Macho bungeni, akili jimboni


William Kapawaga's picture

Na William Kapawaga - Imechapwa 09 June 2009

Printer-friendly version

WAKATI mkutano mrefu zaidi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulianza jana Jumanne kwenye ukumbi wake mkuu mjini Dodoma, karibu wabunge wote wapo njiapanda kwa sasa.

Kila mmoja amejaa mawazo kichwani. Anafikiria hatima yake jimboni. Mbunge – hata yule ambaye amekuwa adimu jimboni kwake kwa sababu hajali thamani ya wapiga kura – anafikiria namna atakavyorudi ukumbini baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwakani.

Mkutano unaoendelea bungeni hutumika kwa mambo makuu mawili: kujadili na kuidhinisha makadirio ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka wa fedha ujao wa 2009/10 ikiwa ni pamoja na kupitisha miswada ya miwili ya sheria ya kuidhinisha matumizi hayo na mabadiliko ya utozaji kodi maeneo mbalimbali; na wabunge kuiuliza serikali maswali mbalimbali.

Fursa ya wabunge kujadili bajeti ya serikali ni muhimu sana kwani mbali na kusaidia kushauri serikali kuhusu mgawanyo wa uwiano wa fedha za kodi, pia huwapa uwanja wabunge wa kueleza kero za majimboni kwao kwa nia ya kuibana serikali kutatua shida za wananchi.

Ila ukweli ni kwamba wabunge watakaofanikiwa kutumia vizuri njia hiyo kuwasilisha malalamiko au kero za wapiga kura wao, ni wale tu ambao wamekuwa wakipita majimboni mwao na kukutana na wananchi na kuwasikiliza.

Hawa wanayajua matatizo yalioko maeneo ya jimboni. Ingawa watakuwa na hofu ya kupigwa kumbo kurudi bungeni mwakani, angalau wanajiamini hawakuudhi wananchi. Walikuwa karibu nao kwa shida na raha.

Hiki ni kipindi cha wabunge wengi kufunga safari majimboni kukutana na wananchi. Wanataka kufahamu kwa karibu shida zao na matumaini yao ili wajenge hoja za kutoa wakati wa mijadala bungeni.

Wakati wanakumbuka wapiga kura wao saa hizi, wanakuna vichwa kujiuliza hatima itakuwaje wakati kumejitokeza wanachama wengine wa vyama vyao wanaotaka ubunge.

Hapo hawajajua wakipitishwa kugombea, watashinda vipi ushindani wa chama kingine chenye nguvu katika jimbo husika. Hii ni kuwepo njiapanda.

Na hiyo ndiyo hali inayowaondoa wabunge wengi katika utulivu wa kujadili bajeti. Sehemu kubwa watakuwa macho bungeni, akili jimboni!

Tayari baadhi ya wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wameanza kulamimikia wenzao kwa viongozi wa juu wa chama; wenyeviti wa mikoa au katibu mkuu, kuwa kuna watu wanajipitisha majimboni wakipiga kampeni za kuwachafua wao wanaowakilisha kwa sasa.

Wiki iliyopita, kulianza malalamiko kwa wabunge wakisema makadirio ya bajeti ya wizara mbalimbali huenda yakaleta mizozo mingi kati yao na mawaziri kwa kuhisi fedha nyingi zimeelekezwa kwenye majimbo yanayopendelea mawaziri.

Ni hoja ya wabunge waliolalamika kwamba mwelekeo huo unatafsiriwa kwamba ni mpango na  mkakati wa mawaziri husika kupiga kampeni ya kuvutia kuchaguliwa tena huku wakisahau wabunge wenzao wasiokuwa mawaziri.

Hiyo inaonesha kuwa raslimali za taifa zinatumika vibaya kwa maslahi ya mawaziri badala ya kuangalia hali halisi ya mahitaji ya kila eneo.

Hali hiyo itasababisha wabunge wengi kutoroka vikao vya bunge ili kupata nafasi ya kujipanga vizuri jimboni ikiwemo kupambana na wanaowaita ‘wavamizi’ dhidi ya matakwa yao ya kujihakikishia kurudi bungeni.

Tafsiri ya haraka inayopatikana ni kwamba wabunge wanaanza kuamka sasa na kufikiria namna ya kujinasua baada ya wengi wao kubweteka mara tu walipochaguliwa kwa kuona miaka mitano ni kama 20. Wanachokifanya, ni sawa na mtu kukumbuka shuka wakati kumeshakucha.

Watanzania wanaamini spika wanayemjua alivyo kweli mtendaji wa “viwango na kasi” atakataa utoro wa wabunge ili kila mmoja ajishughulishe kikamilifu na mijadala ya makadirio ya bajeti ya serikali.

0
No votes yet