Mafia wastukia mradi wa mazingira


Editha Eustace's picture

Na Editha Eustace - Imechapwa 30 June 2009

Printer-friendly version

MRADI mkubwa kuliko yote inayotunza maeneo ya Bahari ya Hindi katika kisiwa cha Mafia (Mafia Island Marine Park - MIMP), sasa unaonekana kuwa kero kwa wakazi wa kisiwa hicho.

Tayari wananchi wameanza kuzuiwa kuvua; au wanaambiwa wavue wapi; wavue lini na watumie vifaa gani kuvua huku wakiambiwa kuwa ni mpango wa kuhifadhi mazingira kwa uvuvi endelevu.

Mwenyekiti wa serikali ya Kijiji cha Jibondo, Faki Alli Hassan anaamini kuwa huu ndio mwanzo wa kuwazuia kuvua kwenye maeneo ya bahari ambayo toka enzi za mababu zao yalikuwa tegemeo lao kwa kitoweo na mapato.

Anasema ni uzushi mtupu kudai kuwa mamlaka zinalenga kuhifadhi mazingira na mazalia ya samaki ili kuongeza kiasi cha samaki baharini na kuwezesha uvuvi endelevu kwa faida ya jamii hiyo.

“Wao ni wataalamu wa uvuvi kwa vitabu na sisi ni wataalamu wa uvuvi kwa kuishi na kutumia mazingira ya bahari tokea kuzaliwa kwetu… wanayojaribu kulaghai tunayang'amua yote,” anasisitiza.

“Pepo za Kusi na Kasi ndizo pekee zilizowekwa na Mungu kwa ajili ya kudhibiti ongezeko la samaki baharini. Zinapovuma za kusi, sisi huhamia Kasi, vilevile zivumapo za Kasi, huhamia Kusi kwa kipindi cha miezi mitatu mitatu,” anasema Hassan.

Uvuvi ni njia kuu ya kupata kitoweo na mapato mengine kisiwani Mafia. Kisiwa chenye ukubwa wa kilometa za mraba 875 kina wakazi wapatao
42,024. Hii ni kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2002.

Visiwa vinavyounda Mafia ni pamoja na Jibondo, Juani, Chole na Bwejuu ambavyo ni makazi ya watu; na Nyorolo, Mbarakuti na Shungimbili ambavyo havitumiki kwa ajili ya makazi ya watu.

Uvuvi wa samaki, mazao mengine ya baharini na uundaji vyombo vya baharini – mashua, boti, jahazi na vyombo vingine vya aina hiyo, ndizo kazi kuu kisiwani. Nazi ni zao kuu lenye soko thabiti jijini Dar es Salaam.

Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, kwa kushirikiana na mashirika ya kiserikali na yasiyokuwa ya kiserikali imeanzisha miradi mbalimbali visiwani humo kwa lengo la kuhifadhi fukwe na mazingira ya baharini.

Kwa mujibu wa serikali, lengo kuu la hatua hizo ni kuweka mazalia salama ya samaki, ili kuongeza idadi ya samaki. Hivi sasa tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwepo kasi ya kupungua kwa samaki.

Kati ya kilometa za mraba 875 za Mafia, kilomita za mraba 822 zipo chini ya hifadhi ya mradi huo wa hifadhi.

Umuhimu wa MIMP unaelezwa kutoishia kwenye hifadhi na kutunza mazingira visiwani humo, bali unayo manufaa kwa wakazi takribani 10,000 wanaoishi ndani ya mipaka ya eneo hilo lililo chini ya hifadhi.

Mimea asilia pia hutumiwa na jamii hiyo katika shughuli mbalimbali za kila siku; mathalani ujenzi wa nyumba. Asilimia kubwa ya nyumba visiwani humo huezekwa kwa nyasi na miti ambapo mikoko ndiyo aina ya miti inayotumika.

Mradi kupitia taarifa zake ambazo zimekuwa zikitolewa mara kwa mara kwa njia mbalimbali ikiwemo ya mtandao wa intaneti, unaeleza kuwa utekelezaji wa jukumu lake la kuhifadhi mazingira hayo hautekelezwi kwa urahisi.

Hapa panahitajika umakini na busara ili kuhakikisha kunakuwepo ulinganifu kati ya kuhifadhi mazingira na kuzingatiwa kwa mtindo wa maisha wa wakazi hao.

Aidha, lengo la msingi katika shughuli zote za mradi ni kuwezesha uvuvi endelevu kwa faida ya jamii husika na taifa kwa ujumla.

Mfuko wa Kimataifa wa Kuhifadhi Mazingira na Viumbe asilia, (WWF) na Shirika la Misaada la Norway (NORAD) ni mashirika yanayotajwa kuufadhili mradi wa MIMP katika kuujengea uwezo wa kuwasaidia wavuvi kutekeleza shughuli zao.

Kwa mujibu wa kanuni za uvuvi endelevu, wavuvi wanatakiwa kutumia nyavu zenye matundu kati ya inchi 1.5 na 2. Vilevile inashauriwa wavue kwenye maji ya kina kirefu ambacho ni kuanzia mita 20.

Bali hayo ni maelezo ya mamlaka zinazotekeleza mradi wa kuhifadhi na kutunza mazingira. Wananchi wanasema miradi hiyo haina manufaa makubwa kwao.

Desemba mwaka jana, wakazi 27 walikamatwa na kupigwa na askari kwa tuhuma za kumiliki nyavu za matundu madogo na kuvua katika maeneo yasiyohusika; hivyo kufanikisha uvuvi haramu.

Imeelezwa kuwa hata wanawake, tena wajawazito na watoto wadogo, walipigwa sana.

Simulizi zinasema walioendesha kipigo walikuwa askari wakati wananchi hawakuwa na silaha za aina yoyote wala nguvu za kujitetea. Jambo hilo limefanya jamii ya visiwani humo kugubikwa na hofu na chuki dhidi ya karibu mamlaka zote zinazoshiriki mradi huu.

Katika hali ya kawaida, hata kama ilikuwa lazima kutumia askari, ilibidi kwanza ufanywe upekuzi wa kusaka zana hizo haramu, kuzingatia taratibu, na endapo ingethibitika kuwepo watu wanaozimiliki, ndipo zichukuliwe hatua za kisheria.

Mwenyekiti wa serikali ya Kijiji cha Jibondo, Faki Alli Hassan anaamini kuwa huu ndio mwanzo wa kuwazuia kuvua kwenye maeneo ya bahari ambayo toka enzi za mababu zao yalikuwa tegemeo lao kwa kitoweo na mapato.

Anasema ni uzushi mtupu kudai kuwa mamlaka zinalenga kuhifadhi mazingira na mazalia ya samaki ili kuongeza kiasi cha samaki baharini na kuwezesha uvuvi endelevu kwa faida ya jamii hiyo.

“Wao ni wataalamu wa uvuvi kwa vitabu na sisi ni wataalamu wa uvuvi kwa kuishi na kutumia mazingira ya bahari tokea kuzaliwa kwetu… wanayojaribu kulaghai tunayang'amua yote,” anasisitiza

“Pepo za Kusi na Kasi ndizo pekee zilizowekwa na Mungu kwa ajili ya kudhibiti ongezeko la samaki baharini. Zinapovuma za kusi, sisi huhamia Kasi, vilevile zivumapo za Kasi, huhamia Kusi kwa kipindi cha miezi mitatu mitatu,” anasema Hassan.

Anasema kama samaki wangekuwa wanaisha, basi kizazi cha sasa kisingepata samaki hata mmoja. Lakini kwa kuwa wanapata, tena wa kutosha ni dhahiri kwamba wapo na wataendelea kuwepo.

Hoja hapa ni kwamba karibiu miradi yote ya kuhifadhi mazingira na viumbe hai wa baharini, ilianza utekelezaji bila kutekeleza mfumo shirikishi au kama ulitekelezwa basi ni kwa kiwango kidogo sana.

Mazungumzo na jamii ya wakazi wa Mafia yanathibitisha kutoshirikisha jamii katika kuboresha mazingira ya uvuvi endelevu. Hapa, matumizi ya mabavu yalikuwa uvunjaji wa haki za binadamu.

Wakati wa kutekeleza miradi kwa kutumia vipeperushi na maelezo kupitia mitandao na majukwaani huku uhalisia ukibainisha kinyume umepita.

Wananchi wanastahili kuelimishwa vya kutosha ili kila mmoja awe mwalimu na mlinzi wa mwenzie.

0
No votes yet