Lusinde ni zao la uoza wa CCM


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 18 April 2012

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

TANGU ulipomalizika uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi ya ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki, makala nyingi zinaandikwa kuhusu matusi aliyoporomosha kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Livingstone Lusinde.

Kada huyo alikuwa akiporomosha matusi hali akijua, makada wengine wa chama hicho walikuwa wakisubiri katika Mahakama Kuu hukumu dhidi ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ya kutumia lugha chafu katika kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2010.

Kuwepo kwa kesi hiyo mahakamani kulipaswa kuwa onyo kwa CCM, lakini wakitumia uzoefu wa kampeni chafu walizoendesha mwaka 2010 bila ya yeyote kati ya viongozi wake kushtakiwa, wakamwacha Lusinde aburudishe umati wa watu kwa matusi.

“…alipokuwa mahabusu alipata bwana na tunajua alichofanywa kule…” “…akitembea ndani ya makombati ni kama amejinyea…” “…washamba na mabwege…hata chupi hawavai…” na “…ana mimba ya CCM….”

Vyombo vingi vya habari vimejiepusha kuandika matusi aliyotoa, na vichache vimedokeza kama hapo juu kwa kuwa ni kweli hayaandikiki.

Kwenye mitandao ya jamii wapo wanaohoji kama kweli huyo ndiye wananchi wa Mtera waliyeona ni bora kuliko Mzee John Samuel Malacela! Mtu anayetaka kujua kama wana-Mtera walipata au walipatikana afuatilie michango ya mbunge huyo bungeni.

Wanaolalamikia matusi ya Lusinde wakati wa kampeni Arumeru Mashariki labda wamesahau CCM ilivyoendesha kampeni za urais mwaka 2010.

Pamoja na kuweka matangazo hadi chooni baada ya maeneo mengi kujaa, bado walitumia makampuni ya simu kukashifu na kumtukana mgombea urais kupitia CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa ambaye alikuwa anamweka Rais Jakaya Kikwete katika nafasi ya kutotetea urais.

MwanaHALISI tukaandika, serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) inajivunia usajili wa simu za mkononi.

Serikali ilikuwa inadai simu za mkononi zinatumiwa kufanya uhalifu. Uhalifu uliotajwa ni pamoja na kutukana, kupanga wizi na, au hujuma; kutoa vitisho kwa watu mbalimbali; kutoa taarifa za upotoshaji na wakati wote huo bila mhusika kufahamika.

Serikali ilidai simu zikisajiliwa, kazi yake ya “ulinzi wa amani” itakuwa imerahisishwa. Simu zilisajiliwa. Wamiliki walisajiliwa. Je,  serikali na TCRA wanaweza kutuambia simu Na. +3588976578 na +3588108226 ni za nchi gani, mtandao gani na mmiliki wake ni nani?

Tuliuliza TCRA waeleze asili ya namba hizo lakini hawakueleza. Tukahoji kampuni ya nje inaweza kutuma ujumbe ukaingia kwenye simu za Watanzania bila kushirikiana na kampuni yoyote nchini petu? Jibu likawa hapana.

Tukaambiwa mchezo huo unachezwa na wataalamu wa kompyuta mahali fulani Dar es Salaam. Tukasema kama ni hivyo, tuwafuate wataalamu wa intelejensia ya kujua al-Shaabab wanavyochukia maandamano ya CHADEMA lakini wakafurahia mikusanyiko ya CCM – Polisi.

Polisi wakasema hawazijui namba. Iwapo polisi na TCRA hawajui na hawataki kudhibiti namba zisizojulikana, ni dhahiri mfumo wa utawala ulishiriki kufanikisha kashfa dhidi ya Dk. Slaa.

Tulipiga hodi kwa Msajili wa Vyama Vya Siasa. Bwana huyu akasema hajaziona namba hizo hivyo hawezi kuzungumzia kitu asichokijua.

Chombo cha mwisho kilikuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Wao wakasema polisi wanaweza kuwa katika nafasi nzuri ya kuzungumzia lakini si wao.

Ujumbe wa kashfa unasambazwa dhidi ya mgombea lakini Polisi, TCRA, NEC na Msajili wakajiweka kando. Hivi ingekuaje kama ujumbe ule wa kashfa ungekuwa dhidi ya mgombea wa CCM?

Kama Arusha makada watatu wa CCM wanasubiri hukumu dhidi ya Lema kuwa alitukana, inawezekanaje makada wa Arumeru Mashariki wasiwe na hofu juu ya athari ya matusi waliyoporomosha?

CCM wanajua TCRA ni yao, polisi ni wao, NEC ni yao, msajili ni wao na mahakama ya kusikiliza kesi kujua hili ni tusi au laa, ni yao.

Mwaka 2010 CCM ndiyo ilikuwa na kauli ya mwisho. Mfano aliyegawa jimbo la Kahama liwepo jimbo jipya la Ushetu ni aliyekuwa Katibu mkuu wa CCM, Yusuf Makamba ila NEC ilidai haina fedha.

Nguvu hizi za CCM hata katika mambo yasiyokihusu ndiyo tunaziona kwa Lusinde: anatukana wapinzani matusi ya nguoni, pembeni akiwepo mlezi wa chama Mkoa wa Arusha, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Siasa na Mahusiano), Steven Wassira (Mbunge wa Bunda), na meneja wa kampeni Arumeru Mashariki, Mwigulu Nchemba (Mbunge wa Iramba Magharibi).

Wakati wa mfumo wa chama kimoja, mgombea urais hakulazimika kujinadi kila kona, watendaji wa mikoani na wilayani walimkampenia. Kampeni hasa za kunadi sera, kujua sifa za mtu, uwezo wake, busara zake na hekima zake zilianza mwaka 1995 uchaguzi wa vyama vingi ulipoanza kufanyika.

Wapinzani walikosoa serikali kwa vielelezo, rushwa na ufujaji wa mali, lakini CCM ikisaidiwa na Mwalimu Julius Nyerere, ilinadi sera hadi Benjamin Mkapa akashinda.

Ingawa CCM ilisaidiwa sana na polisi kwa kupiga, kuwatia ndani na kuvuruga mikutano ya wapinzani, mara zote mbili 1995 na 2000 hakukuwa na kampeni za matusi.

Kampeni chafu ziliasisiwa na makundi ndani ya CCM uchaguzi mkuu wa mwaka 2005. Mtandao ulioasisiwa na wanasiasa wenye fedha na waliojipanga kutwaa kwa nguvu madaraka ya nchi ulipaka matope wagombea wote na mbaya zaidi “ukamvua” uraia Mwanadiplomasia Dk. Salim Ahmed Salim.

Baadhi wakadaiwa wamepoteza uwezo wa kufikiri, wengine wakaambiwa wanasomesha watoto wao kwa fedha za Shirika la Posta na wengine wana ranchi mkoa mzima wa Dodoma. Tuhuma hizo zilifutika baada ya kampeni kumalizika.

Mfumo wa utawala, labda ukiwa umeanza kutengeneza mrithi wa kiti cha enzi haukujitokeza kukemea wala kulaani siasa za majitaka. Kwa kuwa CCM waliheshimu utaratibu wa kumwachia rais kipindi cha pili mwaka 2010 sera ile ya matusi ndiyo ilielekezwa moja kwa moja kwa mgombea mwenye nguvu Dk. Slaa.

Hapa Watanzania wajiulize kama mfumo wa utawala umekuwa kiini cha kuporomoka kwa maadili kitaifa kati ya 2005-2012 ni nani anayejipa mamlaka ya kimaadili kukemea wengine?

Kama yupo anayeona yanayoandikwa magazetini ni chukizo mbele yake, mbele ya Mungu, viongozi, wake kwa waume au wananchi kwa jumla, kwa nini anashindwa kukemea matusi ya nguoni ya Lusinde?

Maana haiwezekani matusi yale yafurahiwe lakini aliyoyatoa Lema ambayo hata mahakama haikuyathibitisha (ikashinikizwa kujitukana) yaonekane laana. Ni rahisi kujumlisha hapa kwamba mfumo wa utawala ndio umemjenga Lusinde awe hivyo.

Picha ya mfumo wa utawala ulioharibiwa anaionyesha Katibu mkuu wa CCM, Wilson Mukama ambaye alipoulizwa kuhusu matusi ya Lusinde, alisema, “alikuwa anajibu mapigo ya wapinzani wao wa kisiasa”. Ni dhahiri basi, Lusinde ni zao la mfumo unaojiangamiza wa CCM na serikali yake.

0789 383 979
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: