Lowassa, unaitwa Kigamboni


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 15 September 2010

Printer-friendly version

EDWARD Lowassa, waziri mkuu aliyejiuzulu, anadaiwa kumwacha “kwenye mataa” Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Shaaban Simba, baada ya kuahidi kuisaidia shule iliyopewa jina lake na kisha asifanye hivyo.

Shule hiyo ya sekondari iliyopewa jina la Edward Lowassa, iko katika eneo la Mwikambe, Kigamboni jijini Dar es Salaam. Ilipangwa kufunguliwa Agosti mwaka huu lakini kutokana na Lowassa kutotimiza ahadi yake, haijafunguliwa hadi leo.

Mufti Simba ndiye mlezi wa shule hiyo inayomilikiwa na taasisi ya Tanzania Sports Catalyst (TSC) na ina lengo la kusomesha watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi.

Baada ya kuitembelea shule hiyo Juni mwaka huu, Lowassa alimuahidi mufti kwamba atahakikisha anaitisha harambee kuchangia kiasi cha Sh. 55 milioni zinazohitajika kwa ajili ya kumalizia ujenzi.

Lowassa, kwa maneno yake mwenyewe, alimuahidi mufti kwamba “…kwa kiasi hicho (milioni 55), atatafuta rafiki zake wachache tu na kitapatikana,” ameeleza mtoa taarifa akinukuu kauli ya Lowassa.

Hata hivyo, miezi mitatu baada ya kutolewa kwa ahadi hiyo, Lowassa hajatimiza ahadi yake hiyo, kitu kilichosababisha shule kutofunguliwa na kuwaacha njiapanda watoto hao waliotarajiwa kuneemeka kwa na shule hiyo.

“Miongoni mwa watoto hawa wako wenye vipaji na uwezo mkubwa katika masuala mbalimbali, hivyo ni lazima tuwathamini na kuwasaidia kwa hali na mali kwa faida ya jamii. Ndiyo maana nimekubali jina langu litumike kwenye sekondari yenu,” ananukuliwa Lowassa akisema.

Alisema, “Nitaitisha harambee hivi karibuni ili tupate fedha za kufanikisha ujenzi wa shule hii ambayo inahitaji zaidi ya Sh. milioni 55 ili watoto wetu waanze kusoma. Nampongeza mufti kwa kuwa mlezi wa shule hii itakayowaendeleza yatima,” alisema Lowassa tarehe 4 Juni mwaka huu shuleni hapo.

Mbali na mufti Simba, mlezi mwingine wa shule hiyo ni aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam (RPC), Alfred Tibaigana.

Fedha ambazo zingetokana na harambee hiyo ya Lowassa zingetumika katika ujenzi wa mabweni ya wanafunzi, vifaa vya maabara na maktaba na ujenzi wa miundombinu ya shule.

Akizungumza na MwanaHALISI juzi Jumatatu, Simba alikiri kwamba shule hiyo haijafunguliwa kama ilivyopangwa kwa vile kuna upungufu wa vifaa muhimu vinavyohitajika kabla masomo kuanza.

“Ni kweli kwamba shule ilipangwa kufunguliwa Agosti mwaka huu lakini kutokana na upungufu wa vifaa, hilo halikuwezekana. Huwezi kufungua shule bila ya mambo muhimu kukamilika,” alisema.

Mufti alisema walikuwa na matumaini makubwa na harambee hiyo ya Lowassa lakini “kwa sababu zilizo nje ya uwezo wao, hilo halikuwezekana.”

“Unajua mwenzetu (Lowassa) ni mwanasiasa na ana mambo mengi. Kwanza alikwenda bungeni na baada ya hapo ndiyo ameingia kwenye harakati za siasa. Nafikiri atakuwa ametingwa na shughuli zake hizo,” alisema mufti.

Wakati Lowassa alipotembelea shule hiyo, mufti alimpongeza kwa “huruma yake kwa Watanzania na watoto wa makundi mbalimbali hasa wanaoishi katika mazingira magumu.”

Taarifa zinasema ni mufti Simba ndiye aliyependekeza kwamba shule hiyo iitwe kwa jina la Lowassa.

Mufti alisema wanasikitika kwamba watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi wanakosa fursa ya kupata elimu lakini wao (shule) hawana la kufanya kwa vile hawana uwezo wa kupata fedha hizo.

Gazeti hili lilifanikiwa pia kuzungumza na mratibu wa ujenzi wa shule hiyo, Suleiman Matthew, ambaye alisema wanachokifanya kwa sasa ni kuvuta subira.

“Ndugu yangu, naomba usituingize kwenye mambo ya siasa. Sisi tunachotaka ni kuwapa hawa watoto fursa ya kujiendeleza kielimu na kukuza vipaji vyao. Lowassa atatusaidia tu.

“Ninachojua ni kwamba kama alituahidi kutusaidia, atatusaidia tu.

Hajatukimbia wala kututelekeza. Naomba mumpe nafasi atusaidie na msimchafue,” alizungumza kwa upole.

Lowassa mwenyewe hakuweza kupatikana kwa simu kueleza kwa nini hajatimiza ahadi yake hadi leo, ilhali akijua watoto hao yatima wanategemea misaada ili waanze masomo.

MwanaHALISI ilifanya ziara shuleni hapo mwishoni mwa wiki iliyopita na kumkuta mtu aliyejitambulisha kuwa mlinzi wa shule ambaye alisema wanafunzi bado hawajaanza masomo.

Mlinzi huyo aliyejulikana kwa jina moja la Mkombozi, alisema kazi yake yeye ni kulinda mali za shule hiyo na hajui mambo ya ndani ya kiutawala na utendaji ya shule hiyo.

“Ndugu yangu, mimi hapa ni mlinzi tu kama unavyoniona. Mambo ya sijui kwa nini shule haijafunguliwa na itafunguliwa lini hayanihusu. Naomba uwatafute wenye shule wakupe majibu,” alisema.

Shule hiyo ya Lowassa itakapokamilika, imepangwa kuwa na watoto zaidi ya 200.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: