Maboya hayatoshi, chakavu


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 21 March 2012

Printer-friendly version

NIMO katika meli iitwayo m.v. Noora. Natoka Tanga kwenda Wete, Pemba. Ninaongea na Ali Khamis anayejitambusha kuwa ni nahodha.

Anasema ni mzaliwa wa Kilwa Masoko, Tanzania bara. Lakini hivi sasa anaishi mjini Zanzibar.

Ninauliza na kuambiwa kuwa meli niliyopanda ina abiria 164 na wafanyakazi wanane. Ninaomba kuona orodha ya wasafiri (manifesto). Ananipa orodha. Ninaisoma.

Nahodha: Kwa nini unakuwa dadisi jinsi hii?

Mwandishi: Ni mara yangu ya kwanza kupanda meli. Nimezoea kupanda kivuko cha Dar es Salaam.

Nahodha: (kicheko)

Katika mazungumzo, nahodha anasimulia jinsi  meli hiyo ilivyowahi kupata tatizo la kuzimika kwa injini ikiwa njiani. Anasema ilichukua nusu saa kuwasha injini nyingine na kuanza safari.

Meli hii ina injini mbili; ya pili inatumika pale inayoendesha ikizima au ikiwa na hitilafu. Lakini kilichonistua ni kwamba ina maboya manane tu ya kuokolea abiria.

Kila boya lina uwezo wa kuokoa abiria 10. Kwa hesabu ya haraka, iwapo maboya yatahitajika kutumiwa, wakati abiria ni 164 kama ilivyokuwa nikiwa melini; basi abiria 84 hawatapata huduma ya uokozi.

Kwa mujibu wa mfanyakazi mwingine melini, ambaye hakutaka jina lake litajwe popote, kila boya linagharimu Sh. 1.5 milioni.

Tabia ya maboya haya ni kutumiwa mara kwa mara. Yasipotumiwa kwa miaka mitatu au zaidi, huwa yanagandana na wakati wa kukunjuliwa huweza kuchanika, ameeleza.

Mtoa taarifa anasema Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchikavu (SUMATRA) hufanya ukaguzi katika meli hiyo mara moja tu kwa mwaka. Anasema ukaguzi hufanywa kwenye injini, maboya na vyakula vilivyomo katika meli.

Je, Sumatra wanajua kisa cha maboya ya m.v Noora?

Nikarudi kwa nahodha Khamis:

Mwandishi: Naambiwa maboya yenu ya siku nyingi. Yamepitwa na wakati. Unajua hilo?

Nahodha: Hilo waulize wenye meli.

Mwandishi: Lakini meli iko mikononi mwako sasa.

Nahodha: Ni kweli. Lakini nakuelekeza kwao ili upate jibu sahihi.

Meli hii ina umri wa miaka 27 Hufanyiwa huduma kwenye bandari ya Mombasa nchini Kenya; kila baada ya miaka miwili.

Nahodha anasema huduma au hata matengenezo madogo hufanya na wafanyakazi wenyewe. Haya ni pamoja na kupaka rangi, kukarabati milango, viti na hata kuzibua pampu za maji au mafuta.

Safari kutoka Tanga kwenda Pemba ilifanyika tarehe 7 mwezi uliopita. Nilirudi Tanga kesho yake. Mara hii meli ilikuwa na abiria 32.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)