Lwakatare atikisa Bukoba


Alfred Lucas's picture

Na Alfred Lucas - Imechapwa 21 April 2009

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala
Umati  uliomlaki Wilfred Muganyizi Lwakatare

“HAIJAPATA kutokea!” Ndivyo wengi wanavyosema mjini Bukoba. Ni baada ya kuona umati uliomlaki Wilfred Muganyizi Lwakatare, akitokea Dar es Salaam kwenye Mkutano Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF).

“Ni shujaa wetu,” waliimba kuanzia uwanja wa ndege wa Bukoba hadi ofisi za CUF na baadaye hadi uwanja wa Uhuru kwenye mkutano wa hadhara walikomsindikiza mbunge wao wa zamani.
 
Ilikuwa 3 Aprili 2009. Itabaki katika historia. Ilikuwa shangwe, nderemo, vifijo na hoihoi. Mzee Yusuf Byeyombo wa mjini Bukoba anasema, umati kama huo haujawahi kuonekana katika miaka ya karibuni.

Taarifa zilikuwa zimeenea kuwa huenda Lwakatare akahama CUF kwenda Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) au kwenda Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kupoteza nafasi yake ya Naibu Katbu Mkuu wa chama chake Bara.

Mwishoni mwa mkutano mkuu mwezi uliopita, Mwenyekiti wa CUF alimteua Lwakatare kuwa mjumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya CUF, jambo ambalo wengi wanadai ilikuwa “kumshusha hadhi.”

Kutokana na uvumi juu ya uwezekano wa kuhama chama chake, Lwakatare hakutarajia kukuta umati mkubwa wa wafuasi wake, wanachama na wapenzi wa CUF na vyama vingine ukimsubiri.

Alipoona umati huo, Lwakatare aliyetua Bukoba saa saba mchana, alidondokwa chozi kutoka jicho la kulia. “Ni kweli,” aliiambia MwanaHALISI, “Nilibubujikwa na machozi ya furaha. Niliemewa ndugu yangu.”

Kwenye mkutano wa hadhara, Lwakatare alitamka mara tatu, “Emali Bantu! “Emali Bantu! “Emali Bantu! Kwa maana ya “Mali ni watu.”

Akijibu waliokuwa wanadai atahamia vyama vingine, Lwakatare alisema, “Tunaangalia penye demokrasi ndani ya vyama. Nina thamani kubwa katika CUF.”

Alielezea thamani hiyo kwamba baada ya kuondolewa kwenye unaibu Katibu Mkuu Bara, amepewa kazi nzito na Profesa Lipumba kuwa Mjumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ikiwa ni uthibitisho tosha wa kukubalika kwake na kuthaminiwa ndani ya CUF.

Lwakatare alirejea kwenye mada kuu ya upinzani dhidi ya CCM. Alisema, “Tuna kazi kubwa kuing’oa CCM; ni kwa sababu iliishakuwa na mizizi mirefu, vinginevyo itaongoza milele.” 

Alifanya uwanja mzima uangue kicheko pale aliposema enzi za Mwalimu Julius Nyerere, “chama kilishika hatamu; lakini sasa kinashika ‘utamu.’” Alisema wakati wa Nyerere CCM ilihubiri ujamaa na kujitegemea lakini sasa inahubiri, inasimamia na kutekeleza “utamaa” na “kujimegea.”

Alifafanua kuwa katika kushika utamu, Manispaa ya Bukoba imeingia katika kashfa ya ufisadi na kusema, “Kwa kuanzia, tunataka maelezo ya matumizi ya Sh. 25 milioni  za mapambano dhidi ya UKIMWI. Zimekwapuliwaje?

“Tunataka Meya aweke wazi mtu aliyempekea shilingi milioni moja katika mazingira ya kutatanisha; vinginevyo majibu ya ufisadi huo wote yatatolewa na Wana-Bukoba katika chaguzi za mtaa mwezi Oktoba mwaka huu na Uchaguzi Mkuu mwaka 2010,” alionya.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: