Mafisadi wakwama


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 03 February 2010

Printer-friendly version
Jengo la Bunge Dodoma

TUNDU pekee la watuhumiwa wa ufisadi kujitakasa limezibwa, MwanaHALISI ina taarifa. Bunge, kwa ujasiri wa kipekee, limekataa kutumiwa na serikali kusafisha watuhumiwa wa kashfa ya Richmond.

Kwa hatua hiyo, ambayo imesababishwa na serikali kudai kuwa bunge halina uwezo wa kuishinikiza, tayari umeibuka mgogoro juu wajibu na madaraka ya bunge kuhusiana na serikali.

Sasa ni suala la nani zaidi au “jino kwa jino,” kati ya bunge na serikali; mazingira ambayo yanaziba kabisa uwezekano wa watuhumiwa kujisafisha.

Hayo yamedhihirika kutokana na ripoti ya serikali iliyowasilishwa katika Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ambayo bunge limekataa na kuagiza ifanyiwe marekebisho.

Taarifa ya serikali yenye kurasa 30 imeanza kwa kujikanganya juu ya mamlaka na wajibu wa bunge katika uhusiano wake na serikali.

Huku ikijiandaa kujenga hoja za kuwasafisha watuhumiwa wa kashfa ya Richmond, serikali ilisema katika utangulizi kuwa kazi ya bunge ni “kuishauri na kuisimamia tu.”

Lakini pamoja na kutambua “usimamizi,” serikali inaishia kutaja wajibu wa bunge kuwa ni kuuliza maswali kwa waziri, kujadili, kuidhinisha, kuridhia mikataba na kutunga sheria.

Kauli hiyo ya serikali ndiyo ilizua utata na mabishano katika hatua ya awali ya kujadili taarifa na kusabisha bunge liagize kufanyika kwa marekebisho kabla kamati haijaijadili.

Msimamo wa serikali, kuainisha majukumu ya bunge kama inavyotaka, ulilenga kudhoofisha bunge katika msimamo wake wa kutaka mapendekezo yake yote 23 juu ya kashfa ya Richmond yatekelezwe.

Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini na baadaye Kamati ya Uongozi ya Bunge la Jamhuri iliyokutana 25 Januari 2010, iliishauri serikali kuondoa taarifa yake, kuirekebisha na kuiwasilisha upya.

Ingawa mjadala uliishia kwenye utangulizi, ndani ya ripoti ambayo MwanaHALISI imeona, taarifa ya serikali “inasafisha” karibu watuhumiwa wote pamoja na  Edward Lowassa aliyekuwa Waziri Mkuu.

Wiki iliyopita gazeti hili liliripoti Waziri Mkuu Mizengo Pinda akiagizwa kutopeleka ripoti ya serikali bungeni kwa hofu kwamba ingeumbua serikali.

 Jeuri ya serikali inatokana na kunukuu kwa ufupi tu ibara 63(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 juu ya kushauri na kuacha hatua nyingine ya kusimamia serikali.

Ndipo serikali inahitimisha utangulizi wake kwa kusema, pamoja na mambo mengine, “… maazimio ya Bunge ni ushauri kwa serikali na siyo maagizo. Serikali ilikubali ushauri huo na kuutekeleza kwa kuzingatia misingi hiyo ya Katiba.”

Hapa ndio mwanzo wa mnyukano wa “jino kwa jino.” Bunge lina hoja kwamba ibara ya 8 (1) (a) inasema hivi, “Wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii….(b) Serikali itawajibika kwa wananchi.”

Bunge lina hoja nyingine kuwa ibara ya 63(2) ya Katiba inaeleza, “Bunge ndilo litakuwa chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri serikali.”

Lakini pia bunge lina hoja kuwa ibara ya 46A (1) inasema, “Bunge linaweza kupitisha azimio la kumuondoa Rais madarakani endapo itatolewa hoja ya kumshitaki Rais na ikapitishwa kwa mujibu wa masharti ya ibara hii.”

Kwa mujibu wa duru za gazeti hili bungeni, ibara hizo za Katiba zinamaanisha kwamba Bunge lina madaraka makubwa kuliko kuishauri serikali tu kwa vile lenyewe linawakilisha wananchi ambao ndiyo wenye serikali.

“Bunge, kupitia Katiba hiyohiyo limepewa madaraka ya kumwajibisha Waziri Mkuu na Makamu wa Rais. Sasa katika msingi huo, serikali inawezaje kusema kazi ya Bunge ni kushauri tu?” amehoji mbunge mmoja aliyezungumza na gazeti hili.

Wabunge waliohojiwa na MwanaHALISI wamesema serikali inatafsiri katiba itakavyo ili kukwepa utekelezaji wa maazimio ya Bunge.

Novemba mwaka 2007, Bunge liliunda Kamati Teule iliyokuwa na lengo la kuchunguza mchakato mzima uliotoa zabuni ya kufua umeme wa dharura kwa kampuni ya kitapeli ya Richmond Development Company LLC.

Ripoti hiyo iliwasilishwa bungeni Februari 2008 na mwenyekiti wa Kamati, mbunge wa Kyela (CCM), Dk. Harrison Mwakyembe, uchunguzi wake ulikuwa chanzo cha kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.

Wengine waliojiuzulu ni Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi waliokuwa mawaziri wa nishati kwa nyakati tofauti.

Lowassa alituhumiwa kufanya upendeleo kwa kampuni ya Richmond ambayo tayari ilithibitika kwamba haikuwa na sifa, uwezo wala hadhi ya kupewa kazi iliyoomba.

Baada ya ripoti hiyo kupitishwa, Bunge lililitoa jumla ya maazimio 23 kuhusiana na mkataba kati ya Tanesco, kwa niaba ya serikali na kampuni ya Richmond.

Miongoni mwa maazimio hayo lilikuwa ni kuchukuliwa hatua za kisheria wahusika wote katika mchakato huo.

Lakini katika taarifa ya utekelezaji wa maazimio hayo iliyotakiwa kuwasilishwa bungeni, serikali imesema wazi kwamba watumishi wote wa serikali waliotajwa hawakuwa na makosa.

“Serikali imeridhika na maamuzi ya mamlaka za nidhamu za kuwafutia mashitaka watumishi wa serikali kwa vile hawakuwa na wajibu wa kutoa maamuzi au ushauri kwa serikali,” inasema taarifa hiyo ya serikali.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)