Lugha moja, watu tofauti


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 01 September 2010

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

MGOMBEA urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa na mwenzake wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba wanazungumza lugha inayofanana wakati huu wa kampeni.

Profesa Lipumba anasema wengi wa Watanzania hufunga mwaka mzima bila ya kunuia kwa sababu ya hali ngumu ya maisha. Kwa maneno yake, “Watanzania hawana mwezi wa Ramadhani wala Shaabani.” Wao kila siku wamepigika.

Dk. Slaa anasema kuendelea kuwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani ni kuendeleza umasikini na ufisadi kwa wananchi.

Hii ni lugha moja. Wanatoa kilio na kutaka Watanzania waliojiandikisha kupiga kura, wainyime CCM kura ili chama hicho kiondoke madarakani.

Kwa lugha nyingine, unaweza kusema katika hili, CUF na CHADEMA “wameungana.” Na kuna mambo mengi yanayoonyesha vyama hivi viwili vimeungana kuliko yale yanayovitenganisha.

Vyote vinataka kuwepo kwa katiba mpya ya Tanzania. Vyote vinazungumzia hali bora ya maisha kwa Watanzania. Dk. Slaa anapozungumzia usawa na Prof. Lipumba anapozungumzia haki, wote wanazungumzia kitu kimoja. Usawa na haki huenda pamoja.

Swali kubwa ambalo watu wamekuwa wakiniuliza mara kwa mara ni sababu zinazovifanya vyama hivi visiungane. Jibu lake ni rahisi, viongozi wa juu wa vyama hivyo ndio kikwazo.

Nitumie mfano wa Zanzibar ambako baada ya miaka mingi ya uhusiano mbaya kati ya viongozi wa CUF, CCM na wapenzi na wafuasi wao, hali ya mambo sasa inakwenda vizuri.

Waliokutana na kuamua kuhusu amani ya Zanzibar walikuwa watu wasiozidi kumi. Hawa walikutana kwenye msiba wa Mzee Shaaban Khamis Mloo, muasisi wa chama cha CUF. Wakazungumzia nchi yao na wakaamua la kufanya.

Ukizungumzia uhasama wa Seif Shariff Hamad na Amani Abeid Karume, Unguja na Pemba, na CCM na CUF, usingeweza kuwaza kwamba ingetokea siku wakapatanishwa.

Lakini Maalim Seif na rais Karume wamekutana na kumaliza mivutano na siasa chafu. Ukiangalia kwa makini, kazi kubwa zaidi kwenye mapatano hayo ilifanywa na watu hawa wawili, mara nyingine katika mazingira ya usiri.

Walikwenda mbali zaidi ya tofauti za kisiasa za vyama na rafiki zao. Waliamua kuwa viongozi na kufanya kile ambacho viongozi wema wanatarajiwa kufanya; kuongoza njia.

Nakumbuka namna Maalim Seif alivyonusurika kupopolewa mawe mara baada ya kutangaza mwafaka wake na Karume. Wengi wa wanachama na wapenzi wa CUF hawakufurahishwa na mapatano hayo.

Leo hii, wananchi wengi, ndani na nje ya Tanzania, wanawapongeza Maalim Seif na Karume kwa ujasiri na uongozi thabiti waliouonyesha hadi kuifikisha Zanzibar ilipo sasa.

Kama rais Karume na Maalim wamekutana na kumaliza tofauti zao, vipi kuhusu, kwa mfano Freeman Mbowe na Prof. Lipumba? Vipi kuhusu Maalim na Slaa?

Kuna uhasama gani mkubwa baina ya CHADEMA na CUF kuzidi ule wa CCM na CUF Zanzibar? CUF kuna watu waliofunguliwa kesi za uhaini na kufungwa jela na serikali ya CCM lakini leo wamekaa nao chini kuzungumza.

Hata kama CUF na CHADEMA wameshindwa kuelewana katika kusimamisha mgombea mmoja wa urais, wana uadui gani mkubwa wa kushindwa kukaa pamoja na kusema nani atagombea ubunge wapi?

Ninachoona viongozi wa vyama hivi viwili wameshindwa kuonyesha uongozi badala yake wanaendelea kukubali kuendeshwa na wapambe na viongozi wengine.

Kwa namna gani vyama hivi vikubwa vinatakiwa kufanya kazi pamoja ni suala la kuamuliwa na watu wawili au wanne tu miongoni mwa viongozi: Mbowe, Lipumba, Maalim na Slaa.

Lolote litakaloamuliwa na viongozi hawa wanachama watalifuata.

Mimi sioni uwezekano wa Mbowe au Lipumba kutimuliwa uenyekiti wa vyama vyao eti kwa sababu wameungana dhidi ya adui mmoja, (wanaitaja) CCM.

Kuna sababu gani ya Zitto Kabwe kushindana na mgombea wa CUF katika kinyang’anyiro cha ubunge jimbo la Kigoma Kaskazini ilhali ingekuwa rahisi kwake kushindana na mgombea wa CCM?

Kuna sababu gani ya CHADEMA kushindana katika kuwania ubunge katika mikoa ya Kusini mwa Tanzania ambako kwa sasa CUF ina nguvu kuizidi?

Kuna haja gani ya CUF kutumia nguvu nyingi kushindana na CHADEMA katika mikoa ya Kaskazini na Nyanda za Juu Kusini ambako wenzao hao wana nguvu kuwazidi?

Viongozi wa vyama hivi viwili wanakwepa majukumu na kwa kufanya hivyo wanadhoofisha nguvu za upinzani. Hili si suala la kutaka ridhaa ya wanachama wote.

Sote tunajua namna Morgan Tsvangirai na Robert Mugabe walivyokaa na kuzungumza pamoja hata kama walikuwa na tofauti kubwa na uhasama mzito siku zote.

Nelson Mandela alifungwa miaka 27 na utawala wa Makaburu nchini kwake Afrika Kusini. Mandela huyohuyo alikaa mezani na makaburu na kukubaliana mambo ya msingi na leo nchi yao inatawalika vizuri tu.

Suala hapa si kukutana pekee, lakini pia kukubaliana kwa maana ya kufikia maazimio ambayo si lazima kila upande upate kila unachotaka. Msingi muhimu ni “nipe nikupe.”

CHADEMA ni lazima ijue kwamba maafikiano yoyote itakayofikia na CUF yatakuwa na hasara kiasi fulani na faida kwa kiasi hichohicho. Hiyo ndiyo dhana nzima ya mazungumzo yenye nia ya kuleta suluhisho.

Cheo ni dhamana. Uongozi si nafasi ya heshima pekee bali ni nafasi inayotazamwa na watu wengi wakitarajia makubwa kutoka kwayo. Uongozi ni kufanya maamuzi magumu.

Nina masikitiko makubwa kwamba hii ni fursa ambayo viongozi wa vyama hivi vikubwa vya upinzani wameiruhusu iondoke.

Napata shaka iwapo viongozi wetu hawa wataweza kufanya maamuzi magumu wakati watakapokuwa madarakani. Ni hofu inayonipa fadhaa kubwa.

Kinachoniuma ni kwamba wagombea wa vyama hivi viwili - CHADEMA na CUF – wanazungumza lugha moja kwa muda wote huu wa kampeni. Wanachoshindwa ni kuwa kitu kimoja tu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: