Madudu mengine ya Kikwete haya hapa


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 19 May 2010

Printer-friendly version
Rais Jakaya Kikwete

RAIS Jakaya Kikwete yuko hatarini kubebeshwa kashfa mbili kubwa, MwanaHALISI limegundua.

Kashfa ya kwanza inahusu chaguo lake la Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana CCM (UV-CCM), Hamad Masauni Yussuf anayetuhumiwa kughushi vyeti vya kuzaliwa.

Kashfa ya pili ni ya naibu waziri wake kuwaambia wapigakura wa mkoa wa Kilimanjaro kuwa hata wasipompigia kura, Kikwete atashinda tu.

Kashfa hizi zinakuja wakati imebaki miezi mitano kufikia uchaguzi mkuu, 31 Oktoba mwaka huu.

Lakini kashfa hizo zimetanguliwa na nyingine ya wiki mbili zilizopita, pale rais aliposema kuwa hahitaji kura 350,000 za wafanyakazi iwapo watatumia uzito wa kura zao kudai nyongeza ya mishahara aliyosema serikali yake haina uwezo wa kulipa.

Hamad Masauni Yussuf ana nyaraka mbili zinazoonyesha alizaliwa tarehe mbili tofauti.

Cheti cha kuzaliwa kinaonyesha kuwa alizaliwa 3 Oktoba 1979 wakati nyaraka za Uhamiaji za kupatia pasipoti zinaonyesha alizaliwa 3 Oktoba 1973.

Wakati akiwasilisha fomu zake za kugombea ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kupitia UV-CCM mwaka 2007, Masauni alitumia cheti kinachoonyesha alizaliwa mwaka 1979 katika hospitali ya V.I. Lenin, Zanzibar.

Cheti kinachoonyesha amezaliwa 3 Oktoba 1979 chenye Na. 00023509 kilitolewa 15 Juni 2007. Ni cheti hiki ambacho Masauni alitumia kugombea ujumbe wa NEC na uenyekiti wa UV-CCM.

Lakini nyaraka za Uhamiaji zinazoonyesha kuwa aliishaomba pasipoti mara mbili, zinathibitisha kuwa alizaliwa 3 Oktoba 1973.

Nyaraka zinaonyesha kuwa pasipoti yake ya zamani ni Na. A 0300026 iliyotolewa Zanzibar; wakati pasipoti aliyonayo sasa ambayo alikabidhiwa 16 Februari 2006 ni Na. AB 705604.

Tofauti ya mahali pa kuzaliwa inajitokeza katika nyaraka hizi mbili. Wakati moja inasema alizaliwa hospitalini V.I. Lenin, nyingine inasema Masauni alizaliwa Kisimamajongoo, wilaya ya Mjini, mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Kwa kutumia nyaraka hizi, baadhi ya viongozi ndani ya UV-CCM wamezua kasheshe wakitaka Masauni, aliyebebwa na Kamati Kuu ya CCM chini ya uenyekiti wa Kikwete, ang’olewe.

Kwa mujibu wa kanuni za UV-CCM, mgombea wa nafasi yoyote ya uongosi sharti awe na umri usiozidi miaka 30 anapokuwa anaingia madarakani.

Suala hili linamgusa zaidi Rais Kikwete kwa vile ilikuwa chini ya uongozi wa kikao cha CC, wagombea uenyekiti ngazi ya taifa kutoka Bara, waliwekwa kando na kuchukuliwa wagombea kutoka Zanzibar.

Wagombea kutoka Zanzibar, akiwemo Masauni, walikuwa wameomba nafasi ya makamu mwenyekiti. Kutoka bara, waliokuwa wameomba nafasi ya mwenyekiti ni Beno Malisa, Hussein Bashe na Zainab Kawawa.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari vya gazeti hili, kuvuja kwa taarifa za Masauni kudanganya umri zimeibuliwa na wapinzani wake wa kisiasa visiwani Zanzibar, hasa baada ya kutaka kugombea ubunge katika jimbo la Kikwajuni.

“Unajua yule kijana alisahau kuwa alikuwa anatupa mawe wakati akiwa katika nyumba ya vioo. Wenzake walikuwa wanamvutia pumzi. Alipoingia wakamuingiza kitanzini,” anasema kiongozi mmoja wa CCM Zanzibar.

Inaelezwa kwamba Masauni alikuwa na mivutano ya muda mrefu na Naibu Katibu Mkuu wa UV-CCM, Mohammed Moyo na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Saleh Ramadhani Feruzi.

Feruzi ni mmoja wa wanaotajwa kuwania ubunge katika jimbo hilo kupitia CCM. Moyo anatajwa kuwania ubunge katika jimbo la Kwahani ambako mbunge wake wa sasa ni Dk. Hussein Mwinyi.

Gazeti hili liliwahi kuandika miezi mitatu iliyopita kuwa kuna mgogoro ndani ya UV-CCM na kwamba ulikuwa unahatarisha uenyekiti wa Masauni.

Wanaomsakama Masauni walitajwa kuwa Ridhiwan Kikwete, Makamu mwenyekjiti Beno Malisa na Mohammed Moyo ambaye ni naibu katibu mkuu wa umoja huo Zanzibar.

Wakati viongozi hawa hawajawahi kukana njama hizo, UV-CCM taifa ilitoa taarifa ya kukana mgogoro ndani ya umoja huo.

Taarifa zilizopatikana wakati gazeti likienda mitamboni zilisema kabrasha la tuhuma dhidi ya Masauni tayari limefikishwa mezani kwa Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Kamati Kuu ya CCM ilitarajiwa kukutana keshi jijini Dar es Salaam, kujadili, pamoja na mambo mengine, hali iliyojitokeza katika UV-CCM.

Kwa upande mwingine ni Dk. Chami aliyetoa andishi linalosadikiwa kukejeli wapigakura katika jimbo lake.

Anadaiwa kuandika kwenye mtandao wa intaneti, “Ninachosema ni kwamba, Kikwete atachaguliwa tu hata kama Kilimanjaro yote watamnyima kura.”

Kauli ya Dk. Chami, ama kwa kuagizwa au kwa kujituma mwenyewe, imewastua wapigakura mkoani Kilimanjaro ambao wamemjibu kwa ukati kwa njia hiyo ya mtandao na wenginme kusema amewanyanyapaa.

Katika andishi lake, Dk. Chami amesema, “…kumbukeni tulivyomnyima (kura) shemeji yetu Mkapa (Benjamin William) na bado mikoa mingine ikamfanya Rais wa Tanzania).

Dk. Chami ametoa kauli hiyo zikiwa wiki mbili tangu Rais Kikwete atamke hadharani kuwa kama wafanyakazi wanataka kutumia uwezo wao wa kura kuweka madai ambayo serikali haina uwezo nayo, basi hataki kura zao.

Wafanyakazi wakiongozwa na Shirikisho la Vyama vya wafanyakazi nchini (TUCTA), ilikuwa imeitisha mgomo usio na ukomo nchini kote hapo 5 Mei lakini Rais Kikwete aliuzima kwa vitisho kuwa polisi watawatia ngeu.

Dk. Chami alikuwa akijibu kile kilichoitwa malalamiko ya wananchi wa Uru, waliokuwa wanakumbushia ahadi ya Rais Kikwete ya kujenga barabara mkoani humo.

Katika waraka wake, Dk. Chami anasema, “Ni kweli Mheshimiwa rais aliahidi kuzijenga kwa kiwango cha lami barabara mbili (na siyo tatu kama ujumbe wa Dr. Kiwale unavyoonyesha –mbili za Kibosho na moja ya Uru) katika jimbo la Moshi Vijijini.”

Anasema, barabara ya kwanza ni ile inayoanzia Rau Madukani kupitia Mawela, Mengeni, Sokoni, Uru Sekondari na kuishia Njari.

Barabara ya pili ni ile ya Kibosho inayoanzia Kibosho Shine kupitia Sambarai, Kindi Parish, Mawaleni, Umbwe kwa Rafaeli, Mango Parish, Kwa Mangi, Usagara, Chuo Kikuu cha Masoka, Kirima, na kuishia International School Moshi.

Hata hivyo, akiandika kwa njia ya kujibu madai ya waibua hoja kwenye intaneti, Dk. Chami anasema, “Rais huyu ana ajenda gani hadi awadanganye wana Moshi Vijijini ili tu tumpe kura na baadaye atuache kwenye mataa kana kwamba Moshi Vijijini tuna kura ya turufu,” anahoji.

Akiandika kama vile anagombana, Chami anasema, “Ninachosema ni kwamba, Kikwete atachaguliwa tu hata kama Kilimanjaro yote watamnyima kura.”

Hata hivyo, mbunge huyo ameahidi kutekeleza ahadi zake, pamoja na hii ya barabara ya Uru.

MwanaHALISI liliwasiliana na Chami ili kupata maelezo yake kuhusu waraka aliousambaza kwa njia ya mtandao wa intaneti.

Akiongea kwa sauti ya ukali na iliyojaa vitisho, kwanza Chami alikiri kwamba waraka huo ni wake.

Hata hivyo, alisema maelezo aliyoyatoa katika waraka huo hayakuwa kwa ajili ya vyombo vya habari, isipokuwa alikuwa ameyaandaa maalum kwa watu wa Moshi Vijijini na mkoa wa Kilimanjaro.

Alipoelezwa kwamba gazeti liko tayari kumpelekea taarifa zake ili aweze kuzithibitisha, Chami alikubali na hatimaye kukiri kuwa huo hakika ulikuwa waraka wake.

Chami, hata hivyo, alisema waraka huo “umehaririwa sana.” Akataja kifungu kinachohusu barabara iliyopo nyumbani kwa waziri mkuu.

Alipoulizwa nini alichokiandika katika waraka huo kuhusu barabara hiyo, Dk. Chami alishindwa kueleza, badala yake alitishia kupeleka mahakamani gazeti hili iwapo litachapisha taarifa hizo.

Matukio mbalimbali ndani ya CCM yanaendelea kumpa Rais Kikwete wakati mgumu.

Katika muda mfupi Kikwete ameshuhudia migogoro ndani ya Jumuia ya Wazazi, minyukano, matusi na kutuhumiana ufisadi ndani ya Umoja wa Wanawake (UWT) na migogoro inayohusu miradi ya kiuchumi ndani ya UV-CCM.

Si hayo tu, minyukano ndani ya bunge imeleta mgawanyiko mkubwa ndani ya chama na serikali na kumweka pabaya rais ambaye amekuwa akituhumiwa kushindwa kuchukua hatua.

Miezi mitano hadi uchaguzi mkuu, meli ya Kikwete – CCM inayumba na wachunguzi wa mambo wanasema rais akendelea kubanwa kwa kasi hii, huenda kampeni yake ya urais ikaathirika vibaya.

0
Your rating: None Average: 4.1 (7 votes)
Soma zaidi kuhusu: