Mafanikio ya Kikwete hayajaonekana


David Kafulila's picture

Na David Kafulila - Imechapwa 04 August 2009

Printer-friendly version

NAJADILI makala ya Salva Rweyemamu iliyochapishwa katika MwanaHALISI toleo la 16-21 Julai mwaka huu na kupewa kichwa cha "Lipumba: Nani kashindwa kazi?"

Nimesukumwa na hoja aliyoitoa Salva kwamba ni Rais Jakaya Kikwete pekee aliyefanikiwa kuleta maendeleo ukilinganisha na marais wote waliotangulia baki Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Ukweli ninaouona, unashawishi niamini ni rais Kikwete anayeweza kuwa amevunja rekodi kwa kuwa kiongozi aliyeongoza serikali iliyoshindwa kuliko watangulizi wake. Mifano ipo.

Kwamba, kabla ya Kikwete kuingia madarakani mwaka 2005, idadi ya watu masikini nchini – wale wanaoishi kwa kipato cha chini ya Dola moja (Sh. 1,200) kwa siku, walikuwa 11 milioni.

Pamoja na chama chake, waliahidi kupunguza kiwango cha umasikini hadi kufikia asilimia 50. Kwa maneno mengine, rais Kikwete aliahidi kupunguza idadi ya masikini hadi kufikia 5.5 milioni.

Lakini taarifa ya mwaka 2008 ya Umasikini na Maendeleo ya Binadamu Tanzania (Poverty and Human Development Report), inasema idadi ya masikini imeongezeka kwa watu 1.7 milioni hivyo kufikia masikini 12.7 milioni.

Je, kwa takwimu hizi zilizotolewa na serikali yenyewe, Salva haoni kwamba CCM na Kikwete wameshindwa kutimiza kile walichoahidi?

Taarifa za serikali zinaonesha hadi mwaka 2005, kati ya wanawake 100,000 waliojifungua, 520 walipoteza maisha wakati wa kujifungua. Leo mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mwingine, taarifa ya hali ya uchumi inaonesha idadi ya vifo hivyo imeongezeka hadi kufikia 527.

Je, kwa takwimu hizi, Salva haoni kwamba CCM na Kikwete wameshindwa kutimiza walichoahidi?

Salva anamsifu Kikwete kwa kuimarisha elimu nchini na kusema ndiye rais aliyehakikisha kila Kata inakuwa na shule ya sekondari. Sawa.

Lakini sote nani asiyefahamu kuwa shule hizi hazikulenga kuwapa watoto wetu elimu bora. Bila miundombinu, bila walimu, bila vitabu, bila maabara; hizi si shule au ni vijiwe vya vijana kukulia na kuvutia bangi?

Mwalimu Nyerere aliwahi kusema, "Tunapoongelea kupanua elimu ya sekondari, tunaharakisha sana kusema watu watachangia ujenzi kwa juhudi zao. Lakini majengo hayana umuhimu wa kwanza…vitu muhimu katika elimu ni walimu, vitabu, na kwa sayansi ni maabara."

Ndiyo maana pamoja na serikali kuhakikisha kuwa kila mwenye umri wa kwenda shule anapelekwa kuanza shule, bado kiwango cha wananchi wasiojua kusoma na kuandika kinazidi kuongezeka.

Wakati wa utawala wa Mwalimu Nyerere – mwaka 1974 – Watanzania wasiojua kusoma na kuandika walikuwa asilimia 10 tu ya idadi ya watu wote nchini.

Miaka 35 baadaye leo, Profesa Jumanne Maghembe, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, anasema, "kiwango cha wasiojua kusoma na kuandika kimefikia asilimia 30." Sasa Salva haoni hakuna sababu ya majigambo kuhusu eneo hili?

Kwa uzoefu mdogo nilionao, naona ujasiri wa kusema CCM haijashindwa wanao watu wachache mno Tanzania. Watu wa jamii ya Yusuf Makamba, katibu mkuu wa chama hicho.

Mtu makini hahitaji elimu ya chuo kikuu kujua kwamba CCM imeyumbisha na inakwamisha maendeleo ya elimu nchini. Salva anajua fika kuwa hadi kufikia miaka ya 1990 vijana waliofanikiwa kupata nafasi ya kusoma sekondari za serikali walionekana wamefanikiwa kweli!

Hii ni kwa sababu ubora wa elimu katika sekondari za serikali, ulikuwa juu. Leo shule za sekondari za serikali ni maalum kwa watoto wa masikini. Ndio shule hizi za kata; vijiwe vya kukulia na kuvutia bangi.

Kwamba, pamoja na serikali kusema bajeti ya 2009/2010 ni bajeti ya "Kilimo Kwanza," serikali imekataa kupunguza ushuru wa mazao ya kilimo kutoka asilimia 5 mpaka asilimia 3 katika bajeti ya mwaka huu.

Badala yake, serikali inasema hilo litatekelezwa mwaka ujao wa bajeti. Hoja inayotumiwa ni kwamba "Tukitoa msamaha huo kwa wakulima, halmashauri zitapungukiwa fedha za kujiendesha."

Je, kama serikali imetoa mabilioni ya shilingi kwa ajili ya kuokoa makampuni yaliyofanya biashara ya pamba kupitia mfuko wa kuokoa uchumi, kwanini imeshindwa kuelekeza kiasi cha fedha kati ya hizo kwa halmashauri kufidia punguzo hilo?

Ni mambo ya namna hii yanayonipa shida kuamini kama kweli Salva niliyemjua miaka iliyopita ndiye huyu aliyeko Ikulu. Sitaki kuamini kuwa Salva ameporomoka kiuwezo kiasi hiki muda mfupi tu tangu apate kazi Ikulu.

Jamani kushindwa kwa Kikwete na chama chake hakuhitaji sana taarifa za uchumi wala utafiti mpana. Mtanzania hahitaji kuambiwa na serikali kama ahadi ya "Maisha bora kwa kila Mtanzania" imetekelezeka au imeshindwa.

Chukua mifano rahisi. Wakati rais Kikwete anaingia madarakani, kilo moja ya sukari ilikuwa ikiuzwa kwa Sh. 600. Hivi sasa inauzwa hadi Sh. 1,500.

Mwaka 2005 mfuko mmoja wa saruji ulikuwa unauzwa kwa Sh. 11,000. Sasa ni Sh. 21,000. Doti moja ya khanga kutoka India, inauzwa Sh. 3,500 kutoka Sh. 2,000 mwaka 2005.

Je, Salva hazifahamu takwimu hizi rahisi ambazo hata mkulima asiye na elimu anaweza kuzichambua?

Hoja nyingine ya Salva ni anaposema, "Ni ukweli usiopingika kuwa miongoni mwa viongozi wote wa vyama vya upinzani, pengine ni Lipumba ndiye ana sifa angalau zinazokaribia zile za mtu anayeweza kufikiriwa kuwa kiongozi wa kitaifa."

Hii ni kauli ya kutusi mtu. Ni dharau na kebehi kwa Watanzania. Ndani ya upinzani wapo viongozi wazuri, wenye kufikiri vema, walio wazalendo kwelikweli kwa nchi yao kuliko walivyo wa CCM.

Salva alipaswa kujiuliza: Hivi Kikwete amelifanyia nini taifa hili hadi akapimwa na mtu kama Dk. Willibrod Slaa?

Kwa hakika, vigezo vyote ambavyo Salva amevitumia kutaka kuaminisha umma kuwa Kikwete na CCM wako kwenye mstari sahihi, vimeshindwa hata kabla havijaanza kutumika.

Hata hoja kwamba Kikwete ana dhamira ya kutanzua mgogoro wa kisiasa Zanzibar, imeshindwa na kinachoonekana ni kile kiitwacho na Profesa Lipumba na CUF, "usanii mtupu."

Tangu wakati wa utawala wa Benjamin Mkapa mpaka sasa, watawala wamekuwa wakiimba "tunashughulikia, tunashughulikia" basi.

Uko wapi ushindi wa Kikwete kwa eneo hili? Tena kitu kibaya hapa ni kwamba yeye mwenyewe aliahidi 30 Desemba 2005 alipokuwa anazindua Bunge kuwa atahakikisha alichoita "mpasuko wa Zanzibar" unapatiwa ufumbuzi wa kudumu. Uko wapi ufumbuzi huu?

Sasa kwa yote hayo, ni wapi Salva anapata jeuri ya kumtofoa macho Profesa Lipumba kuwa eti ndiye alishindwa? Bado Watanzania wanasubiri kuona mafanikio ya rais Kikwete angalau yale ya kuwathibitishia "maisha bora kwa kila Mtanzania."

(Mjadala unaendelea)

David Kafulila ni Afisa Habari wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) anayepatikana kwa Simu Na: 0716 426220.
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: