Mabomu katika siasa ni kashfa


editor's picture

Na editor - Imechapwa 11 August 2009

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

WIKI iliyopita polisi walitangaza kutokea kwa milipuko miwili ya mabomu ya baruti (TNT) kisiwani Pemba.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Yahya Bugi, amesema milipuko hiyo ililenga kushambulia familia za masheha wa Muhogoni, Salim Said Salim na Amina Khatib wa Msuka.

Milipuko yote imeelezwa kuwa ilitokea baada ya kusikika vishindo nje na masheha hao kutoka kuangalia kunani. Tunaambiwa walikuta "vijana wakikimbilia vichakani ndipo ilisikika milipuko." Maelezo haya yana matundu; hayakidhi haja ya kujua kilichotokea.

Tunapoangalia yanayotokea Pemba, tunajenga mashaka kuhusu taarifa hizi. Uzoefu wa mwenendo wa kisiasa wa Zanzibar ni msingi muhimu wa hofu yetu. Kila unapokaribia uchaguzi Zanzibar, hutokea visa, vikiwemo vile visivyoingia akilini.

Polisi wanapotoa taarifa za namna hii, ni vema wajue kuwa wanatisha wananchi. Na kwa kuwa wananchi wenyewe wanajua mantiki ya taarifa hizo, wanataharuki.

Wale walio karibu na maeneo yaliyodaiwa kulipuliwa, wanaanza kukimbia makazi yao kwa kuhofia kukamatwa na kuswekwa vituoni mwa polisi.

Tunajua hofu zao si za kitoto. Wanajua fika kuwa hawa polisi tayari wameanza kuendekeza "siasa" katika utendaji. Ni siasa hizi ambazo huko nyuma zimekimbiza maelfu ya raia, wengine hadi kwenda kuishi nchi jirani.

Taarifa za milipuko zinakuja wakati Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imesimamisha kazi ya uandikishaji wapiga kura baada ya wananchi kuchoka kunyimwa haki na kuamua kugoma kuandikishwa katika mfumo wa kibaguzi.

Uandikishaji ni wapigakura Zanzibar ni siasa tupu. Wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinataka kutumia uandikishaji kujijengea mazingira ya ushindi, Chama cha Wananchi (CUF) kinasimama kuhakikisha kila raia anayestahili anaandikishwa.

Ukweli ni kwamba kusimama kwa uandikishaji ni aibu kubwa kwa serikali. Hali ni mbaya kwao kwa vile upo ushahidi makini kuwa zoezi hilo la kiraia linaendeshwa kijeshi.

Picha za vyombo vya habari zimeonyesha wazi vituo vya uandikishaji vilivyosheheni askari, wakiwemo wa vikosi vya ulinzi vya SMZ, ambao wanajulikana kwa utendaji wenye upogo.

Penye zoezi la kiraia, makumi kwa makumi ya askari wanatafuta nini kama si kusaidia dola kutekeleza mbinu za kulazimisha yasiyotakikana?

Kumbe tunakosea wapi tukisema kuwa uandikishaji, kama unavyokuwa upigaji kura, unadhibitiwa na dola Zanzibar kwa lengo la kukidhi matakwa ya utawala – ya kuvuruga uchaguzi?

Wakati tunasihi serikali ijiheshimu, tunataka kwanza polisi watoe taarifa ya uchunguzi wa milipuko ya miaka ya nyuma; hapo ndipo watujulishe hili jipya; la sivyo, tutaamini kuwa wametumwa kushiriki mbinu za kuangamiza haki ya raia.

0
No votes yet