Mafisadi sasa watumia al Shabaab


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 02 November 2011

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, wiki iliyopita, lilifanikiwa kuzima maandamano yaliyopangwa na Mtandao wa Wanaharakati kwa lengo la kupinga Serikali kulipa kampuni ya kufua umeme ya Dowans yapata Sh. 10 bilioni za fidia.

Aliyekabidhiwa jukumu la kuzima maandamano hayo yaliyopangwa kufanyika Jumamosi, alikuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova.

Katika mkutano na waandishi wa habari, Kamishna Kova alisema wamepata taarifa, nadhani za kiintelijensia, kuwa kikundi cha kigaidi cha al Shabab kinapanga kushambulia mikusanyiko ya watu jijini Dar es Salaam.

Kamishna Kova hakutaja siku, mahali wala sababu za al Shabaab kushambulia. Aliwaacha watu wajiulize maswali yasiyo majibu.

Ninavyofahamu, magaidi hawashambulii tu mradi kuua watu, huwa wanapeleka ujumbe kwa watu maalum kwamba wakiingiliwa katika mambo yao, watatumia ‘lugha’ inayojulikana madhara yake – kuua.

Al Qaeda waliposhambulia Tanzania na Kenya mwaka 1998 walilenga balozi za Marekani japo waliokufa ni Watanzania na Wakenya. Marekani wanajua kwa nini wanalengwa na al Qaeda na wanajua sababu za wao kupigwa 11 Septemba 2001.

Kwa hiyo, kama al Shabaab watashambulia mikusanyiko ya watu wanaopinga Dowans kulipwa isivyostahili, ina maana kikundi hicho kina uhusiano na Dowans hivyo kutaka serikali ilipe fidia hiyo.

Maana kama sababu ingekuwa kupinga msimamo wa Tanzania kuunga mkono Kenya kusaka wapiganaji wa kikundi hicho nchini Somalia, walengwa wa mashambulizi ya kigaidi wasingekuwa waandamanaji wa Dar es Salaam dhidi ya malipo kwa Dowans pekee.

Kamishna Kova alipodai al Shabaab hawana nongwa na mkusanyiko wa mpira wa miguu kwa washabiki wa Simba na Yanga ila wanaoandamana kupinga Dowans, alikuwa anamaanisha kuwepo uhusiano wa kundi hilo na Dowans.

Je, al Shabab ndio wanamiliki Dowans au mafisadi wameamua kutumia ugaidi kushinikiza malipo? Kwa hiyo, Dowans limegeuka dude linalotishia usalama wa Watanzania.

Sasa ni dhahiri katika kampeni za kuhujumu uchumi wa nchi, Dowans inatumia gia ya ugaidi na Polisi wamekubali kutumiwa.

Kama chombo cha serikali kimekubali kutumika kwa maslahi ya kifisadi, basi Dowans wako ndani ya serikali na ni watu wenye mamlaka makubwa. Hiki ni kitisho kipya kwa raia.

Wiki mbili zilizopita, al Shabaab, kikundi ‘kinachotawala’ Somalia, kilifanya mashambulizi mawili katika klabu za usiku jijini Nairobi. Watu 14 walijeruhiwa. Mashambulizi hayo yalifuatia hatua ya serikali ya Kenya kuingia Somalia kupambana nao.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Orwa Ojode alisema wanapanga kufanya operesheni kubwa – ‘mama ya operesheni zote’ Nairobi ili kusambaratisha magaidi wote wa al Shabaab.

Akasema “al-Shabaab ni kama mnyama mkubwa ambaye mkia wake uko Somalia. Bado tunaukabili mkia ulioko Somalia wakati kichwa chake kiko hapa Kenya”. Ojode alisema katika mapambano hayo, watakilenga kitongoji cha Eastleigh jijini Nairobi kinachokaliwa na wakazi wenye asili ya Somalia.

Kamishna Kova akaona abebe ‘bomu’ la hofu ya jiji la Nairobi na kulibwaga Dar kwa lengo la kuzuia maandamano ya kupinga serikali kuilipa Dowans.

Intelijensia ya Kamishna Kova inasema al Shabaab wala hawakuwa na nongwa na washabiki wa soka hata kama ni wengi kuliko wale ambao wangeshiriki maandamano. Hata kama al Shabaab wangekuwa na nongwa hiyo, yeye aliahidi kujaza polisi Uwanja wa Taifa ili mabomu ya al Shabaab yasidhuru maelfu ya wanazi wa soka.

Mkuu huyu wa Polisi Dar es Salaam aliwataka watu wafike kwa wingi Uwanja wa Taifa kushangilia timu zao kwa sababu “kutakuwa na ulinzi wa uhakika.”

Alisema, "Al Shabaab wanapenda kwenye mikusanyiko ya wanaharakati." Kauli hii kwamba al Shabaab wanapenda kushambulia penye mikusanyiko ya wanaharakati, kwa mazingira ya Tanzania, wenye chuki na wanaharakati ni mafisadi.

Alisema Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, wamepanga mkakati madhubuti wa kuhakikisha mechi hiyo inafanyika kwa amani na utulivu, lakini si maandamano.

Wapi Kamanda Kova ameona magaidi wakishambulia eneo la wazi bila kulenga watu maalum? Chuki ya al Shabaab kwa wanaharakati ni nini?

Wanaharakati hao wangeamua kuandamana kwa nguvu, wasingepatikana polisi wengi na magari mengi ya maji ya kuwasha kwa ajili ya kuvunja maandamano hayo? Kamanda Kova ametumiwa na mafisadi ndani ya serikali kutisha ili wasiingiliwe mambo yao.

Ripoti na rekodi zilizopo zinaonesha kuwa matukio mengi ya kigaidi hufanyika kwenye masoko, viwanja vya michezo, sehemu za starehe, vizuizi vya polisi, kambi za jeshi, njia za treni, misafaya ya mabasi, mikutano ya wanasiasa, hoteli na majengo marefu ya kifahari kutoa ujumbe maalum.

Marekani wanajua ujumbe waliopewa kwa shambulio walilolipa jina maarufu la 9/11 (Nine Eleven).

Viwanja vya michezo hulengwa sana. Nadhani, mwaka 1972, Kamanda Kova ama alikuwa shuleni au chuoni, pale kikundi cha magaidi kilichoitwa "Black September" cha Kipalestina kiliposhambulia wanamichezo wa Israel kwenye uwanja wa Olimpiki wa Munich, nchini Ujerumani.

Ujumbe wa Black September ulikuwa kutaka watu 200 waliokamatwa Israel kwa misingi ya kisiasa waachiwe huru.

Shambulio jingine kubwa lilifanyika wakati wa Michezo ya Olimpiki mwaka 1996. Bomu lililipuliwa kwenye ukumbi wa burudani wa Centennial Olympic Park wakati mamia ya wanamichezo wakiwa wanastarehe.

Wapenzi wa michezo watakuwa wanakumbuka tukio la mwaka 2002 saa chache kabla ya pambano la soka la nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Real Madrid na Barcelona. Watu 17 walijeruhiwa.

Mwaka 2002 ulikuwa mbaya nchini Indonesia pale watu 202 walipouawa na wengine 240 kujeruhiwa baada ya klabu za usiku eneo la ufukwe wa kitalii la Bali kushambuliwa na magaidi usiku.

Baada ya Saddam Hussein kuondolewa madarakani nchini Irak mwaka 2003, nchi haikukalika. Irak ilianza kukumbwa na mashambulizi ya kigaidi kwenye vizuizi vya polisi na masoko.

Michezo ililengwa. Moja ya mashambulizi makubwa ya kigaidi mwaka 2006 yalifanywa mchana kweupe wakati wa kongamano la michezo jijini Baghdad.

Mwaka 2009 India ikihofia usalama wake, ilijitoa katika mashindano ya kriketi yaliyopangwa kufanyika nchini Pakistan. Magaidi wakaamua kumaliza hasira kwa kushambulia basi la timu ya kriketi ya Sri Lanka. Watu saba waliuawa na wanamichezo sita walijeruhiwa.

Januari 2010 timu ya Togo ilishambuliwa na magaidi ilipokuwa inakwenda kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zilizopangwa kufanyika nchini Angola. Hali hiyo ilizusha hofu kwamba huenda hata fainali za Kombe la Dunia zilizopangwa kufanyika miezi mitano baadaye nchini Afrika Kusini zingevurugwa na magaidi.

Kwa mifano hiyo, al Shabaab wasingeacha washabiki wa mpira kama alivyodai Kamanda Kova.

Aidha, magaidi wakishambulia eneo la wazi huwa wamemlenga kiongozi maalum kama alivyouawa mwanamama machachari Benazir Bhuto wa Pakistan na hata aliyekuwa Waziri Mkuu wa India, Rajiv Gandhi.

0789 383 979, jmwangul@yahoo.com
0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)