Maboresho ya leseni yamejaa karaha


Paschally Mayega's picture

Na Paschally Mayega - Imechapwa 20 July 2011

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

SERIKALI imeleta leseni mpya kwa wanaoendesha vyombo vya moto. Katika mpango huu mpya madaraja ya leseni yameongezeka. Wenyewe wanasema kwamba yamenyumbuliwa.

Kubadili, kwa nia ya kuboresha ni kitendo cha maendeleo. Lakini lazima elimu itolewe kwa wananchi kwa nini imelazimu kufanya mabadiliko hayo. Pia lazima kuweko na uangalifu katika kufanya mabadiliko hayo ili kuzuia kumnyima mtu haki aliyokuwa nayo kwa leseni yake ya zamani.

Na katika utekelezaji wa mabadiliko hayo kusiwepo karaha na kadhia kwa wananchi.

Yamekuwepo malalamiko mengi katika zoezi hili la leseni mpya. Malalamiko katika kuzipata na malalamiko katika kuzitumia. Nitatolea mfano halisi.

Nilifuzu na kutunukiwa leseni daraja la ‘C’ No. 1001182 Julai 16, 1980. Malipo yake yalikuwa shilingi hamsini. Wakati wa kuomba upya au kuihuisha (renew) leseni yangu nilikwenda Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Baada ya taratibu zote wakaniambia watanipa leseni daraja ‘D’. Nikawaambia nimekuja “ku-renew” leseni yangu siyo kupewa leseni mpya. Mazungumzo yetu yakawa kama ifuatavyo:-

TRA – Hii C uliyonayo ni kavu. ‘C’ ya sasa imenyumbuliwa katika madaraja tofauti tofauti.

Dereva - Katika hayo madaraja mimi nipatie lililosawa na ‘C’ hii yangu.

TRA – Ndiyo hii ‘D’ ninayokupatia.

Dereva –Kama gari yangu ni teksi, kwa leseni hiyo nitaruhusiwa kuendesha kwa shughuli zangu kama vile kumpeleka mgonjwa hospitali?

TRA – Hutaruhusiwa.

Dereva – Kama nina daladala nimepatwa na msiba nitaruhusiwa kubeba watu kuwapeleka makaburini kuzika? Au nina sherehe kama harusi, nitaruhusiwa kuwapeleka watu kanisani au sehemu ya tafrija?

TRA – Huruhusiwi.

Dereva – Nimekuwa nikiendesha magari tofauti tofauti kwa muda wa miaka 31 mfululizo. Ni kitu gani kimetokea kwangu mpaka unishushe daraja?

TRA – Kimya.

Dereva – Huoni kama unaninyang’anya haki yangu niliyopewa na Jamhuri kwa cheti cha kuthibitisha uwezo na uhodari wangu katika kuendesha Na. 81749 (Certificate of competence PF140) kilichotolewa tarehe 16-7-1980?

TRA – Kimya

Dereva – Nini kinachofuata?

TRA – Nenda Trafiki

Zamani kazi ya TRA ilikuwa kukusanya kodi au mapato ya Serikali. Hii ya kupangia watu madaraja ya leseni bila kuwatesti wameianza lini?

Msema ukweli mpenzi wa Mungu. Kule Trafiki nilipokewa vizuri sana kuanzia barabarani. Kila chumba nilichoingia nilishughulikiwa kwa haraka bila kuzungushwa wala kuulizwa maswali ya ajabu ajabu.

Wengine waliniita Dokta, wengine wakaniita Mwalimu Mkuu wote walionyesha furaha kuniona. Nawashukuru kwa hilo. Niliuliza maswali machache niliyowauliza TRA na mahojiano yetu yakawa kama ifuatavyo:-

Dereva –Kwa nini unanipa daraja, ‘D’ na ‘B’ na siyo ‘C’ niliyokuwa nayo?

Trafiki – Daraja ‘C’ mpaka ukasome.

Dereva – Kwa nini usinipe huo mtihani wanaofanya wanaoleta cheti niufanye kukuthibitishia uwezo wangu badala ya kunidhulumu haki yangu?

Trafiki – (Huku akicheka) Nakuongezea na hii ya daraja ‘A’ kwa sababu wewe ulikuwa na ‘C’.

Dereva – Kwa nini unashindwa kukithamini cheti kilichotolewa na Serikali ya Jamhuri kupitia kwa Afisa Mkuu Usalama Barabarani Mkoani Iringa tarehe 16-7-1980 kuthibitisha kuwa mtu huyu amethibitisha kuwa ni hodari katika kuendesha kwa usalama barabarani na nimekuwa nikifanya hivyo kwa vitendo kwa miaka 31 mfululizo?

Trafiki – Kimya.

Dereva –Kama gari yangu ni teksi, kwa leseni hiyo nitaruhusiwa kuiendesha kwa shughuli zangu kama kumpeleka mgonjwa hospitali?

Trafiki –Unaruhusiwa.

Dereva – Kama nina daladala nimepatwa na msiba nitaruhusiwa kubeba watu kuwapeleka makaburini kuzika? Au nina sherehe kama harusi, nitaruhusiwa kuwapeleka watu kanisani au sehemu ya tafrija?

Trafiki – Unaruhusiwa. Tunachoangalia ni kuwa huyatumii kufanya biashara.

TANESCO kuna vishoka, TRA Kuna mashoka. Siku ya kwanza tu nilipoingia kuomba fomu alinidaka kijana mmoja na kuniambia, “Mzee hiyo fomu itakusumbua nitakujazia”. Alipoiona TIN yangu akasema, Imetolewa 2006 ni zamani sana. Fanya kitu kidogo upate TIN mpya sasa hivi”. Nikamwambia endelea nayo. Nilitoka.

Niliporudi nikadakwa na mama mmoja mtu mzima. Akanitaka nimpe Sh. 1,000 akanipgie fotokopi. Nilishangaa alivyozing’ang’ania karatasi zangu. Akanitaka nimpe shilingi laki nne halafu atamalizana na watu wa TRA na Polisi wa Trafiki na atanikabidhi leseni daraja ‘C’ bila mimi kuhangaika.

Nilipomuuliza msimamizi kuhusu adha hii alinijibu, “Ndugu yangu tunajua kuwa hawa vishoka wanawaumiza sana wananchi, lakini tutafanyaje? Kila tukiripoti, polisi wanakuja wanawakamata wote lakini baada ya siku mbili wanarudi tena.” Nikakumbuka changudoa wanavyong’ang’aniwa na polisi!

Nikafikiria kwenda kushtaki kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, lakini ‘vichomi vikanibana’ nilipokumbuka jinsi mamilioni ya shilingi za walipa kodi yaliyotumika kumlipia pango katika Hoteli ya anasa.

Kwa muda wa miezi saba tangu aapishwe yametokea matukio mengi ya kutisha na maisha ya raia kupotea, sikumsikia. Nilidhani kasafiri kumbe alikuwa Hotelini!

Uchungu! Watu wamefika mahali hawamwogopi tena Mwenyezi Mungu! Akina mama wanakufa kwa kujifungulia vichakani kwa umaskini wao, viongozi wao wanaitafuta pepo duniani kwa kodi yao watajisumbua na hili la leseni! Nyerere ulale pema peponi!

Umbali kati ya jengo la TRA na ofisi ya Suleiman Kova yule kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, hauzidi mita mia mbili. Mashoka niliyokuwa napishana nayo TRA ndio nilipishana nao ofisi za Trafiki zilizoko chini ya kamanda Kova.

Waliingia na kutoka kila ofisi bila kupanga msitari. Walionyesha ni watu waliokuwa na ushirikiano mkubwa na maafisa wa Polisi na maafisa wa TRA. Mtu mwenye akili timamu akiwaza kuwa Kova anaiacha kero hii iendelee kwasababu ananufaika nayo atakuwa amekosea wapi!? Vishoka waliopo mbele ya ofisi yake wamshinde, majambazi yaliyoko mafichoni atayaweza vipi?

IJP Said Mwema, kwa nini anaruhusu kero hii iwafikishe wananchi mahali wamkashfu hata rais wao kwa kukosa watendaji? Rais wetu ni mwema. Angekuwa na watendaji kama Edward Moringe Sokoine au John Pombe Magufuli wenye dhamana ya kuondoa kero hii kwa wananchi, wengi wangekuwa hawana kazi. Wananchi wangepata haki zao bila kulazimika kuzinunua.

Nani atawaondolea Watanzania kero hii? Itajulikana kesho maana nakwenda kuchukua leseni yangu niliyodhulumiwa. Wacha wenye laki nne waendelee kupata daraja ‘C’ watumalize Watanzania!

Tel. 0713 33 42 39, Email: ngowe2006@yahoo.com
0
No votes yet