'Mafahali wa MULEBA: Ni Tibaigana, Tibaijuka, Masilingi


Serapion Damian's picture

Na Serapion Damian - Imechapwa 24 February 2010

Printer-friendly version

ITAKUWA piga-nikupige mwaka huu katika Jimbo la Uchaguzi la Muleba Kusini; na tayari michuano imeanza kimya kimya kuwania ubunge jimboni humo.

Wanaotajwa kuwa katika kinyang’anyiro mwaka huu ni Ni Alfred Tibaigana, Anna Tibaijuka na Wilson Masilingi, mbunge anayemaliza muda wake.

Kwa mazingira ya Muleba, ni “ngoma mzito,” kwani wote ni maarufu na mashuhuri. Anayebisha kuwa mwanamke hawezi kuwa “fahali” anajidanganya.

Wakati Masilingi amejichimbia jimboni kiasi cha kutoonekana kwenye Mkutano wa 18 wa Bunge uliomalizika mjini Dodoma hivi karibuni, Tibaigana na Tibaijuka wametajwa kufanya maandalizi.

Kinachoweza kupunguza makali ya ushindani ni matarajio ya kuwa na jimbo jipya Muleba Kusini. Kuna maombi ya wilaya ya kutaka lianzishwe jimbo litakaloitwa Muleba Magharibi.

Hili litamega kata 19 za jimbo la zamani kwa kuchukua kata za Nshamba, Ikondo, Ijumbe, Buganguzi, Kishanda, Kibiriza, Bulugora, Kashasha, Biirabo na Kibanga.

Kata zitakazobaki katika Muleba Kusini, iwapo Tume ya Uchaguzi itakuwa imeridhia uanzishwaji wa jimbo jingine ni Muleba, Buleza, Magata, Kasharunga, Kyebitemba, Karambi, Kimwani, Mazinga, Mubunda na Kagoma inayotarajiwa kukatwa kwenye jimbo la Muleba Kaskazini.

Hili likifanyika litapunguza ushindani. Anna Tibaijuka anaweza kubaki Muleba Kusini na Masilingi na Tibaigana wakamenyana Muleba Magharibi.

Kama mpango wa kugawa jimbo hautafanikiwa, kutakuwa patashika nguo kuchanika; na tayari imeanza. Mjini Muleba kuna taarifa kuwa makundi ya vijana na watu wazima yameanza kutafuta “nani ana nini” na nani mwepesi wa “kuachia,” tofauti na “mkono wa birika.”

Mbali na hao, padri mmoja wa parokia ya Kijwile aliyetajwa kwa jina moja, Anchileus ametajwa kuwa upande wa Anna Tibaijuka na kwamba anaandaa waumini “kufanya kazi.”

Hata hivyo, padri huyo alipohojiwa kwa simu Jumatatu, kuhusu kumuunga mkono Tibaijuka, alisema “Kwa nature ya kazi yangu, siwezi kufanya hivyo. Lakini nasikia anaweza akagombea na huyu ni muumini katika parokia yangu.”

Padri huyo alisema, “Kama Mtanzania, nina mapenzi yangu; naweza nikachagua mmoja maana nitapiga kura.”

Kwa upande mwingine Harid Kahahuza, aliyekuwa mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya Muleba, ametajwa kuwa mstari wa mbele kumtetea “mama.”

Baadhi ya wafuatiliaji wa masuala ya siasa walinieleza mjini Muleba wiki iliyopita kuwa Kahahuza anataka kugombea udiwani kwa mara nyingine.

Kuna mpango wa kugawa Kata ya Magata ambako Kahahuza ana “uhakika” wa kuwa diwani wa kata mojawapo, ili hatimaye agombee na “bila shaka” kupata umeya wa mji wa Muleba.

Mji huu unatarajiwa kupewa hadhi hiyo hivi karibuni, taarifa za hapa zimeeleza. Kahahuza hakupatikana kuongelea nafasi yake katika kambi hiyo.

Vijana mjini hapa wamemtaja Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM-W), Hemed Kantangayo na mwenyekiti wa sasa wa halmashauri Chysant Kamugisha kuwa baadhi ya wanaoshughulikia uteuzi wa Anna Tibaijuka.

Wakati Kamugisha hakupatikana kusema lolote, Kantangayo alisema, “Ni mapema mno. Kama chama, wakati wake bado. Sasa hivi mtu anaweza kutangaza nia na ninajua Tibaigana tayari ameeleza; sina msimamo binafsi. Wagombea wote ni wetu.”

Kijana mjasiriamali aliyetajwa kwa jina moja, Nyerere aishiye mjini Bukoba na Joan Mary Rwegasira, diwani wa kuteuliwa anayetarajia kugombea nafasi hiyo kata ya Ijumbe, nao wametajwa kumsaidia Tibaijuka.

Nyerere hakuweza kupatikana kwa simu yake ya mkononi lakini diwan Rwegasira alikataa katakata kuzungumzia suala hilo kwa kusema “siwezi kuzungumza na mwandishi ambaye simjui.”

Taarifa zinasema baadhi ya wapigadebe ambao hawajajitaja rasmi walioko upande wa Tibaigana walikwishahudhuria vikao vya awali vya Alfred Tibaigana.

Kijana mmoja aliyetaka jina lake lisitajwe gazetini amenieleza kuwa hata Kahahuza na Nyerere walikuwa upande wa Tibaigana na kwamba Nyerere, mwenye “udugu” na Tibaijuka, anasubiri mama huyo atangaze rasmi kuwa anagombea ndipo ahame kambi.

Hata hivyo vijana wengi nilioongea nao mjini Muleba wanasema wanasubiri Anna Tibaijuka atangaze jina ili waweze “kumchota.”

Bali Alfonce Kabalimu wa Biirabo amenieleza, “Huyu ni profesa wa uchumi. Ameshika nafasi za juu za uongozi kimataifa. Akigundua utapeli anajua la kufanya.”

Hapa Masilingi na Tibaigana wakoje? Hata jimbo likigawanywa, itabidi wapambane kwenye kura za maoni katika jimbo jipya la Muleba Magharibi. Vyovyote iwavyo watabaki kapu moja.

Bali Masilingi, kijijini kwake, anatawaliwa na mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Hii ni ishara kuwa hata wanakijiji wake waliishasema, liwe na liwalo.

Taarifa za Masilingi kugombana na mwekezaji aliyepewa ardhi kujenga shule zimeenea kote jimboni. Baada ya mwekezaji kuanza kujenga, naye Masilingi anadaiwa kuanza kujenga katika eneo hilohilo.

“Unajua, mwekezaji tayari amepewa katazo la mahakama kuzuia Masilingi kujenga ndani ya viwanja hivyo, lakini anaendelea,” ameeleza Sebastian Kagalala.

Kauli hiyo inaungwa mkono na Kantangayo anayesema “mgogoro wa Masilingi na mwekezaji unazorotesha maendeleo ya elimu. Tunakabiliana nao maana malumbano hayajengi. Lazima yamalizike.”

Lakini Masilingi anakana kuwepo zuio la mahakama. Amesema ujenzi unaendelea na kwamba ameahidiwa na wizara ya elimu kupeleka wakaguzi ili shule iweze kufunguliwa.

Kuhusu uwezo wake wa kupambana na Tibaigana, Masilingi alisema, “Huyu ni mjomba wangu, nitamuweza. Naamini nitarudi bungeni.”

Kuna taarifa kwamba wanafunzi wa darasa la saba waliochaguliwa kwenda shule za mbali walikuwa wameahidiwa shuleni kwa Masilingi lakini hadi Jumatatu shule ilikuwa haijakamilika kwani hata wizara haijakagua madarasa mawili yaliyokamilika.

Ubunge wa Muleba Kusini waweza kuwa mgumu kwa kila mgombea, bali jimbo likigawanywa na Tibaijuka akabaki Muleba Kusini, Alfred Tibaigana anaweza kumpa Masilingi wakati mgumu.

Tibaigana ni Kamishena wa Polisi mstaafu. Ni miongoni mwa polisi wachache wasomi akiwa na digrii ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Kwa hiyo Masilingi na Tibaigana wanatemnbeza digrii za sheria kutoka chuo kilekile wakati Tibaijuka ni mchumi. Hata hivyo maneno ya kusutana tayari yameanza.

Kuhusu iwapo anatarajia kugombea, Tibaigana anasema, “Ninagombea. Chama kinafahamu. Niliishaeleza nia yangu.”

Kuhusu uwezo wake kumshinda Masilingi kama kutakuwa na jimbo jipya, Tibaigana amesema, “Tutagombea sote tukiwa wapya. Nguvu zangu ziko kwa wananchi. Wanajua. Nimepita. Nguvu yangu ni wao.”

Naye Sebastian Rwetelana, Diwani Kata ya Nshamba anadaiwa kumwandikia Mkurugenzi Mtendaji, Muleba akilalamikia kilichoitwa “tabia” ya Mbunge Masilingi.

Katibu huyo anasema, katika andishi lake la tarehe 8 Januari 2010, kuwa Masilingi anatukana viongozi na kwamba CCM Nshamba wanadharau Jumuia za Vijana na Wazee na wanatumia ile ya Wanawake kumchagizia Masilingi.

Wakati Masilingi anakabwa koo hata na viongozi wa chama chake; na Tibaijuka ananyemelewa na “watafutaji,” Tibaigana aweza kupata upenyo. Utakuwa msuguano wa aina yake.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: