Maandamano ni haki ya kila raia


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 09 February 2011

Printer-friendly version
Uchambuzi
Maandamano ya wananchi

DUNIANI kote, dawa ya maandamano ya wananchi – wakulima, wafanyakazi, wanafunzi, asasi za kijamii, wasio na kazi na makundi yoyote yale – haijawahi kuwa mateke, rungu, bunduki, maji ya upupu wala mabomu ya gesi ya kuwasha machoni.

Kwa kuwa hayo hayajawahi kuwa dawa, ndiyo maana watu wanaendelea kufanya maandamano. Pale ambako polisi na jeshi wanatambua haki ya wananchi kujieleza kwa njia hii, wamewaacha waandamane hadi mwisho wa nguvu za misuli yao.

Baada ya wiki ya pili ya maandamano nchini Misri, yakitaka rais akae pembeni baada ya kutawala kwa miaka 30, ndio jeshi limejitokeza na kuwaambia waandamanaji, “Ujumbe wenu umewafikia wahusika; mahitaji yenu yamefahamika. Nyie ndio mnaoweza kurejesha maisha ya kawaida nchini Misri.”

Hiyo ni kauli ya msemaji wa jeshi Ismail Etman kupitia televisheni ya taifa. Aliongeza, “…Majeshi yanawaagiza waandamanaji kurudi majumbani ili kurejesha amani;” lakini bado majeshi yakaendelea kuvumilia waandamanaji.

Tawala za nchi mbalimbali hutofautiana kama zilivyo nchi zenyewe. Bali nchi hizo na wakazi wake huunganishwa na kitu kimoja: Haki. Kila mtu, popote alipo, ana haki ya kuishi. Kuna haki nyingine ambazo zinafanya mataifa yafanane.

Moja ya hizo ni haki ya kuwa na maoni na kuyatoa maoni. Hii ni haki ya kujieleza – kwa kauli ya  mdomo, kuchapisha gazetini, jaridani na kitabuni, kutangaza kwa njia ya mikutano ya hadhara, redio, televisheni, video na sinema na kwa njia ya miguu – maandamano.

Maandamano ni njia ya kujieleza; kuweka wazi maoni ya wahusika. Ni njia ya kupeleka ujumbe kwa jamii; hata mamlaka ya eneo au nchi. Ni njia ya kuwasilisha kilichoko moyoni hasa baada ya njia nyingine kugonga ukuta.

Chukua mfano wa wanafunzi wa chuo kimoja nchini. Wanasema Sh. 5,000 wanazopata kutwa kwa chai ya asubuhi, chakula cha mchana na chakula cha jioni hazitoshi, hata kwa mamalishe. Wanaomba utawala – kwa maana ya serikali kupitia vyombo vyake husika – iongeze kiasi hicho hadi Sh. 10,000.

Wanafunzi wanalilia Sh. 5,000 katikati ya mazingira ya matumizi ya kifisadi ambamo wajanja na wenye madaraka wameingia katika ubia wa kuchota mabilioni ya shilingi ya kodi za wananchi na kuingiza katika matumizi yao binafsi.

Huwa sisahau kuandika juu ya majumba makubwa – mahekalu jijini Dar es Salaam – ambamo utakuta anaishi mume, mke, mtoto mmoja na mbwa mkubwa mweusi. Hawakujenga kwa mahitaji. Ufahari tu.

Kila baada ya miezi miwili au mitatu utasikia waziri mkuu mstaafu Joseph Sinde Warioba akilia kuwa nchi inakwenda pabaya; kwamba pengo kati ya walionacho na wasionacho linaongezeka; kwamba ulimbikizaji wa fedha na mali nyingine, tena za taifa, “utaanganiza amani na utulivu.”

Ni vema bado kuna mtu wa kuonya. Kuna mtu wa kuona tishio la nchi na taifa. Wako akina Warioba wengi. Ni sauti iliayo nyikani. Wanachosema ni kile ambacho wengi wanaona lakini huenda hawana fursa ya kukisema.

Wakati wanafunzi wanaomba kuongezewa Sh. 5,000 kwenye posho ya   mlo – na bila kusikilizwa – wafujaji wanacheua, wanapangusa jasho jembamba la shibe ya kilafi; wanapiga mbinja na kulaani “vitoto vinavyopiga kelele vyuoni na mitaani.” Ulimwengu wa samaki!

Wanafunzi wanaendelea kuomba. Wanasihi. Wanafanya mikutano ya ndani. Wanapeleka ujumbe kwa mkuu wa chuo. Wanaandikia bodi husika. Wanapeleka ujumbe kwa waziri. Wanaandika magazetini na kusihi kupitia vyombo vya habari.

Pamoja na juhudi zote hizo, bodi haiendi kuwasikiliza. Waziri haendi. Rais hasikilizi au hasikii. Wanapaza sauti. Wanasema sasa wanakwenda kumwona rais. Wanaandamana. Hawajatenda kosa lolote. Wanatumia haki yao ya kujieleza kwa njia hiyo ambayo, hata hivyo, wasingeitumia iwapo wangesikilizwa.

Wanafunzi hawa hawana silaha. Hawakwenda kuvamia ghala la silaha ili kuzichukua na kuzifanyia uhalifu. Wanahisi rais wao ama hapati taarifa; au ana kazi nyingi, au amepuuza au haelewi. Wanaamua kwenda kumweleza uso kwa uso, mdomo kwa mdomo.

Njiani wanafunzi wanakumbana na polisi “waliosomea kazi yao.” Wanawazuia kuandamana. Wanawapiga kwa rungu. Wanawamwagia maji ya upupu. Wanawafukuza kama wahalifu. Wanawatawanya. Lindo linaendelea kuona nani atajaribu kutoa pua tena. Usiku unaingia. Polisi wanakwenda kulala au kuacha wachache kuzima wakorofi watakaoibuka usiku.

Siku imepita. Ni kesho ambayo ni leo. Polisi bado wanahesabu silaha zilizotumika kwa watoto wa wakulima na wafanyakazi masikini. Walafi wanaendelea na ulafi wao. Watawala wako usingizini kama siku zote. Rais kayasikia kwa mbali na kama kawaida kaendelea kutabasamu. Wanafunzi wanaendelea na njaa; ile njaa ya kusukumiziwa.

Sababu za kuandamana bado ziko palepale. Ziko vichwani mwa wanafunzi. Tatizo halijaisha. Haliwezi kwisha. Haliwezi kumalizwa na silaha, kebehi wala kejeli. Bado zinahitajika Sh. 5,000; na hiyo ni kwa leo. Baada ya miezi kadhaa, kutegemea nguvu ya soko, watahitaji Sh. 15,000 au zaidi na siyo tena 10,000/=.

Kama silaha zingekuwa zinaondoa sababu za kufanya maandamano, basi Mwanza wasingeandamana tena. Vivyo hivyo Arusha. Kigoma na Shinyanga wangekuwa wametosheka, kwani huko ndiko polisi wametembeza mkong’oto kwa waandamanaji.

Kumbe silaha haziondoi maana, shabaha na umuhimu wa maandamano. Wala haziwezi kuwa mbadala wa kile ambacho wafanyakazi, wanafunzi na makundi mengine yanadai kwa kutumia maandamano.

Kutii ni muhimu katika maisha ya askari na hata raia. Lakini kutii haki ni muhimu zaidi kuliko kutii amri ambazo zinalenga kuneemesha wachache na wasio na uchungu na nchi wala watu wake.

Kutumia silaha na hata vitisho vya kila aina, ili kuziba kauli za wananchi kwa njia ya maandamano, siyo kumaliza matatizo yao wala kuzima nia ya maandamano. Ni kuahirisha hoja yao. Ni kujenga chuki ya muda mrefu. Ni kuasisi hasira fupi mno za wanaodhibitiwa. Ni kutengeneza bomu litakalolipukia walioko madarakani.

Viongozi wa Tanzania hawana budi kujenga tabia ya kukubali maandamano kuwa moja ya njia za watu kujieleza. Wakubali kuyapokea na kupata ujumbe. Kutumia polisi au hata jeshi, kujeruhi na huenda hata kuua ndugu zao eti kwa kuwa wameandamana, ni kujenga uadui wa kudumu kati ya wananchi na watawala.

Huko tuendako, lazima watawala watashindwa, hata kama wana maghala na maghala ya silaha za kila aina; hata za maangamizi.

Acha mwanafunzi, mkulima, mfanyakazi waandamane; hata polisi waliokatwa mishara yao kwa madai kuwa ni michango au askari Magereza wa Mwanza ambao hawajalipwa mishahara ya Desemba na Januari mwaka huu.

Yeyote anayeandamana anatumia haki yake ya kujieleza; mara hii anatumia miguu kufikisha ujumbe uliokataliwa kwa njia nyingine. Acha wanafunzi wafikishe ujumbe kuwa fedha wanazopata hazitoshi kwa mlo wa siku. Fedha hawawapi, hata kuwasikiliza hawataki? Huu ni ukatili usiosameheka.

0
Your rating: None Average: 5 (3 votes)