'Luku' ya Makamba imedondoka


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 09 December 2009

Printer-friendly version
YUSUF Makamba

YUSUF Makamba, Mtendaji Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), amepoteza "luku." Hajui lini ilidondoka na ilipodondokea. Tunaambiwa anahaha kuitafuta. Potelea mbali!

Sasa kuna wanaosema Yusufu angekuwa na luku yake, ambayo haizibi kauli bali inachuja maudhui kulingana na mtu alipo na wale anaoongea nao, asingesema wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama chake ni “wehu.”

Lakini yamemwagika. Hayazoleki. Ni wale walioongea kwenye Kongamano la Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere ambao Yusufu ameita wehu. Atakayeokota luku ya Yusufu ampelekee haraka.

Kongamano hilo la siku tatu liliandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere inayoongozwa na Mwenyekiti Salim Ahmed Salim na Katibu Mkuu Joseph Butiku katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.

Ni kwenye kongamano hilo, lililohudhuriwa na watu mashuhuri nchini, baadhi yao walibwaga mitima yao hadharani; bila woga wala aibu. Palipohitaji uchambuzi, lawama, shutuma, malalamiko na hata kejeli, paliguswa vilivyo.

Kongamano lilikuwa shamba la fikra huru na lilitoa mwanya kwa maoni na uchambuzi wa mazingira ya sasa kisiasa, kiuchumi na kijamii. Hakuna aliyenyimwa nafasi kwa misingi yoyote ile. Kama kulikuwa na adui wa mtu, basi  alikuwa mmoja: Muda.

Wasomi walichambua. Viongozi wa vyama vya siasa walichangia. Mawaziri walitetea serikali. Wananchi wa kada mbalimbali walisema kilichoko rohoni. Viongozi wa sasa na wa zamani katika CCM na serikali walitoa mawazo na wengine walikandia walichoita “mwenendo” mbaya katika utawala.

Yusufu Makamba hakuwepo. Hakuingia katika darasa la umma. Ameshiba au alikimbia elimu? Ni yeye anayejua sababu iliyomzuia; lakini lazima alikuwa anasikilizia mbali au kupitia vyombo vya habari au “vijana wake” wanusaji.

Ni kutoka huko Yusufu amechomoka na kusema waliomkandia Rais Jakaya Mrisho Kikwete, wakisema hafanyi maamuzi makubwa na kwamba anastahili kuwekwa kando katika uchaguzi ujao, ni wehu.

Kongamano halikuwa la wehu. Halikujadili wehu. Lilisisitiza kuwa taifa linatoswa katika lindi la ufisadi na utovu wa maadili kwa upande wa viongozi. Lilijadili. Lilichambua. Lilikosoa. Lilipendekeza. Lilikanya. Lilijenga muono mpya na mwelekeo. Lilileta mwamko.

Hakukuwa na mwehu aliyealikwa rasmi wala aliyeingia kwa makosa. Kwa Yusufu kuona wehu ndani ya ukumbi wa Karimjee, na waandaaji wasione mwehu na kumsaidia au kumchukulia hatua, bila shaka kunalenga kudhalilisha kazi iliyofanywa.

Wakati wengi wamebaki wakiuliza lini wataitwa tena kwenye mavuno mengine katika shamba la Mwalimu Nyerere Foundation, Yusufu anaona wehu. Anataka kuwaziba midomo. Anataka pia wanaounga mkono yale ambayo walisema, nao waitwe wehu. Wakiogopa kuitwa wehu, basi wanyamaze.

Miongoni mwa wehu au waliokaa na “wehu” katika Karimjee ni Dk. Salim Ahmed Salim, mwana-diplomasia wa kuigwa na Waziri Mkuu wa zamani. Atakayeokota luku ya Yusufu ampelekee haraka.

Wengine ni mawaziri wakuu wa zamani Joseph Warioba na Frederick Sumaye. Tanua orodha. Kulikuwa na Askofu mstaafu Elinezar Sendoro, Profesa Issa Shivji, Profesa Mwesiga Baregu, Balozi Daudi Mwakawago na Askofu Methode Kilaini.

Kulikuwa na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM; wale waajiri wa Yusufu; wale ambao Yusufu ni karani wao: Harisson Mwakyembe, Kate Kamba, Nape Nnauye na wengine.

Ama wote hawa walikuwa wehu au walifurahia wehu wa wehu ukumbini. Kumbuka jina mojamoja la maaskari hawa: Brigedia Mwita, Brigedia Mbena, Hashim Mbita na Meja Jenerali Rashid Makame. Aliyeokota luku ya Yusufu ampelekee haraka.

Kulikuwa na walimu wa vyuo vikuu na wakuu wa asasi mbalimbali za kijamii, ambao kwa siku tatu, walishiriki kugeuza ukumbi kuwa shamba la fikra na uchambuzi maridhawa. Nisisahau Ibrahim Kaduma alyewahi kuwa makamu mkuu wa vyuo vikuu Dar es Salaam na Mzumbe.

Siyo kweli kwamba Yusufu aliona wehu wawili au watatu. Hapana. Alitaka kudhalilisha kazi ya waliohudhuria wakiwa ni pamoja na viongozi wa vyama vya siasa – James Mbatia wa NCCR-Mageuzi, John Cheyo wa UDP, wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kiongozi wa UPDP.

Katika ukumbi kulikuwa na katibu mkuu wa zamani wa CCM, Phillip Mangula, wakili na mbunge Stella Manyanya, wakili mashuhuri Tundu Lissu, mabalozi wa Ujerumani, Burundi na Kenya, waziri Stephen Wassira na waziri Hawa Ghasia. Atakayeokota luku ya Yusufu ampelekee haraka.

Katika ukumbi wa Karimjee kulikuwa na wanawake na wanaume. Achana na viongozi. Watu waliojisikia kwenda pale, kusikiliza kwa makini na hatimaye kuchangia kwenye mijadala. Kulikuwa na waandishi wa habari.

Nilivutiwa sana na kuwepo kwa Gulus Abeid. Huyu aliwahi kuwa mkuu wa wilaya ya Ngorongoro. Alipomaliza kuongea nilisimama, peke yangu kwa heshima yake. Niliona baadhi ya waalikwa wakinishangaa.

Abeid alisema anaifahamu wilaya ya Ngorongoro na vitongoji vyake. Alisema anaifahamu Loliondo, hasa eneo ambako wafugaji walifukuzwa kwa njia ya kuwachomea makazi yao na kuswaga mifugo yao maporini.

Abeid alisema amesikia majina ya vijiji – Arash, Soitsambu, Ororosokwani na vingine vya Loliondo. Akasema vyote ni vya asili. Vimekuwa na wakazi kwa miaka nendarudi. Akahitimisha kwa kusema anashangaa kusikia serikali inadai kuwa watu anaowahahamu kwa miaka mingi ni wahamiaji kutoka Kenya.

Kilichonifurahisha ni kukuta Abeid ni shahidi wangu. Alisema kile nilichoandika nilipokwenda Loliondo na serikali ikakana. Na Abeid siyo mwehu. Atakayeokota luku ya Yusufu ampelekee haraka. 

Kwenye lango la ukumbi kulikuwa na wauza vitabu. Vingi vilikuwa juu ya Nyerere –  hotuba zake na maandishi yake mwenyewe; uchambuzi wa Nyerere mtu na Nyerere kiongozi. Wote hawa walinufaika na shamba la Mwalimu Nyerere Foundation. Hawakuwa wehu.

Tunaleta ushahidi. Soma maazimio ya Kongamano la Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ukurasa 7. Lakini atakayeokota luku ya Yusufu ampelekee mara moja. 

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: