Maandamano haya yaungwe mkono


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 11 May 2011

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala
Maandamano ya CHADEMA Mwanza

NIMEFUATILIA kwa muda maandamano yanayofanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) toka mwanzo wake na nimejaribu kutumia muda kuyaelewa. Mwanzoni niliyaona kama maandamano ya watu ambao bado wana machungu ya matokeo ya uchaguzi mkuu wa 30 Oktoba 2010.

Yalionekana kama maandamano ya watu ambao hasira na machungu ya kile walichokiona kuwa ni dhulma ya kuchezewa rafu ya kisiasa katika uchaguzi huo.

Hata hivyo, mara baada ya mandamano ya kushinikiza serikali kutolipa anayejiita mmiliki wa Dowans, ongezeko la bei na tatizo la nishati ya umeme nchini ndivyo wengi walivyoona kuwa kinachopiganiwa na CHADEMA, si matokeo ya uchaguzi, bali uchungu wa rasilimali za taifa na demokrasia.

Hata mauwaji ya wananchi mjini Arusha ni kielelezo cha vita dhidi ya mfumo wa utawala wa kifisadi na mazao yake.

Ni pale tunapoyaangalia maandamano haya kwa mwanga huo ndipo tunaweza kuulewa ujumbe wake vizuri na kuelewa ni kwanini wananchi bila kujali rangi, dini, makabila, au hali zao za maisha wanayaunga mkono.

Ufisadi kama mfumo wa uchumi na utawala unagusa maisha ya kila mmoja. Msingi wa ufisadi ni mambo matatu – utumiaji mbaya wa madaraka, uvunjaji wa sheria bila kujali matokeo yake na kulimbikiza utajiri na njia za kupata utajiri miongoni mwa kikundi cha watu wachache.

Ili ufisadi uimarike na ufanikiwe ni lazima wawepo watu wenye kutumia madaraka vibaya; kikundi cha watu wanaoamini kuwa wanaweza kutumia rasilimali za nchi kwa maslahi yao binafsi.

Ili ufisadi uimarike na ufanikiwe unahitaji watu ambao wako tayari kuvunja sheria bila kuwa na hofu ya kuchukuliwa hatua. Watu wenye mawazo hayo huweza kufanya jambo lolote kwa mtu yeyote, katika hali yeyote na wakati wowote bila hofu wala mashaka ya kuchukuliwa hatua na vyombo vya sheria.

Ndiyo maana ya wizi wa EPA, wizi wa Meremeta, uhalalishaji wa matumizi ya Sh. 5 bilioni zilizotumika kwa ujenzi wa nyumba mbili za serikali, wakati maelfu ya watoto wanasoma katika shule zisizo madarasa wala vyoo!

Ndiyo msingi wa watawala kushindwa kuwajengea wajawazito wodi za kujifungulia na badala yake inawapa maneno matamu, “Mchakato uko mbioni,” huku ukiwa unashindwa kufika.

Ili ufisadi ufanikiwe unahitaji kundi la watu ambao hutengeneza mfumo wa kupata utajiri. Matokeo yake mtu wa kawaida akitaka kufanikiwa kibiashara lazima apitie kwa “magodfather;” akitaka mambo yamnyokee anajikuta anaingia kwenye chama tawala au kuwa karibu na watawala.

Haya mambo matatu ndiyo matokeo ya ufisadi. Kwamba katika nchi kunakuwepo na makundi ya wale walionacho na wasionacho.

Kundi hilo la pili maisha yake yote hutegemea kundi hilo la kwanza. Hivyo, wamachinga na wakulima wanajikuta mara zote wakisubiri wema na neema na fadhili kutoka kwa wale walionacho.

Wale walionacho na ambao katika kuwa nacho wamejiongezea na madaraka ya kuwa nacho huamua mtu aliye chini afanye nini, wapi na kwa nini. Kimsingi ufisadi ni unyonyaji.

Naam! Ufisadi na unyonyaji ni kitu kimoja. Utaona mambo hayo matatu niliyoyataja hapo juu yalikuwa yanajitokeza kabisa katika mfumo wa ukoloni.

Katika ukoloni kikundi cha watu wachache kilijiaminisha kinaweza kuwatawala na kuwaamulia watu wengine maisha yao huku chenyewe kikijineemesha na utajiri wa kundi hilo jingine.

Katika utawala wa kikoloni, watawala wa wakati huo waliamua mafanikio ya watu wengine huku wenyewe wakijiakikishia kuwa ili mtu aweze kufanikiwa ilimpasa kwa namna moja au nyingine kufanya biashara na wakoloni au kuwatumikia.

Sote tunajua jinsi ukoloni ulivyotunyonya. Mfumo wa kikoloni na mafisadi unafanana. Ni mifumo ya utawala ambayo tofauti yake kubwa ni nani anafanya. Ukoloni hufanywa na mgeni anapojilazimisha kutawala watu wengine na ufisadi hufanywa na mwenyeji akijilazimisha kuwatawala wengine.

Matunda ya mifumo yote miwili ni ukandamizaji wa walio wengi ambao huishi kwa kutegemea huruma ya wahusika- wakoloni/mafisadi.

Utawala wa kikoloni uliondolewa kwa kupingwa kwa hoja na kwa makusudi kabisa. Ukoloni kama mfumo dhalimu ulikataliwa kwa sababu kuu kabisa kuwa ni kinyume na utu wa mtu mwingine. Na vivyo hivyo ndivyo ufisadi utakomeshwa. Kwa kuupinga na kuukataa na mawazo yake kuyakataa na pia kukataa matokeo yake.

Ni kwa sababu hiyo basi, maandamano yanayofanywa na CHADEMA yanakumbusha  harakati za kudai uhuru. Mengi yamesemwa na hata kuandikwa na waasisi wa vita vya ukombozi wa uhuru ikiwamo kitabu cha Mohammed Said kinachomzungumzia maisha ya mpigania haki za wanyonge na mmoja wa waasisi wa taifa, Bw. Abdulwahid Sykes.

Ijapokuwa kitabu hicho kinamzungumzia Bw. Sykes, lakini kwa kiasi kikubwa kinagusia harakati za uhuru na jinsi ambavyo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiwa shujaa miongoni mwa mashujaa aliweza kuongoza harakati za kumkataa mkoloni kwa hoja za wazi na kwenda kila kona ya nchi kuwahamasisha wananchi kutambua haki zao na utu wao.

Ni katika kitabu hicho kilichosheni hoja za kudai uhuru, ndimo unaweza kuelewa kwanini tunahitaji uhuru wa pili kutoka katika mfumo wa utawala wa kifisadi ambao tumeacha ujengwe na kutamalaki juu yetu.

Kila mwananchi anayeamini katika utu wa wengine hawezi kupuuza vita hii: Hii ni vita ya wote na hivyo kila raia wa Jamhuri ya Muungano ana haki na wajibu wa kuukataa ufisadi hata kama yeye ni miongoni mwa wanaonufaika na ufisadi.

Jamani wakati wa harakati za wakoloni watu kama Mwalimu Nyerere wangeweza kunufaika na ukoloni kwa kuendelea na ajira zao wakipata mishahara minono na kuwaachia kina Sykes wagombane na wakoloni. Maana wapo wengi tu wakati ule ambao waliona Mwalimu Nyerere na wenzake wanataka kuleta vurugu. Lakini hawakufanya hivyo.

Wapo waliojikomba kwa wakoloni na wakabakia kuwa mamluki. Leo hii wapo kati yetu makuwadi na mamluki wa ufisadi. Wapo ambao wanaona jitihada za kuwaamsha wananchi kudai haki zao na kulilia utajiri wao (sio wa mafisadi) ni kama “kuleta uchochezi na vurugu.” Hawa ni jamaa ya mafisadi na ni wanufaika wa mfumu huu. Wote hawa ni wa kuwakataa.

Swali moja kubwa linabakia ni hili: Je, mwenye dhamira safi juu ya taifa lake anaweza kukaa pembeni na kutounga mkono maandamano haya dhidi ya ufisadi?

Je, Mtanzania ambaye bila kujali dini, kabila, au rangi yake, anaweza kukaa pembeni wakati wenzie wanasimama kuupinga mfumo huu dhalimu uliotupilia mbali utu na hadhi yetu?

Jibu ni moja: Haiwezekani. Ni lazima wote tutoke pamoja kupiga vita mfumo huu. Vingenevyo wapinzani wa vita hii, ni wanufaika wa ufisadi.

mwanakijiji@jamiiforums.com
0
Your rating: None Average: 3.3 (3 votes)
Soma zaidi kuhusu: