Mabomu Gongolamboto: ‘Tuliponea chupuchupu’


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 02 March 2011

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki

SAIDA binti Rajab amepigwa na kitu chenye ncha kali. Kimekata mkono wake wa kushoto. Akauona: Ule pale! Akashindwa kuuokota. Akauacha Ukonga mbele ya msikiti.

Ni wiki mbili kamili sasa tangu hayo yatokee. Saida anasema alikatwa na kigae cha moja ya mabomu/makombora yaliyolipuka katika kambi ya Jeshi la Wananchi (JW) kikosi Na. 511, Gongolamboto jijini Dar es Salaam.

Nilishindwa kumuuliza Saida ulipo mkono wake uliokatika. Nilimuuliza mume wake, Salum Mbaruk, kwa njia ya simu.

Mwandishi: Salum, naja kwako kwa mara nyingine. Naona nikuombe radhi mapema. Swali langu linaweza kukuudhi bali naomba univumilie.

Salum: Uliza tu ndugu yangu.

Mwandishi: Unajua lolote juu ya mkono wa mkeo uliokatika?

Salum: Kwanza ni kweli ulikatika. Nilikuwepo. Niliuona. Sikuweza kuuchukua. Katika mazingira yale, nilishindwa kuubeba. Niliuacha tu. Nikiwa majeruhi, natokwa damu uso mzima, nilishindwa…Nilichoweza kufanya ni kumburuta mke wangu na dada yangu, Mwahija Mbaruk hadi lango la Magereza Ukonga, kuomba msaada wa usafiri kwenda hospitali.

Mwandishi: Unajua uliko sasa?

Salum: Ninajua. Ndugu zangu walipata taarifa. Wakaenda eneo la tukio. Wakachukua mkono na kuupeleka kituo cha polisi cha Sitakishari; wakatao taarifa na baadaye kwenda kuuzika. Tangu hapo sijaulizia…

Mwandishi: Hapa pia naomba radhi mapema. Ni mkono huo uliokuwa na pete?

Salum: Sijui. Siwezi kuwa na uhakika. Sijamuuliza. Hatujapata muda wa kukaa pamoja kwa utulivu. Unafahamu “kwetu” pete zinavaliwa lakini hazina kanuni ya mikono na vidole…

Saida ameruhusiwa kutoka hospitali kuu ya Muhimbili. Anasafisha na kufunga vidonda katika hospitali ya TMJ Mikocheni, jijini Dar es Salaam ambako pia anapewa dawa.

Ananiambia, “Nafuu ipo. Bado kuna maumivu kwenye mkono ingawa pia nina maumivu makali mgongoni ambako nilichomwa na chuma. Lakini kwa jumla, kila siku inayokuja inaleta matumaini.”

Jumatano, tarehe 16 mwezi huu, mabomu yalilipuka katika kambi ya Jeshi la Wananchi (JW)  Gongolamboto. Saida anakumbuka kuwa siku hiyo, yapata saa 12 jioni, walisikia “mpasuko mdogo – pwa!” nje ya nyumba yao.

Walipokwenda kuangalia wakakuta ni ajali ya gari na baisikeli. Lakini kwenye saa mbili kasoro robo hivi, mtoto aliingia ndani na kuwambia Saida na mumewe, Salum aliyekuwa ametoka msikitini, kuwa nje kuna milipuko mikubwa.

Wakati huo, tayari moto ulikuwa umeanza kutengeneza wingu jekundu angani na milipuko ilikuwa ikiendelea moja baada ya mwingine. Walipata ushauri kutoka kwa majirani kuwa watoke nje ya nyumba. Walifanya hivyo.

Hapo safari ya kujiokoa na kuwa karibu na wengine ilikuwa imeanza. Ni watu 10: Salum na mkewe Saida; watoto wao Fatma, Warda na mwingine; dada yake Salum na watoto wake watatu; mama mdogo wa Salum na shemeji yake.

Hawa ni wakazi wa Ukonga, Mombasa; wameangaliana na kambi ya jeshi kitengo cha polisi cha – FFU. Waliongozana hadi Magereza na kupita kidogo hadi msikiti ulio karibu mita 50 kutoka magereza.

Ni hapa ambapo Saida alipotezea mkono. “Hatukuwa peke yetu. Kulikuwa na kusanyiko kubwa la wananchi,” anasimulia Salum.

Anasema, kwanza walijishauri iwapo waingie msikitini au wabaki nje. Waliamua kubaki nje. Kabla hawajakaa chini ndipo walisikia mlipuko mkubwa uliofuatwa na mingine na katika mstuko huo, Saida alistukia “kitu chenye ncha kali” kikikata mkono wake wa kushoto na kuuona ukijiviringisha mbele yake.

Saida alikatwa pia kwenye kiwiko cha mkono wa kulia; alichomwa na “kitu kizito” mgongoni na kuchomwa  miguuni na kile alichoita “labda vipande vya mabomu” pembeni mwa ugoko ambako vimeacha majeraha.

Kigae kilichokata mkono wa Saida kiling’ang’ania hapohapo kwenye sehemu ndogo ya mkono wa kushoto iliyobaki karibu na bega.

Salum alipigwa na “vipande kama vya chuma” juu ya nyusi za jicho la kushoto na chini ya jicho hilo. Mtoto wao Fatma, mwenye umri wa miaka saba, alipigwa kwenye kiwiko cha mkono wa kulia, wakati dada yake alipigwa usoni na kwenye bega la kushoto.

Saida amepoteza mkono. Anachuruzika damu. Anaishiwa nguvu. Hawezi kutembea. Salum anatokwa damu usoni ambayo inachuruzikia machoni na Dada yake, Mwahija Mbaruk anavuja uso mzima na hana nguvu tena za kutembea.

Wengine wote wametawanyika pamoja na umati uliokuwa karibu na msikiti. Hapa ndipo Salum alifanya kazi ya “fatiki.”

“Huku nikitokwa damu usoni, niliweza kuwaburuta – mke wangu na dada yangu – kumbuka wote ni wazito, hadi kwenye lango la Magereza kuomba msaada wa gari. Hapa nikaambiwa hawakuwa na gari,” anasimulia Salum.

“Niliwalaza hapo mchangani. Muda mfupi baadaye yalikuja magari mawili kutoka kambi ya Magereza lakini katika yote hayo kulikuwa na nafasi ya mtu mmoja. Hapa nilishindwa nimweke nani – mke wangu au dada,” Salum anasimulia kwa sauti ya uchungu.

Ama kweli lilikuwa fumbo la “Nimwokoe nani?” wakati Salum alitaka kuwafikisha wote hospitalini kwani kila mmoja alikuwa katika hali mbaya. Aliendelea kuvuta subira.

Hata kabla ya bomu kupora mkono wa Saida, hakukuwa na mabasi. Hakukuwa na taksi, malori, magari ya jeshi wala ya serikali. Barabara zilifurika wananchi wanaokimbia mabomu na gari mojamoja la familia inayokimbia milipuko.

Mwandishi: Kuna wakati vyombo vya usalama hufanya mazoezi ya kukabiliana na maafa, ambamo polisi, jeshi, zimamoto, msalaba mwekundu, maskauti, makampuni ya ulinzi hujitokeza kwa ukakamavu. Je, hali hii uliiona wakati wa milipuko ya Gongolamboto?

Salum: Sikuona chochote cha aina hiyo. Nadhani mpaka sasa nimekueleza niliyoyaona na nilivyohangaika kupata msaada wa usafiri.

Lakini hata kama vyombo vya usafiri vya kulipia vingekuwepo, vingegharimu kiasi kikubwa, wakati Salum alitoka nyumbani kwake akiwa na Sh. 2,000 tu. “Hizi zingetumiwa na nani?” anauliza katikati ya kicheko chenye chembechembe za kujuta na kujihurumia.

Akiwa katika msongo wa mawazo, Salum aliweza kuona gari – pick-up – linaegeshwa nje ya Magereza. Alilikimbilia. Aliomba msaada wa kubeba majeruhi wake.

“Aliyekuwa akiendesha gari hilo – mwanaume – alikubali, bali aliniambia nisubiri hadi familia yake ifike ili tuondoke pamoja. Walikuja. Tuliingia na kuondoka,” Salim anasimulia.

Haikuwezekana kwenda hospitali ya Amana iliyoko Ilala. Barabara iendayo huko, kutokea njiapanda ya Barabara ya Nyerere na Mandela ilikuwa imeziba kwa wingi wa magari yaliyozuiwa kwenda Ukonga na maeneo mengine. Magari yalikuwa hayaendi. Ndipo mwenye gari aliamua kuwapeleka hospitali ya Temeke.

Familia ya Salum ndiyo ilikuwa ya kwanza, miongoni mwa majeruhi kutoka Gongolamboto kuhudumiwa na hospitali ya Temeke.

Huku kigae kilichokata mkono wa Saida kikiwa bado kinaning’inia kwenye mkono wake, daktari wa Temeke alinukuliwa akimwambia  “…wewe unastahili kupelekwa hospitali kuu ya Muhimbili.” Ndivyo ilivyokuwa pia kwa dada yake Salum. Walihamishiwa huko.

“Mimi nilibaki Temeke,” Salum anasimulia. “Madaktari walianza kunishughulikia. Tangu hapo sikujitambua hadi saa nane usiku nilipotoka usingizini na kukuta nimewekewa dripu. Nilipojipapaswa nikakuta bado nina simu. Nikaanza kufanya mawasiliano.”

Mwandishi: Unafikiri au uliambiwa kuwa ulipoteza fahamu au walikupa dawa za kupunguza maumivu na kuleta usingizi?

Salum: Naona walinipa dawa; hasa sindano kwa njia ya dripu, kwani muda wote huo wa mahangaiko sikuwa nimepoteza fahamu hata kidogo.

Asubuhi yake, Alhamisi, Salum alianza mawasiliano mapana kujua waliko wale wote aliotokanao nyumbani kwenda kujiukinga mabomu.

“Niliongea na dada yangu mkubwa, Ziledi Mbaruk anayeishi Mbagala, naye akanithibitishia kuwa watoto wote wako salama. Alisema mtoto wangu Fatma na mwingine Aisha Jamal wa dada yangu, waliumia lakini walikuwa wakipata matibabu katika hospitali ya Amana,” anakumbuka Salum.

Aisha aliumuia kwenye paji la uso, kisogoni na kwenye paja. Wakati wa operesheni, madaktari walitoa kipande cha chuma kisogoni mwake.

Saida anasema muda mfupi baada ya kufikishwa hospitali ya Muhimbili, hakuweza kukumbuka chochote. Anasimuliwa tu jinsi alivyokuwa chumba cha upasuaji hadi saa sita usiku wa manane na jinsi madaktari walivyoondoa “kigae cha bomu/kombora” kilichokuwa kumeng’ang’ania kwenye mkono wake.

Saida, mwenye umri wa miaka 36 ni sekretari katika kampuni ya uwakili ya East Africa Law Chambers ya jijini Dar es Salaam.

Akijigeuza huku na kule kwa shida, kitandani kwake, nyumbani kwa mama yake, Sania Yusuph, Mikocheni jijini Dar es Salaam anapougulia, Saida anasema wakati kidonda kinaendelea kukauka, bado anasikia maumivu makali mgongoni.

Kuhusu janga hili, Sania Yusuph ambaye ni mwalimu Shule ya Msingi Tumaini, Kawe, Dar es Salaam anasema “…yote nampa Mungu. Nawashukuru wote ambao waliwapa msaada na Mwenyezi Mungu awazidishie.”

Kuhusu mwenye gari aina ya pick-up aliyewabeba hadi hospitalini Temeke, Salum anasema anamfahamu na kwamba huwa wanaswali pamoja msikitini.

“Nikirudi Ukonga, nitamtafuta na kujitambulisha kwake. Nadhani na yeye atanikumbuka,” anasema Salum na kuongeza kuwa anawashukuru wote  waliowasaidia na kwamba anamwomba Mungu awazidishie moyo wa huruma.

Hivi sasa Salum (45) anaishi Mbagala kwa dada yake. Kutoka huko anakwenda kumjulia hali mkewe Saida ambaye anaugulia kwa mama yake, Mikocheni.

Kwa upande wake, Saida anasema anashukuru wote waliowasaidia tangu alipoumia hadi sasa. Pamoja na wengine, anamtaja Bw. Juvenalis Ngowi ambaye ni bosi wa kampuni anayofanyia kazi, kwa alichoita “msaada mkubwa” ambao kampuni yake imetoa.

Anamtaja pia Stella Ndikini, mwanasheria wa kampuni hiyohiyo kwa moyo wa kusaidia.

Familia ya Salum na Saida ni moja ya familia nyingi na watu mmojammoja ambao wamekumbwa na janga la mlipuko wa mabomu/makombora ya Gongolamboto.

Familia hii sasa, na nyingine zinafanya kazi moja: Kujiuguza, tena kwa gharama kubwa. Salum anafanya kazi gani?

Serikali imetangaza kuwa mpaka sasa watu waliofahamika kuwa wamekufa kutokana na milipuko wanafikia 25. Kuna wengi walioumia kwa viwango tofauti ikiwa ni pamoja na waliopatwa na mstuko.

Hii ni mara ya tatu mabomu kulipuka ndani ya kambi za JW. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1995 huko Gongolamboto. Mara ya pili ilikuwa Mbagala, miaka miwili iliyopita; na mara ya tatu imekuwa palepale Gongolamboto.

Mara zote serikali imesema tukio hilo “halitajirudia.” Inawezekana kabisa kuwa halijirudii, bali linarudiwa. Sasa imeahidi kuwa makini. Tuone hivyo.

Vilevile tuone serikali ikiwawajibika katika kusema ukweli juu ya tukio na kutoa pozo stahiki kwa kila mmoja.

0713 614872 ndimara@yahoo.com www.ndimara.blogspot.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: