Lusinde ana hoja, Kikwete hana ubavu


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 20 May 2008

Printer-friendly version

KATIKA siku za karibuni, mmoja wa wanasiasa wakongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Job Lusinde, ametoa kauli kwamba watuhumiwa wa ufisadi wenye nyadhifa ndani ya chama hicho wavuliwe uwanachama.

"Ni vema watuhumiwa wafukuzwe uanachama wa CCM ambao utawanyanganya ubunge moja kwa moja," anasema.

Hata hivyo, amesema ingekuwa vema wanachama hao wakajiondoa wenyewe badala ya kusubiri kuwajibishwa na mwenyekiti wao, Rais Jakaya Kikwete.

Miongoni mwa wanachama wanaotajwa katika tuhuma za ufisadi, ni pamoja na Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, Mbunge wa Bukoba Vijijini, Nazir Karamagi na Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge.

Chenge na Rostam, ni wajumbe wa Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, huku Lowassa akibaki na ujumbe wa NEC pekee.

Kauli hii ya kuwataka watuhumiwa wa ufisadi kung'olewa ndani ya chama si ngeni.

Ndani ya vikao vya CC na NEC, vilivyofanyika mkoani Mara, baadhi ya wajumbe, wakiwamo Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa Msuya, na Mwenyekiti wa Mkoa wa Mara, Makongoro Nyerere, walitoa wito huo pia.

Msuya na Makongoro walisimama na kushinikiza chama kiwafukuze uanachama wote wanaotuhumiwa kuhujumu taifa.

Mbele ya mwenyekiti wao, Rais Jakaya Kikwete, walisema ni vema CCM ikajisafisha kwa kuwaondoa katika uongozi watuhumiwa wanaotajwa kuhusika na ufisadi.

Hiyo ilikuwa ni wakati wa kujadili hoja za utafunaji fedha za chama unaodaiwa kufanywa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Abiud Meregesi, na aliyekuwa Katibu wa Mkoa wa Singida, Mujuni Kataraia.

Wakati huo, hoja mbili kuu zilikuwa zimetawala. Ya kwanza ni ile iliyohusu makampuni 22 yaliyoghushi nyaraka na kujichotea Sh. 133 bilioni kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya Benki Kuu ya Tanzania.

Hoja ya pili ilihusu mkataba wa kufua umeme wa dharura kati ya serikali na kampuni ya Richmond Development Commpany (LLC), ambayo imethibitika kuwa lilikuwa kundi la matapeli waliojipanga kutafuna nchi.

Hoja zote zimejikita katika msingi mmoja. Kwamba, kwa vile watuhumiwa wa Richmond wanafahamika; wa EPA wanajulikana, wakwapuaji katika ununuzi wa rada wako wazi, wanunuzi wa mgodi wa Kiwira wanatanua mitaani, kuna haja kwa chama kuanza kuwachukulia hatua wote waliobainika na watakaobainika ili kukisafisha na kujenga msingi wa kumwadabisha kila "atakayechafua chama."

Kwa hiyo, kauli ya Lusinde imemweka kundi moja na kina Msuya na Makongoro.

Je, CCM chini ya Rais Kikwete kinaweza kuchukua hatua hizo? Kama kinaweza kwa nini kimeshindwa kupitisha azimio hilo katika vikao vyake vya Butiama?

Jibu liko wazi. Kwa jinsi CCM kinavyoendesha chaguzi zake na kwa kuzingatia jinsi Rais Kikwete alivyoingia madarakani, haitarajiwi chama hicho kichukue hatua kali dhidi ya mafisadi.

Ni dhahiri kwamba kwa kufanya hivyo, Kikwete atakuwa anakwenda kinyume cha matakwa ya rafiki zake waliomwingiza na kujiingiza katika uongozi kwa lengo la kujitajirisha.

Ndiyo maana wakati Makongoro na Msuya wanasisitiza azima ya chama ya kubaki na watu waadilifu na waaminifu, tena ndani ya vikao halali, Kikwete anaishia kuwakodolea macho.

Kutokana na hali hiyo, iwapo wanachama wa CCM wanataka kusafisha chama chao, lazima wachukue hatua sasa. Wakubali kuachana na utaratibu wa mwenyekiti wa chama kuwa rais, ili Kikwete abaki na serikali, wao wabaki na chama.

Maana dalili zinaonyesha wazi kwamba mizigo hii miwili ya uongozi kwa pamoja imemuelemea rais Kikwete, na ndiyo maana ameshindwa kuthibitisha kauli yake kwamba urais wake "hauna ubia na yeyote."

Ukweli unabaki palepale, kwamba hakuna njia ya mkato kwa CCM kujisafisha. Tayari kimechafuka na kinanuka mbele ya wananchi waliowengi. Njia pekee ya kujisafisha ni kuwatenga watuhumiwa au kuwafukuza katika chama.

Hilo likifanyika, CCM kitakuwa kimezaliwa upya. Si tu kwamba, watakuwa wamekisafisha chama na tuhuma za ufisadi, bali chama hicho kitakuwa kimerudisha imani kwa wananchi.

Kwa mujibu wa katiba ya CCM, mtu pekee anayeweza kufanya maamuzi magumu kama hayo ni mwenyekiti wake wa taifa, Rais Kikwete.

Pamoja na kwamba maamuzi makubwa ya kichama hufanywa na vikao vya juu, ukweli unabaki kuwa kwa utamaduni wa kiutawala ndani ya CCM na serikali, msimamo wa mwenyekiti ndiyo huwa mwelekeo wa vikao hivyo na maamuzi yake.

Hata hivyo, wana CCM wamekuwa wakilalamika kwamba mwenyekiti wao ni mzito wa kufanya maamuzi magumu yanayowagusa rafiki zake walio serikalini, hasa wale waliomfadhili katika kinyang'anyiro cha urais.

Kuna habari kwamba hoja hii ya Lusinde iliwahi kuwa hoja ya kikao cha faragha na dharula cha wastaafu wa serikali na CCM, chini ya Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, siku chache kabla ya vikao vya Butiama.

Mwinyi alitaka wastaafu wenzake wamshinikize mwenyekiti wao ili, pamoja na mambo mengine, awachukulie hatua kali " ikiwamo kuwafukuza uanachama " baadhi ya watuhumiwa wa kashfa ambazo zimekuwa zinaiandama serikali kwa miezi kadhaa sasa.

Hata hivyo, jitihada za wastaafu ziligonga mwamba baada ya Kikwete kukataa mapedekezo yao. Kutokana na hatua hiyo, baadhi yao akiwamo Mwinyi na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, walikacha vikao vya Butiama ili wasihusishwe na maamuzi "mabovu" ya vikao hivyo.

Tayari zipo taarifa kwamba CCM kimegawanyika katika makundi kutokana na "woga" wa rais kuwachukulia hatua mafisadi walio karibu naye, ambao baadhi yao wamo serikalini na wengine wana nyadhifa za juu katika chama.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: