Mafisadi wamtishia Kikwete


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 25 March 2009

Printer-friendly version
Rais Jakaya Kikwete

WATUHUMIWA wa ufisadi, wanaolalamika kuwa Rais Jakaya Kikwete amewatelekeza, wanapanga kumhusisha katika baadhi ya tuhuma zinazowakabili ili kumshinikiza kutimiza matakwa yao, MwanaHALISI limeelezwa.

Taarifa za kuaminika kutoka kwa baadhi ya viongozi serikalini na watuhumiwa, zinasema tayari mipango imesukwa ya kumchomeka Kikwete katika sakata la mitambo ya kufua umeme wa dharula inayodaiwa kumilikiwa na kampuni ya Dowans Holding Tanzania Limited.

Aidha, watuhumiwa wa ufisadi wameapa kumhusisha Rais Kikwete katika sakata la ukwapuaji wa Sh. 40 bilioni, uliofanywa na kampuni ya Kagoda Agriculture Limited, kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) mwaka 2005.

Njia mbili zinatumika kufanikisha “mradi” huu. Kwanza, viongozi wa watuhumiwa wanadaiwa kuchochea watendaji serikalini – wakiwemo wakuu wa mikoa na wilaya – kutenda ovyo au kutotenda kazi ili ionekane serikali imeshindwa kutawala.

Pili, wanadaiwa kuchochea madai, lawama na malumbano ndani ya chama, yenye lengo la kupandikiza chuki na uhasama miongoni mwa uongozi, wanachana na wananchi ili ionekane kuwa uongozi wa chama, ambao pia uko chini ya Rais Kikwete unalegalega.

“Sikiliza ndugu yangu; mengine rais atakuwa ameyagundua. Angalia ziara zake mikoani; ni kukemea hapa na pale. Anakuta wakuu wa wilaya na mikoa hawatendi kazi zao kana kwamba wanamsubiri yeye,” kimeeleza chanzo cha habari.

Mfano mwingine uliotolewa ni kwamba miaka miwili iliyopita, watendaji serikalini walipewa elimu elekezi; jinsi ya kutekeleza kazi zao.

Lakini hivi majuzi rais ameonekana akirudia kutembelea wizara na kushiriki katika utoaji mijadala na mahojiano hadi kufikia maazimio juu ya jinsi ya kutenda kazi, kimeeleza chanzo cha habari hizi.

“Yote haya yanalenga kuonyesha kuwa bila wao – watuhumiwa wa ufisadi na wengine ambao wamepoteza nafasi zao serikalini – basi serikali haiwezi kutenda,” ameeleza kiongozi mmoja mwandamizi serikalini.

Kiongozi mmoja wa ngazi ya juu katika Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye tayari aliishaondolewa katika nafasi yake, anadaiwa kuendelea kushikilia madaraka akidai “hakuna mwingine mwenye uwezo kama mimi.”

“Hakuna kitu kilichomuuma sana kiongozi huyu (jina tulalo) kama kuondolewa kwenye nafasi hiyo ya kifedha. Yeye na rafiki yake aliyeng’olewa serikalini (jina tunalo) walikuwa wakijigamba kuwa pekee, wenye uwezo wa kumshawishi na hata kumwamuru rais,” kimeeleza chanzo cha habari.

Habari kutoka Dettroite, Marekani zinasema mpango wa kumhusisha Kikwete katika tuhuma za ufisadi, ikiwemo kushiriki kwake katika mradi wa Dowans sasa unaendeshwa kwa kasi.

Shirika moja la habari la Marekani, KLHN limenukuu vyanzo vya habari vikisema, mara baada ya mwandishi M.M. Mwanakijiji, kufanya mahojiano na anayedaiwa kuwa mmiliki wa Dowans, Bregedia Jenerali Sulaiman Mohammed Yahya Al Adawi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), wanaodaiwa kuibeba Dowans wameanza kutafuta jinsi ya kumhusisha Kikwete.

Mbunge mmoja wa Kanda ya Ziwa, aliyekuwa nchini Marekani hivi karibuni, amenukuliwa akisema, “Baada ya mradi wetu wa Richmond kushindwa, Rostam aliombwa na “mkuu” – akimaanisha Rais Kikwete – kumfuata Al-Awadi kuona kama angeweza kuleta majenereta ya kufua umeme.

Mbunge huyo alimwambia mwandishi wa KLHN, “Ni Kikwete aliyeahidi mapema kuwa baada ya muda wa mkataba (wa Dowans kufua umeme) kumalizika, majenereta hayo yatanunuliwa na serikali.”

MwanaHALISI inayo mahojiano kamili kati ya mwandishi wa Marekani na mbunge huyo.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, mara baada ya mahojiano ya kwanza kati ya Mwanakijiji na Jenerali Yahya Al Adawi, ulifanyika mkutano wa faragha, tarehe 8 Machi 2009 huko Dubai, ukiwahusisha baadhi ya wanasiasa wa Tanzania akiwemo mtendaji mmoja wa serikali.

Katika mahojiano hayo ya kwanza, Al Adawi alikana kuifahamu Dowans. Lakini baada ya mkutano wa Dubai, Jenerali huyo alimwambia mwandishi kuwa anaifahamu Dowans na kwamba ndiye anaimiliki.

Makubaliano kwenye mkutano huo yalikuwa ni pamoja na kuelekeza wenye mrengo wa kuitetea Dowans kuendelea kufanya hivyo kwa “gharama yoyote ile” ikiwamo “hata kumtumbikiza Kikwete” katika sakata hili.

Habari kutoka Dubai zinasema watuhumiwa watatu wa ufisadi kutoka Dar es Salaam na ofisa mmoja wa ngazi ya juu serikalini, walihudhuria  kikao hicho ambacho pia kilihudhuriwa na Jenerali Al Adawi.

Kwenye kikao hicho iliamriwa kuwa Jenerali Al Adawi akiri kuifahamu Dowans kampuni hiyo na vilevile kumtuma mmoja wa wanasiasa hao kuhakikisha anawasiliana na Mwanakiji nchini Marekani kwa lengo la “kumuweka sawa.”

Gazeti la Tanzania Daima Jumapili, toleo la 15 Machi 2009 lilimnukuu Al Adawi akisema, aliombwa na Rostam “kuokoa jahazi” baada ya Richmond kushindwa katika kile kilichoitwa “harakati za mwanasiasa huyo” kuvutia wawekezaji.

Katika mahojiano yake na KLHN, Al Adawi anakiri kufahamiana na Rais Kikwete. Anasema ni Rostam aliyemueleza kwamba rais amempa kazi ya kuleta mitambo hiyo nchini.

Taarifa zinasema watuhumiwa wa ufisadi  wanataka kutumia madai kuwa Rais Kikwete na Jenerali Al Adawi wanafahamiana kama njia ya kunyamazisha serikali, asasi za kijamii na wananchi, ili hatimaye mitambo ya Dowans iweze kununuliwa.

Katika mahojiano ya awali na mwandsishi wetu Marekani, Al Adawi alisema ana makampuni lakini hakuna hata moja kati yake ambalo linajishughulisha na nishati ya umeme.

Lakini baada 8 Machi, Al Adawi alisema ana kampuni ya Dowans inayofua umeme.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Nape Nnauye, aliwaambia waandishi wa habari juzi Jumapili kuwa malumbano yanayoendelea hivi sasa nchini juu ya kununua au kutonunua mitambo ya Dowans, ni ishara kwamba “mafisadi wamejipanga kuifanya nchi isitawalike.”

“Tunakokwenda ni kubaya ila naamini serikali iko imara na CCM tutaomba tulizungumze kwenye vikao vyetu,kwa nia njema ya kuliokoa taifa linalovurugwa na watu wachache wenye fedha,” alisema Nape.

Kupatikana kwa mabilioni ya shilingi mikononi mwa watu wengi, wakiwemo wanasiasa, wafanyabiashara na wapambe wao, kuna uwezekano wa kujenga ubabe miongoni mwa wanaopinga serikali, ameeleza mchumi mmoja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

“Tatizo ni kwamba kunakuwa na utawala wa kimafia. Kunakuwa na serikali mbili – ya wananchi na ile ya mafisadi. Kila kinachopangwa na serikali kinapingwa na walioko nje ya serikali na kunakuwa hata na hazina mbili. Hii ni hatari, alisema bila kutaka kutajwa jina gazetini.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: