Lugola: Sijali nikiondolewa CCM


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 16 May 2012

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii
Kangi Alphaxard  Lugola

HATIMA ya Mbunge wa Jimbo la Mwibara mkoani Mara, Kangi Alphaxard Lugola kuendelea na nafasi hiyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) iko shakani.

Ikiwa atapona kujadiliwa na kutimuliwa kwenye chama chake, basi atakuwa na uwezekano mdogo kupitishwa katika uchaguzi mkuu ujao.

Katibu Mkuu, Wilson Mukama amempasulia wazi kuwa atajadiliwa na chama na huenda wakafikia hatua ya kumtimua kwenye chama, lakini ikishindikana jina lake halitapitishwa tena kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu ujao.

“Wanaonitisha ni viongozi wa CCM. Tena wa makao makuu, lakini mimi sijali na wala siogopi.  Sijali kwa sababu nilifanya kile nilichotumwa nifanye na wananchi wangu; kile cha kutowaangusha, kutowatelekeza na kutowasaliti,” anasema Lugola katika mahojiano na MwanaHALISI.

Hatima ya mbunge huyo iko shakani kutokana na hatua yake ya kusimama kidete, kulaani ufisadi na mafisadi na kuunga mkono hoja ya kupiga kura kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda baada ya kushindwa kushughulikia mawaziri wazembe na wabadhirifu.

Lugola hakuwa mbunge pekee wa CCM aliyeunga hoja hiyo kwa kutia saini, wengine walikuwa Nimrod Mkono (Musoma Vijijini) na Deo Filikunjombe (Ludewa).

Akitoa mchango wake kuhusu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na za Kamati za Kudumu za Bunge za Hesabu za Serikali, Serikali za Mitaa na Mashirika ya umma, Lugola alikuwa mmoja wa wabunge waliowashambulia vikali mawaziri wanane akipendekeza wawajibishwe.

“Kaka wanaonitishia wanasahau kuwa mimi nilikuwa nafanya kazi za ubunge. Na ni kweli niliishauri serikali yangu ya CCM iwawajibishe mawaziri wote walioguswa na ufisadi…na ndivyo ilivyofanyika, lakini haitoshi,” alisema Lugola.

“Waziri mkuu ndiye mkuu wa shughuli za serikali bungeni. Yeye ndiye anayepeleka ripoti kwa Rais Jakaya Kikwete, lakini kama asingemshauri rais kuwawajibisha wale mawaziri, hakika tungemng’oa,” alisisitiza.

Mawaziri walioondolewa kutokana na utendaji kazi wao mbovu ni Mustafa Mkulo (Fedha); Omary Nundu na naibu wake, Dk. Athumani Mfutakamba (Uchukuzi); Dk. Hadji Mponda na naibu wake, Dk Lucy Nkya (Afya na Ustawi wa Jamii); Dk Cyril Chami (Viwanda na Biashara); Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), na William Ngeleja (Nishati na Madini).

Mawaziri walioshutumiwa lakini wakapona kutupwa nje ni George Mkuchika aliyekuwa Ofisi ya Waziri Mkuu, (Tamisemi) na Prof. Jumanne Maghembe aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika. Mkuchika sasa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora) na Prof. Maghembe ni Waziri wa Maji.

Mawaziri wapya waliokabidhiwa ofisi jana ni William Mgimwa (Fedha); Profesa Sospeter Muhongo (Nishati na Madini); Dk Abdallah Kigoda (Viwanda na Biashara); Dk Fenella Mukangara (Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo) na Christopher Chiza (Kilimo, Chakula na Ushirika).

Lugola anasema ripoti hizo ziliibua ufisadi unaozuia utekelezaji wa ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010 na kwamba “ilani ya chama haiwezi kuchezewa ovyo ovyo.”

Katika mahojiano hayo, alisema aliamua kuunga mkono hoja hiyo kwa sababu bunge halina uwezo wala mamlaka kikatiba au kikanuni kuwawajibisha mawaziri. “Njia pekee kwa bunge kufanya ni kumwajibisha waziri mkuu. Ni kupiga kura ya kutokuwa na imani naye.”

