serikali kama ilivyokuwa siku zote.

Hata hivyo, mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Bunge juu ya Richmond aliliambia gazeti hili kuwa katika uchunguzi huwa kuna hatua mbalimbali za kuandika taarifa.

Amesema kinachoonyeshwa kuwa taarifa tofauti ni moja ya hatua hizo ambayo wahusika na walioitoa katika magazeti walikuwa na nia ya kuingilia kazi za kamati au kutafuta kujinasua kabla ya wakati wake.

“Hata sisi tulikuwa tunajua kuwa kazi tunayofanya ni muhimu na inawindwa na wengi na hivyo kulikuwa na suala la ‘kutoweka mayai yote katika kapu moja.’ Ndipo wao wakaambulia kitu tofauti,” alisema.

Kwa takriban mwaka mmoja sasa kumekuwa na juhudi za kutekeleza kile kinachojulikana sasa kuwa ni “kumsafisha Lowassa na washirika wake.”

Kila kunapotokea upenyo, hoja zinajengwa haraka, “Lowassa alisulubiwa bila makosa.” Lakini hakuna mwenye utetezi ambao hadi sasa umeweza kumnasua kutoka kwa kashfa Richmond.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: