Maalim Seif alishinda – Zitto


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 11 January 2012

Printer-friendly version

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Zuberi Kabwe amenukuliwa akisema Maalim Seif Shariff Hamad alishinda uchaguzi mkuu wa 2010.

Hii ni mara ya kwanza kwa mtu yeyote ndani ya vyama vya siasa kunukuliwa akijadili suala hili tangu uchaguzi huo ulipokwisha.

Akimwandikia Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Ismail Jussa Ladhu, mbunge huyo alisema hata Jussa anajua kuwa Maalim Seif alishinda uchaguzi.

Zitto anasema Maalim Seif alikubali kutangazwa kuwa ameshindwa na kwamba Jussa anajua kuwa kiongozi wake huyo alishinda urais wa Zanzibar.

Kauli ya Zitto imepatikana kwenye mtandao wa kijamii wa Jamii Forum (JF). Imeelezwa kuwa mawasiliano hayo yalichotwa kutoka mtandao wa Zitto wa Face Book tarehe 5 Januari 2012.

“Ndugu Jussa,” ananukuliwa Zitto akiandika, “kama rafiki yako mkubwa na unajua ninavyomheshimu Maalim Seif kama kiongozi thabiti. Leo nakwambia usilolipenda. Sio sahihi katika demokrasia kama yetu kumfukuza Mbunge Hamad Rashid au hata wanachama wengine wa chama chenu cha CUF.”

Tarehe ya waraka huu inaonyesha ndiyo siku ambayo Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF lilikutana mjini Zanzibar kufukuza baadhi ya viongozi waandamizi wa chama hicho akiwemo mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed.

“Kama Maalim aliweza kumsamehe Salmin, aliweza kumsamehe Karume, aliweza kukubali kutangazwa kushindwa ilhali hata wewe (Jussa) unajua alishinda Urais wa Zanzibar, iweje iwe muhali kumaliza tatizo hili dogo la Hamad Rashid?” anahoji Zitto.

Katika mawasiliano hayo, Zitto anasema, “Hamad ana makosa lukuki. Nimefanya naye kazi bungeni. Hamad pia ana mazuri mengi kafanya. Hamad amejitoa muhanga. Uamuzi wa Baraza Kuu la CUF kumfukuza uanachama ufikiriwe upya.”

Zitto, kwa mujibu wa mawasiliano hayo, alikuwa akijaribu kumsihi Jussa kumshawishi Maalim Seif kuangalia upya uamuzi wa kumfukuza uanachama Hamad Rashid na wenzake waliopo katika mvutano wa uongozi.

Salmin aliyemlenga Zitto anafikiriwa kuwa ni Dk. Salmin Amour Juma (Komandoo) na kwa Karume inasadikika kuwa ni Amani Abeid Karume aliyeongoza kuanzia Novemba 2000 mpaka Oktoba 2010.

Viongozi wote hao, Komandoo na Karume, walitangazwa washindi huku CUF iliyomsimamisha Maalim Seif ikilalamikia matokeo kwa maelezo kwamba Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ilikula njama kuvuruga uchaguzi ili kunufaisha Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Matokeo hayo yalisababisha mgogoro mkubwa wa kisiasa na kujenga uhasama kati ya viongozi hao, Maalim Seif na uongozi wa CUF.

Hata hivyo, wakati Dk. Salmin alikataa kutekeleza muafaka wa 1996 wa CCM na CUF uliofikiwa chini ya usimamizi wa Jumuiya ya Madola, Karume aliingia katika mazungumzo ya siri na Maalim Seif yaliyozaa utawala wa ubia kati ya vyama hivyo viwili.

Kauli ya Zitto kwamba Jussa anajua Maalim Seif alivyokuwa ananyimwa ushindi, inaelekea kuthibitisha kauli za malalamiko ya hivi karibuni ya Hamad Rashid kuwa Jussa “alishindwa” kuwasilisha baadhi ya fomu za matokeo zilizokusanywa vituoni Unguja.

Gazeti hili lilinukuu vyanzo mbalimbali ndani ya CUF vilivyosema kuwa timu ya kampeni iliyoongozwa na Jussa ilizembea kukusanya na kuwasilisha matokeo ya urais katika baadhi ya majimbo Unguja.

Aidha, kuna madai kuwa Jussa alimshinikiza Maalim Seif kukubali matokeo ya kura za urais hata kabla matokeo ya mwisho kupatikana.

Madai hayo yametumiwa na kina Hamad Rashid kulalamika kuwa wanasakamwa isivyo halali wakati kuna viongozi walioumiza chama hicho kutokana na kushindwa kuwajibika wakati wa uchaguzi kiasi cha kumkosesha ushindi mgombea wao.

Zitto ambaye pia ni naibu katibu mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amekuwa rafiki wa karibu wa Jussa, wote wakiwa ni wanasiasa vijana wanaokiri waziwazi kuwa na uhusiano wa karibu na mfanyabiashara Rostam Aziz ambaye pia ni kada mwenye nguvu ndani ya CCM.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: