Maalim Seif amezaliwa upya


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 03 November 2010

Printer-friendly version
Maalim Seif Shariff Hamad

BAADA ya matukio yaliyotokea Zanzibar katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, ni wazi jina la Maalim Seif Shariff Hamad, litabaki katika vitabu vya historia ya visiwa hivyo kwa miaka mingi ijayo.

Seif aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) amefanya mambo mawili makubwa ambayo bila shaka yamevizuia visiwa hivyo kuingia katika mgogoro mkubwa wa kisiasa.

Kwanza ni yeye aliyekubali kukutana na rais aliyemaliza muda wake, Amani Karume, katika Ikulu ya Zanzibar na kupanga kile kinachojulikana leo kama “maridhiano ya Karume na Maalim Seif.”

Ni maridhiano hayo yaliyowafanya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wale wa CUF kukaa meza moja na kuzungumza mambo kama Wazanzibari baada ya miaka zaidi ya 10 ya uhasama.

Baada ya maridhiano yale Maalim Seif alipata shida sana kuwaeleza wanachama wake sababu za kukubali kukutana na kukubaliana mambo na Karume.

Ikumbukwe kwamba miaka tisa iliyopita, wanachama wa CUF waliuawa na wengine kukimbilia ukimbizini, kufuatia matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 uliompa Karume ushindi wakati wafuasi wa CUF waliamini mgombea wao alikuwa ameshinda.

Kwa wale ambao waliishi ukimbizini au kupoteza ndugu, jamaa na marafiki kwa sababu ya ushindi wa Karume, maelewano haya na CCM yalikuwa mwiba uliochoma ndani kabisa ya mioyo ya waathirika.

Ndiyo maana Seif alizomewa na kushutumiwa na baadhi ya wana CUF wakati alipotangaza kuelewana na Karume mbele ya wanachama katika mkutano wa hadhara uliofanyika Unguja, Zanzibar.

Ni maelewano hayo baina ya CCM na CUF ndiyo yaliyofanikisha kura ya maoni kuridhia kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa na hatimaye kufanyia marekebisho katiba kuridhia vyama kugawana madaraka.

Vilevile ni kutokana na maelewano hayo baina ya CCM na CUF ndiyo yalisaidia kufanyika kwa uchaguzi uliomalizika kwa amani Jumapili iliyopita.

Na baada ya matokeo ya uchaguzi huo kutangazwa, Maalim Seif aliyakubali matokeo na kuwa tayari kufanya kazi na mshindi wa uchaguzi huo; mgombea wa CCM, Dk. Ali Mohamed Shein.

Watu wanaopewa tuzo za amani za Nobel zinazoheshimika duniani kote, hufanya aina ya mambo ambayo Maalim ameyafanya kwa Zanzibar.

Nelson Mandela alipewa tuzo ya Nobel kwa pamoja na Frederick de Klerk kwa sababu kama wasingekubaliana na kuelewana, amani isingetamalaki Afrika Kusini.

Saa chache kabla Maalim hajakubaliana na matokeo hayo ya uchaguzi wa urais, tayari joto lilikuwa limepanda katika visiwa hivyo vya marashi ya karafuu.

Kama Maalim Seif angetamka kwamba hakubaliani na matokeo hayo, ni wazi Zanzibar ingeingia katika machafuko. Kuna kila sababu ya kuamini kuwa kama hili lingetokea, hali ingekuwa mbaya kuliko wakati mwingine wowote tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992.

Hata hivyo, Maalim Seif amekubali matokeo hayo. Amekubal matokeo wakati taarifa za awali zilikuwa zikimwonyesha yeye kuwa mshindi dhidi ya Dk. Shein.

Alichofanya Maalim ndicho kinachoitwa uongozi. Kiongozi si mtu anayetakiwa kuendeshwa na hisia za wanachama. Kiongozi anatakiwa kwenda mbali zaidi ya hisia za wanachama.

Maalim angeweza kuamua kukataa matokeo. Bila shaka watu wangepoteza maisha na hali ingeharibika Zanzibar. Wapo wana CUF ambao wangemsifia kwa sababu ya msimamo wake.

Kwa maneno yake mara baada ya kutangazwa kwa matokeo, Maalim Seif alitoa kauli zilizoonyesha ya kuwa anaamini kuna mchezo mchafu ulichezwa dhid yake.

Akaeleza namna vitambulisho vya kupigia kura vilivyokuwa chini ya hifadhi ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) vilivyokuja kuonekana mikononi mwa wasiohusika siku chache kabla ya uchaguzi.

Akaeleza kuhusu unyanyasaji dhidi ya wafuasi na mawakala wa vyama vya upinzani uliokuwa ukifanywa na maofisa wa serikali wakati wa kampeni na siku ya kupiga kura.

Maalim Seif akatoa neno zito kuwa anafahamu ZEC si tume huru ya uchaguzi. Na ujumbe huu akaupeleka kwa Dk. Shein ili aushughulikie atakapoingia madarakani.

Katibu Mkuu huyo wa CUF ni mtu mzima anayeelekea uzeeni. Kama utaangalia vitendo vyake, utaona hafanyi kwa faida ya binafsi.

Ni wazi Maalim Seif ameyafanya aliyoyafanya kwa ajili ya vizazi vijavyo. Na hii ndiyo maana ya uongozi. Waziri Kiongozi huyu wa zamani wa Zanzibar anastahili pongezi kwa aliyoyafanya.

Wazanzibari wanatakiwa kusikiliza na kufuata mawaidha makuu mawili aliyoyatoa Maalim mwishoni mwa hotuba yake. Mosi kwamba hakuna chama au mgombea aliyeshindwa katika uchaguzi huo.

Pili kwamba hakuna sababu ya wapenzi na wafuasi wa vyama hivyo kuanza dhihaka na kebehi kwa sababu ya matokeo hayo.

Wananchi wa Zanzibar wanatakiwa kujiona washindi kwa kile kilichotokea na kitakachotokea mara baada ya serikakal ya umoja wa kitaifa kuanza visiwani humo.

Kitu muhimu kuliko vyote kwa Zanzibar kwa sasa ni raia wa visiwa hivyo kufanya kazi na kurejesha imani baina yao. Huu utakuwa ushindi mkubwa kwa yote.

Hili likifanikiwa, wakati utakuwa mwafaka kwa CCM na CUF kurejea katika ushindani wa kisiasa uliozoeleka katika miaka ya nyuma. Tofauti pekee itakuwa kwamba wakati huo, watu watakuwa wanaaminiana.

Na inawezekana wakati huo Maalim Seif asiwepo kabisa kwenye siasa au duniani. Atakayefaidika na maamuzi haya ya kishujaa ya Maalim wanaweza kuja kuwa watu ambao hawajazaliwa bado kwa sasa.

Watakapokuja kuwa wakubwa, wataelezwa na baba na babu zao kwamba yote hiyo imewezekana kwa sababu Novemba mosi mwaka 2010, Maalim Seif, aliamua kuweka kila kitu pembeni, ukiwamo ushindi wake binafsi na kuwapa ushindi Wazanzibari.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: