Mabilioni yakusanywa kumwangusha Kikwete


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 14 April 2009

Printer-friendly version
RAIS Jakaya  Kikwete

RAIS Jakaya Kikwete atahitaji kutumia nguvu mara tatu kukabiliana na “genge” linalotaka kumzuia kugombea urais kwa kipindi cha pili, MwanaHALISI limeelezwa. Taarifa zilizopatika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki zilisema, wanaotaka kumzuia Kikwete kugombea urais kwa kipindi cha pili, wamepanga kutumia, na tayari wamekusanya Sh. 2.5 bilioni kwa shughuli hiyo.

“Hizi si fedha kidogo. Lazima CCM ijipange kutumia mara tatu zaidi (Sh. 7.5 bilioni) kama inataka Kikwete apite,” ameeleza mpasha habari.

Fedha za wanaompinga Kikwete zinalenga kununulia magari, pikipiki, baisikeli, sare – suruali, fulana, khanga na kapelo; mabango na vipeperushi.

Nyingine zimepangwa kutumika katika ununuzi wa mafuta kwa ajili ya magari, posho za wapigadebe na “takrima” kwa wabunge ambao wataamua kuwaunga mkono kwa kuchomoka kwenye mkondo mkuu wa CCM.

Wiki iliyopita, aliyekuwa mwenyekiti wa mkoa wa Dar es Salaam, Hemed Mkali, aliliambia gazeti la NIPASHE kuwa lazima kila juhudi ifanywe “kuzima mahangaiko ya wanaotaka kugombea urais” mwaka 2010 vinginevyo CCM itaangamia.

Mkali alikuwa akisisitiza hoja ya wastaafu wa CCM ambao siku moja kabla ya kauli yake walitahadharisha mgawanyiko ndani ya chama chao, wakisema utatokana na kugombea urais mwaka kesho.

Viongozi wengine waliotoa rai ya kuvunja “mahangaiko ya kugombea urais” ni aliyekuwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dodoma, Pancreas Ndejembi, aliyekuwa mwenyekiti wa mkoa wa Iringa, Tasil Mgoda na aliyekuwa mwenyekiti wa mkoa wa Pwani, Jumanne Mangala.

Akizungumza na MwanaHALISI kwa njia ya simu juzi Jumatatu, Mkali alisema yeye na wenzake wanajua wanachosema na kwamba hawakukurupuka.

Alipotakiwa kueleza kwa undani msingi wa madai yao kuhusu waliomo kwenye mhangaiko wa urais, kwanza Mkali alisita na baadaye alieleza:

“Tunawafahamu. Wapo watu wengi. Wengine ni viongozi wa juu serikalini na ndani ya chama. Wengine ni ‘marafiki zake’ wa karibu,” alieleza Mkali.

Alipobanwa kueleza maana ya “rafiki zake,” na huyo hasa ni nani, Mkali alisema kwa sauti ya kubembeleza, “Ndugu yangu, sasa hivi niko Rufiji; si usubiri nirudi Dar es Salaam ili tuongee?”

Taarifa zaidi zinasema Mkali na wenzake, baada ya kuongea na waandishi wa habari juu ya dukuduku lao, walikwenda nyumbani kwa kiongozi mmoja mstaafu na kumweleza kuwa walikuwa na ushahidi tosha juu ya kile walichokuwa wakisema.

Haijafahamika iwapo wastaafu waliagizwa na baadhi ya viongozi wa CCM au serikali ili kuvunja ukimya juu ya kinachoendelea; lakini kwa nafasi yao ya sasa hawakutegemewa kuwa na maslahi ya kuwafanya kuwa mstari wa mbele.

Wiki moja kabla ya wastaafu kuvunja kimya, makamu mwenyekiti mstaafu na mjumbe wa kudumu wa Kamati Kuu ya CCM, John Samwel Malecela alisema wanaotaka kuchuana na Kikwete kutoka ndani ya chama hicho wanajisumbua.

Aliwaambia waandishi wa habari, nyumbani kwake Sea View, Dar es Salaam kuwa mgombea wa CCM mwaka 2010 ni Jakaya Mrisho Kikwete.

Kauli ya Malecela na zile za wenyeviti wa mikoa wastaafu, haziwezi kuwa mlolongo wa porojo mitaani bali majibu kwa kile ambacho kinachemka ndani ya nyoyo na vikao vya siri vya wanachama na viongozi.

Gazeti hili liliandika Oktoba mwaka jana kuwa kulikuwa na njama za kumg’oa Kikwete. Lilifungiwa kwa siku 90 kwa madai ya wizara ya habari kwa akile kilichoitwa kufanya “uchochezi.”

Toleo Na. 118 la MwanaHALISI liliandika kuwa watuhumiwa wa ufisadi nchini walikuwa wamejipanga kumg’;oa Rais Kukwete ili asigombee urais mwaka 2010.

Gazeti lilinukuu taarifa zilizosema wapinzani wa Kikwete walikuwa wanataka kumfanya awe “One-Term President” – rais wa kipindi kimoja, lengo likiwa kumwadhibu kwa kile kilichoitwa kuwasahau wenzake na kutowatetea walipoingia katika matatizo.

Tangu hapo, vyombo vya habari mbalimbali, yakiwemo magazeti ya serikali na CCM, vimeandika juu ya njama za “kumzuia Kikwete kugombea urais” Oktoba mwaka kesho.

Mbunge wa Maswa ambaye alijitosa katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2005 na kushindwa katika hatua za awali, John Shibuda tayari ametangaza kumpinga Kikwete katika uchaguzi mwakani.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: