Madini ya uranium na ‘ukoloni mpya’ uliotabiriwa


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 30 June 2010

Printer-friendly version
Gumzo

YALIYOTABIRIWA mwaka 1953, kwamba mataifa ya Ulaya yatarudi baada ya nusu karne, kusaini mikataba ya kuchimba “madini ya atomiki,” sasa yametimia.

Shuhuda aliyefanya kazi ya kutafiti madini akiwa na Wajerumani na baadaye Waingereza, ananukuriwa akisema wazungu walitabiri “kurudi” – jambo ambalo limetafsiriwa kuwa “ukoloni mpya kwa njia ya biashara.”

Hii ilikuwa katika kijiji cha Ilindi kata ya Ilindi tarafa ya Bahi ambako leo hii, yapata miaka 57 tangu utabiri huo, makampuni ya kigeni yanakimbizana kuanzisha uchimbaji madini ya uranium.

Madini ya uranium, pamoja na kuwa chanzo kikuu cha nishati ya umeme, ni madini ya aina ya pekee yanayotegemewa katika utengenezaji wa silaha za nyuklia.

“Kwa sasa (1953) madini hayatachimbwa kwa sababu Tanganyika inatawaliwa na Uingereza chini ya Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa (UNO),” aliyekutana na shuhuda wa utabiri anakariri aliyoambiwa.

“Baada ya muda mfupi, Tanganyika itapata bendera yake. (Hivyo) Watanganyika mnatakiwa msome ili muweze kujua sheria na utawala ili mataifa ya Ulaya yatakapokuja yasitokee ‘magomvi’ ya wenyewe kwa wenyewe,” anakaririwa shuhuda mwaka 1989 alipokuwa na umri wa miaka 94.

Mzee Mussa Chizumi (64) anakumbuka aliyosimuliwa. Anasema Wajerumani walifanya utafiti wa madini Bahi mwaka 1913 na kugundua kuwa “hapa ni mfuko (hazina)” au eneo lenye raslimali ya madini aina ya uranium.

Chizumi ambaye ni mvuvi na mkulima, anakiri kusimuliwa historia hiyo na Mtanzania aliyefanya kazi aliyoita ‘usoroveya’ (utafiti – savei) wa madini akiwa na Wajerumani mwaka 1913 na baada ya Vita vya Pili akawa na Waingereza.

Anasimulia, “Mwaka 1989 nilikutana na mzee mmoja niliyemfahamu kwa jina la Paulo. Nilikutana naye katika shughuli za uvuvi kwenye kambi ya Igose kwenye Bwawa la Bahi (wengine huita Ziwa Bahi). Wakati huo alikuwa na umri wa miaka 94.

“Mzee Paulo alizoea kuniagiza ninaporudi kambini niwe nampelekea ubuyu kutoka mbuyu wa Waisoche. Aliniambia kwamba aliufahamu mbuyu huo tangu akiwa na umri wa miaka 18, yaani mwaka 1913.

“Yeye kwa asili alikuwa Mpogolo kutoka Mahenge ila alilelewa na misheni ya Kijerumani. Kutokana na elimu aliyopata, Paulo alitumiwa na Wajerumani katika shughuli za usoroveya katika eneo la Bonde la Ufa.

“Aliniambia kuwa walitembea kwa miguu kutoka Ziwa Eyasi wakifuata chanzo cha Mto Bubu unaomwaga maji katika Bwawa la Bahi au mbuga ya Sulungai. Kambi yao ya utafiti ilikuwa kwenye mbuyu wa Waisoche kwenye mbuga hiyo. Katika utafiti wao, waliweka bikoni (alama) tano katika maeneo tofauti ya Bwawa la Bahi.

“Alisema shughuli za utafiti zilivurugika baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia na baadaye Vita vya Pili kwani naye alichukuliwa na kupelekwa vitani. Baada ya kumalizika vita, akiwa kwenye Jeshi la Waingereza, walianza kupangiwa kazi, kila mmoja na ujuzi wake.

“Baada ya Waingereza kugundua kuwa alikuwa mtaalamu wa masuala ya utafiti na aliwahi kushiriki katika kazi hiyo chini ya utawala wa Kijerumani, walimchukua na kumtumia kufuata nyayo walizopita Wajerumani katika utafiti wao.

“Aliniambia kuwa kazi hiyo waliifanya kuanzia mwaka 1953. Mzee Paulo ndiye aliwaongoza hadi katika kijiji cha Ilindi kata ya Ilindi tarafa ya Bahi ambako waliweka bikoni nyingine.
“Alisema Waingereza walimpa pesa kwa kufanikisha utafiti wao wa marudio. Alisema walipigilia upya bikoni katika maeneo ambako Wajerumani walikuwa wamesimika bikoni; kwenye Bwawa la Bahi na mwaka 1954 wakafunga kambi ya utafiti na kutamka kuwa madini ya atomiki ni mengi sana.

“Mzee Paulo alinisimulia kuwa Waingereza walimwambia kuwa kwa sasa madini hayatachimbwa kwa sababu Tanganyika inatawaliwa na kwamba baada ya nusu karne hivi au zaidi, mataifa ya Ulaya yatarudi kusaini mikataba ya kuchimba madini haya.

“Mzee Paulo aliambiwa na Waingereza hao kwamba madini yoyote yaliyo chini ya ardhi ni urithi wa dunia; kila taifa lina haki ya kuyapata kwa kufuata sheria,” alisema Mzee Chizumi katika mahojiano na mwandishi wa makala hii wiki mbili zilizopita mjini Bahi.

Baada ya maelezo hayo na kwa vile walishamlipa ujira wake wa mwisho, watafiti wa Ulaya walimwambia, “Kwaheri Paulo.”

Hayo ni masimulizi tu, lakini mwaka 2006 akiwa katika kijiji cha Kibumagwa katika Wilaya ya Manyoni mkoani Singida, Chizumi alianza kuona magari yakipita na alipofuatilia aliambiwa wanafanya utafiti wa madini ya uranium katika Bonde la Ufa.

“Ndipo nikakumbuka masimulizi yale ya Mzee Paulo ya mwaka 1989. Mwaka uliofuata yule waziri wa nishati na madini, Nazir Karamagi alithibitisha bungeni kuwa madini ya uranium yamegundulika Bahi, Dareda, Selous na Madaba,” anasema Chizumi.

Taarifa za kitafiti hazionyeshi ushiriki wa Wajerumani kugundua hazina hiyo isipokuwa Waingereza mwaka 1953 na baadaye wanajiolojia wa Tanzania mwaka 1977.

Taarifa iliyotolewa 19 Julai 2009 na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngereja inaonyesha utafiti wa awali wa kijiolojia na kijiofizikia wa mashapo yenye madini ya uranium nchini, ulifanywa na serikali miaka ya kati ya 1976 na 1980. Utafiti huo ulifanywa na kampuni ya Geosurvey International kwa niaba ya serikali.

Vilevile kati ya mwaka 1980 na 1982 kampuni nyingine ya Ubernizerburg ya Ujerumani ilifanya utafiti katika maeneo yaliyohusisha utafiti uliotangulia na kuonyesha kuwa katika mikoa ya kati, kusini na kaskazini kulikuwa na uwezekano wa kupatikana mashapo yenye hazina ya kutosha ya madini ya uranium inayoweza kuchimbwa kibiashara.

Hivi sasa wanajiolojia Godson Kamihanda (mzungu) na Emmanuel Massano wa kampuni ya Tanzoz Tanzania Limited wanafanya utafiti katika mazingira magumu vijiji vya kata ya Ilindi wilayani Bahi. Hii ni moja ya makampuni 70 yanayofanya utafiti wa uranium nchini.

Utafiti huu unahusisha uchimbaji wa mashimo makubwa na ya kina kirefu katika mashamba ya wananchi na kuchunguza safu mbalimbali za udongo.

Hadi hatua hiyo ya uchunguzi na hasa kugundulika kwa madini hayo, hakuna juhudi zozote zilizofanywa na serikali – kwa ngazi yoyote ile – au watafiti wenyewe, kuwaelimisha wananchi wa Bahi kuhusu hatima yao.

Hakuna mwananchi anayejua iwapo atahamishwa, atahamishiwa wapi, atafidiwa, atafidiwa na nani na chini ya sheria ipi, pindi uchimbaji wa uranium utakapoanza.

Msimamo wa serikali ni kuruhusu makampuni ya nje kuchimba madini hayo na msimamo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bahi ni sawa na wa serikali.
Taarifa ya waziri wa nishati inasema uchimbaji wa uranium unatarajiwa kuanza mwaka 2012.

Tayari kumeanza kuchemka hata kabla uchimbaji kuanza. Mwaka juzi, madiwani wa CCM walimkalia kooni mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Bahi, Omari Badwel na kumvua wadhifa huo kwa kosa la “kufungua mkutano uliokuwa unajadili mazingira ya bonde hilo na kuwepo kwa uranium.”

Mwaka jana Naibu Waziri wa Madini na Nishati, Adam Malima alipata shida kueleza athari za madini hayo kwa binadamu pale yatakapokuwa yameanza kuchimbwa. Alikuwa mbele ya wakazi wa Msembeta, Ilindi na baadaye kwa wakazi wa Bahimwanachugu, Bahisokoni, Bahimakulu, Bahinagulo, Lionii, Chimendeli na Chisumuni.

Kampuni ya Mantra Resources ndiyo imekabidhiwa kazi ya kuchimba uranium katika maeneo ya Selous, Mkuju wilayani Namtumbo wakati Uranex itachimba uranium Bonde la Bahi.
Serikali imekamilisha mikataba hiyo huku ikiwa bado haijatoa elimu kwa wananchi kuhusu hatima yao. Suala hilo linafanywa siri, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu huku Kampuni ya Tanzoz Tanzania Limited ikiendelea kufanya utafiti wa mwisho Bonde la Bahi.

Nyaraka mbalimbali kutoka kwenye mtandao kuhusiana na utafiti na uchimbaji, zinathibitisha kuwepo kwa hazina kubwa ya uranium kama alivyosimulia Mzee Paulo.
Jambo ambalo halijawekwa wazi ni juu ya miliki ya eneo la uchimbaji katika Bonde la Bahi. Taarifa ya Alan Phillipe, ofisa mtendaji mkuu wa International Gold Mining Limited (TSX Venture) ambayo 18 Januari 2010 ilibadili jina na kujiita "Central Iron Ore Limited”, inathibitisha hilo.

Ofisa mtendaji mkuu huyo anaonyesha kwamba kampuni yake imeingia mkataba na watu binafsi wa kununua ardhi yenye ukubwa wa kilomita za mraba 906 za makazi ya watu katika eneo lenye utajiri mkubwa wa madini ya uranium ambalo linapakana na Bwawa la Bahi.

“Ununuzi huo utafanya jumla ya eneo linalomilikiwa na kampuni hiyo katika maeneo manne ya makazi ya wananchi ya ukanda wa Bahi/Manyoni wenye uranium kufikia kilomita za mraba 2,365,” inasema taarifa hiyo ya 15 Mei 2008.

Maeneo mawili kati ya hayo yanakutana katika mpaka wa magharibi na eneo moja linakutana na mpaka wa kusini wa Uranex NL (ASX) ambalo lina kitalu cha Manyoni C1.
Taarifa za utafiti zinaonyesha kwamba madini ya uranium yanapatikana katika mikoa ya kati (Singida na Dodoma), mikoa ya kusini (Mtwara na Ruvuma) na katika mikoa ya kaskazini ya Manyara na Arusha.

Katika mikoa ya kati madini yanapatikana katika wilaya za Bahi, Kondoa, Manyoni na Singida vijijini; mikoa ya kusini ni katika wilaya za Namtumbo, Songea, Newala, Tunduru na Nachingwea; wakati kaskazini ni maeneo ya Galapo, Ziwa Manyara, Minjingu, Mbulu na Simanjiro.

Kwa upande wa Bahi eneo la Kisalalo ambalo liko umbali wa kilomita mbili na nusu kutoka makao makuu ya wilaya ya Bahi, ndilo linatajwa kuwa na madini mengi ya uranium.
Watafiti wamewaarifu wakazi wa Bahimakulu, kwenye uwanda mkubwa wa nyasi za kulishia mifugo na eneo la kilimo cha mpunga, kilomita 15 kutoka Mwanachugu, kwamba hapo ndipo kitajengwa kiwanda cha kuchenjua uranium.

Shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa uranium zinatarajia kutibua na hata kupoteza kabisa kilimo cha mpunga, mahindi, uwele, ufuta na karanga.

Aidha, uvuvi, utengenezaji chumvi na ufugaji, vinaweza kufutwa, pamoja na maeneo mengi ya kihistoria kama Kanisa Katoliki la Bahi lililojengwa mwaka 1912 ili kupisha uchimbaji wa uranium.
Itabaki historia kuwa hapo zamani za kale wakazi wa Mwanachugu mkoani Dodoma walikuwa wakifanya biashara na watu kutoka makabila mbalimbali nchini.

Wasandawe ndio walikuwa maarufu na umaarufu wao ulitokana na mifuko ya ngozi waliyokuwa wakitumia kubeba bidhaa. Mifuko hiyo ya ngozi iliitwa ‘bahi’ na ndiyo chanzo cha eneo hilo kuitwa Bahi.
Awali Bahi kilikuwa kijiji tu; baadaye kikawa kata, halafu tarafa, mji mdogo na leo hii ni wilaya yenye makao yake katika kilima kidogo cha mawe, Mwanachugu.

Bahi imekaa juu ya utajiri wa mabilioni ya shilingi yanayoelezwa kwa wingi wa madini ya uranium ardhini. Ni mali ya wana-Bahi. Ni mali ya taifa.

0
No votes yet