Kwa hiyo, anaongeza hata kama bunge lina imani naye ilikuwa muhimu kushinikiza waziri mkuu aamue ama abaki na madaraka yake au amshauri Rais Kikwete kuwawajibisha mawaziri kwani kwa mujibu wa katiba, mawaziri huteuliwa na rais kwa kushauriwa na waziri mkuu.

Alipoulizwa hakuona hatari yoyote dhidi ya serikali yake, Lugola alisema, “…Lakini kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu siyo ya kuiangusha serikali iliyoko madarakani ila ni kumtaka rais avunje na aunde baraza jipya la mawaziri. Watu wasiojua katiba ndio kitendo hiki wanadai ni kuiangusha serikali.”

Anasema kwamba wasiofahamu taratibu ndio huibua maswali kiasi kwamba imefikia hatua ya kutishana kisiasa. “Nilichokifanya nimeongozwa na dhamira safi ya chama changu CCM,” alifafanua.

Je, baada ya hatima yake kuwa shakani atafanya nini, Lugola anasema, “Sitarudi nyuma na naomba siku zote wapiga kura wangu waniunge mkono. Nilikuwa sahihi na ndiyo maana hata rais ameunga mkono.”

“Rais Kikwete alifurahishwa na michango ya wabunge juu ya taarifa za CAG na taarifa za kamati za kudumu za bunge hususani suala la ufisadi, matumizi mabaya ya fedha za umma na matumizi mabaya ya madaraka,” anasema Lugola.

Katika hotuba yake ya maadhimino ya sikukuu ya wafanyakazi, Mei Mosi mwaka huu mjini Tanga, Rais Kikwete aliahidi kuwawajibisha wale wote walioguswa na taarifa za CAG na michango ya wabunge.

Katika hilo Lugola alisema, “Amefanya hivyo ingawa nasema bado. Rais Kikwete asiishie kuwawajibisha tu wahusika lazima wafikishwe mahakamani ikiwa ni pamoja na kufilisiwa mali zao walizopata kwa njia ya kifisadi.”

“Kama Rais Kikwete atasita kufanya hivyo atasababisha idadi ya watu wanaotafsiri kifupi cha CCM kuwa ni Chama Cha Mafisadi izidi kuongezeka siku hadi siku.”

Je, atafanya nini ikiwa Rais Kikwete hataacha sheria ichukue mkondo wake dhidi ya mawaziri na watendaji waliolifikisha taifa hapo, Lugola alijibu haraka, “Mimi ni kada na mbunge wa CCM, sipendi kama chama tuendelee kubezwa. Nina imani na chama changu nina imani na Raia Kikwete ambaye nahisi naye amechoshwa na mafisadi ambao siyo sera ya CCM.”

Upande wa pili wa Lugola ni malalamiko kuhusiana na changamoto katika jimbo lake. Changamoto nyingi ziko katika sekta ya elimu ambako alisema wanafunzi wengi wanasoma wakiwa wamekaa chini, walimu hawatoshi, madarasa hayatoshi, nyumba za walimu hazitoshi na sekondari zote hazina maabara.

“Shule zote za msingi na sekondari zina upungufu mkubwa wa vifaa vya kufundishia, vijiji vingi havina zahanati na pale palipo na zahanati kuna upungufu mkubwa wa dawa, waganga pamoja na wauguzi,” anasema na kuongeza, “Lakini fedha wamechukua mafisadi.”

“Miundombinu ya barabara ni mibovu sana, umaskini kwa ujumla umekithiri, wananchi wamekata tamaa katika kilimo na uvuvi umekufa. Sasa siwezi kukubali kuona fedha za umma zikitafunwa na kikundi cha watu wachache. Nitapambana nao hadi mwisho,” anasema.

Akijibu swali kwa nini wananchi wa Jimbo la Mwibara walimlaki kwa mbwembwe, alisema, “Nimelakiwa kishujaa kwa sababu nao wameibuka mashujaa machoni mwa Watanzania wenzao juu ya vita vya kudumu dhidi ya ufisadi na mafisadi.”

0
No votes yet