Madaraka ni kileo cha watawala


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 09 February 2011

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

CHUKULIA mfano wa Mobutu Sese Seko aliyewahi kuwa rais wa Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Baba yake alikuwa mpishi wa mzungu wakati wa utawala wa kikoloni wa Ubelgiji nchini kwake. Mama yake mzazi alikuwa mhudumu wa hoteli. Familia ya kawaida kabisa.

Miaka 40 baadaye, baada ya kuonja utamu wa madaraka, Mobutu akabadilika. Kabla ya taarifa ya habari ya jioni kuanza, Wazaire walikuwa wakionyeshwa picha ya Mobutu akishuka kutoka mawinguni.

Mtawala huyo alikuwa ni mkristo wa madhehebu ya katoliki. Alijua ni nani ambaye aliwahi kupanda mawinguni katika simulizi za biblia. Alijua pia ni nani atashuka kutoka mawinguni katika siku ya kiyama. Akajifananisha naye.

Akawa anakodi ndege ya aina ya Concorde kwa safari zake fupi. Akajenga uwanja wa ndege kijijini kwake. Akatoa fursa za ajira na biashara kwa ndugu zake kutoka kabila la Gbandi.

Mara moja, Mobutu akaona watu wa kabila lake ndiyo wenye akili kuliko makabila mengine ya Zaire. Ndiyo wenye shida ya fedha kuliko wengine na ndiyo wanaofaa kupewa nyadhifa za uongozi.

Na akajipachika jina la Kuku wa Ngbendi wa Zabanga yaani dume la mbegu. Kwamba kwa sababu ya urais wake, yeye akawa mwanamume mwenye nguvu za kiume kuliko wanaume wote wa kizaire.

Hivyo ndivyo namna madaraka yanavyoweza kubadili mtu. Mtoto huyu wa mpishi ghafla akajifanya hataki kubanana na watu kwenye ndege na mwenye akili.

Siku zote nimekuwa nikishangazwa sana na namna watu wanavyobadilika mara baada ya kupata madaraka. Wanasahau kila kitu na kujiona watu tofauti kabisa.

Inawezekana mtu mlisoma naye darasa moja katika shule ya msingi na alikuwa mwanafunzi wa kawaida kabisa. Anapopata madaraka, atajifanya ana akili kuliko watu wote wanaoishi nchini kwake. Achilia mbali wale aliosoma nao na wakimshinda kwa kila kitu.

Ataenda kwenye klabu ya soka na kufundisha wanasoka mbinu za kushinda mechi ya soka ingawa yeye si mpenzi wa mchezo huo na hajui lolote kuhusu mbinu za soka.

Atakwenda kuhudhuria onyesho la muziki na ataomba apewe kipaza sauti ili aimbe kidogo. Ataeleza namna alivyokuwa mpiga gitaa la besi hodari shuleni ingawa ukweli ni kuwa hakuwahi kuliona gitaa wakati akisoma.

Ndiyo maana najiuliza, madaraka yana nini kinachowafanya watu wabadilike?

Hata kama ana kibyongo, atataka wananchi wake waamini kuwa ni mzuri na anavutia kwa wanawake kuliko Adonis.

Mobutu alijiita dume la mbegu lakini Idi Amin Dada hakuwa na shida ya kujiita hivyo. Yeye alionyesha kwa vitendo kwa kubadili wanawake kila kukicha.

Madaraka yana viagra? Inakuaje wengi wapatapo madaraka hujiona ni wanaume zaidi kuliko enzi zile kabla hawajawa na wadhifa wowote mkubwa?

Madaraka yana nini kinachowafanya watu wabadilike?

Hata mke wa rais au kiongozi naye hubadilishwa wakati mumewe anapokuwa madarakani.

Hebu chukulia mfano wa Leyla Trabelsi, mke wa aliyekuwa rais wa Tunisia, Zine Al Abidine Ben Ali.

Huyu alikuwa mwanamke wa kawaida kabisa kabla mumewe hajamuoa baada ya kufiwa na mkewe wa kwanza.

Ben Ali alipomuoa akaanza kuonyesha namna madaraka yake yalivyombadili Leya. Mama huyo akaanzishiwa NGO yake iliyoitwa SAIDA (jina la mama mzazi wa Leya).

Ghafla yeye akawa ndiye mwokozi wa walemavu. Akawa mwokozi wa wanawake wanaonyanyaswa. Akawa mtetezi wa wagonjwa wa kansa.

Kote huko kwenye mashirika yake hayo ya utetezi, mapesa yakamininika. Leo utasikia Leyla kafanya hiki na kesho kile. Ben Ali akizungumza kutoka Tunis, Leyla anazungumza kutoka Sousse.

Mumewe alipoamua kukimbia nchi, ni Leya ndiye aliyekwenda Benki Kuu ya Tunisia na kuamuru apewe tani moja na nusu ya dhahabu na akaondoka nayo kwenda Saudia.

Huyu ndiye yuleyule Leyla ambaye hakuwa lolote wala chochote kabla hajaolewa na Ben Ali. Madaraka ya mumewe yamemfanya aone hawezi kuishi bila ya dhahabu na fedha!

Madaraka yana nini kinachotufanya wanadamu tubadilike?

Miaka michache iliyopita, aliyewahi kuwa waziri wa fedha, Basil Mramba, aliwahi kuwaambia Watanzania kuwa ikibidi watakula nyasi ili mradi rais wao, Benjamin Mkapa, anunuliwe ndege ya kifahari.

Nini hasa kilichomfanya Mramba aone Watanzania wanaweza kugeuka mbuzi au ng’ombe wakala majani ali mradi Mkapa asafirie ndege ya aina ya Gulfstream? Ni madaraka tu.

0
Your rating: None Average: 5 (2 votes)