Mabadiliko yako katika kura yako


editor's picture

Na editor - Imechapwa 27 October 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

WATANZANIA wenye sifa ya kupiga kura na ambao walijiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura watatumia haki yao kidemokrasia kuchagua viongozi wanaowataka Jumapili ijayo.

Kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Watanzania wapatao 19.6 milioni wenye umri wa miaka 18 na zaidi watashiriki katika upigaji kura.

Katika kipindi chote, tangu kampeni zilipoanza Agosti 21, mwaka huu, wananchi walipata fursa ya kusikiliza wagombea wote kuanzia wa urais, ubunge hadi udiwani.

Wagombea hao, hasa wa urais na ubunge walipita kila kona kunadi sera zao kwa wanachama na wananchi kwa ujumla kushawishi kwa nini wachaguliwe wao na si wengine.

Walipata fursa ya kutoa ufafanuzi wa masuala ya kisera na walipata fursa ya kutoa ahadi kwa wananchi kwamba watawafanyia nini wakiingia madarakani.

Wapo wagombea urais waliotoa ahadi za kununua meli, kujenga viwanja vya ndege, kujenga mabwawa ya maji, kupeleka maji na umeme vijijini, kujenga madaraja na kununua vivuko.

Wagombea wengine waliahidi wakichaguliwa serikali zao zitatoa elimu bure pamoja na huduma ya afya bure. Pia waliahidi kupambana na mafisadi, kushusha bei ya bati na sementi ili kila mwananchi aweze kujenga nyumba bora kwa gharama nafuu.

Ni kutokana na mvuto wa sera za kila chama wananchi, mamia kwa maelfu, wamekuwa wakifurika kusikiliza ili waamue. Baadhi walifanikiwa kuvuta hata wapinzani na wengine waliweza kupata wanachama wapya kutoka makundi ya watu ambao hawakuwa na vyama.

Kwa hiyo, japokuwa siku zimebaki nne, hadi kufika siku ya uchaguzi, wapigakura hao wameshaamua nani wa kuchagua baada ya kusikiliza hotuba na sera kwa amani na utulivu.

Kwa hiyo Jumapili Watanzania wataamua hatima ya nchi yao kwamba iendelee kuongozwa na chama tawala — Chama Cha Mapinduzi (CCM) au cha upinzani kama vile Chama cha Wananchi (CUF) au Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Ikiwa wananchi wataamua kuirejesha CCM ina maana kuwa hawataki yawepo mabadiliko na ikiwa wataamua kuingiza madarakani chama kipya watakuwa wanahitaji mabadiliko.

Tunawahimiza Watanzania wote, kutumia nafasi hiyo muhimu na tunawatakia kila la heri kwani kura yao ndiyo elimu yao, barabara zao, mabwawa yao, au kwa kifupi maisha bora.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: