Madiwani amkeni


editor's picture

Na editor - Imechapwa 07 March 2012

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

MABARAZA ya madiwani ndio mihimili mikuu ya ulinzi na hifadhi ya raslimali za taifa katika manispaa, halmashauri za miji ya majiji nchini.

Kupitia mabaraza haya yanayoundwa na madiwani waliochaguliwa na walioteuliwa kupitia viti maalum, wananchi wanatarajia kunufaika na matumizi mazuri ya fedha za umma na raslimali nyinginezo.

Madiwani wanapaswa kufahamu kuwa kama wabunge walivyokabidhiwa jukumu la kuisimamia serikali, basi na wao, kisheria, wanawajibika kusimamia utendaji wa halmashauri za miji na majiji.

Katika hali ambayo inaonekana kuenea kwa kasi nchini ya kukithiri kwa vitendo vya kifisadi, imedhihirika kuwa watendaji wengi wa halmashauri ndio wanaohusika.

Watendaji wanaokabidhiwa dhamana za kutumikia wananchi kwenye halmashauri, wamekosa uaminifukwa kwa kuwa wameamua kutumia nafasi zao kujinufaisha kwa maslahi binafsi.

Ukweli huu unathibitishwa na yanayotokea katika halmashauri mbalimbali. Miradi ya maendeleo inakwama na ile iliyotekelezwa imekwenda kwa viwango duni visivyokidhi au kuendana na thamani ya fedha zilizotumika.

Ubadhirifu unaofanywa unafikia mamilioni ya shilingi kila mwaka. Ufisadi hufanywa kwa kuiba fedha zilizotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwemo maji, elimu na kilimo.

Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ndio ushahidi mzuri wa hili. Nyingi zimekuwa zikifichua ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma unaofanywa na watendaji.

Pale inapobainika kuwa watendaji katika halmashauri wametumia vibaya raslimali za umma, lazima mabaraza ya madiwani yasimame imara na kuchukua hatua zinazoonyesha madiwani wamekerwa na ufisadi na wanataka mabadiliko.

Ni jukumu lao kutoa maamuzi yanayotoa fundisho kwa watendaji na wale wanaoshirikiana nao.

Tunatoa msisitizo huu kwa sababu kubwa kwamba katika halmashauri nyingi imebainika watendaji hutumia fedha kushawishi madiwani kuidhinisha matumizi mabaya ili tu kujenga ukuta wa kujikinga mipango yao miovu itakapokuja kukwama.

Mabaraza ya madiwani yatatenda haki na kutimiza wajibu wao iwapo siku zote watakuwa mbele kuchukua hatua haraka pale tatizo linapojitokeza badala ya kusubiri mambo kuharibika na wao kuja kuingia kutafuta ufumbuzi.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)