Mafisadi wamtishia Kikwete


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 19 March 2008

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir
Waapa kuanika 'vimemo'
Spika Sitta asalimu amri
Rais  Jakaya Kikwete

WATUHUMIWA wa wizi wa mabilioni ya shilingi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wameapa kudhalilisha serikali pindi watakapofikishwa mahakamani.

Habari za uhakika kutoka kwa jamaa wa walionufaika na fedha hizo zinasema wenye makampuni yaliyochota Sh. 133 bilioni za umma wamejiapiza kutoa taarifa zote ambazo zitaiweka serikali pabaya.

"Viongozi wengi wa ngazi ya juu katika serikali iliyopita na ya sasa wamenufaika na fedha hizi. Kama ni kutajana, basi hata wale ambao hawajawahi kutuhumiwa wataumbuka," kimeeleza chanzo cha habari.

Iwapo serikali itaogopa kuumbuliwa, au viongozi wake wa ngazi ya juu kuogopa kuwekwa kwenye orodha ya mafisadi, basi uwezekano wa kupata fedha zote zilizoibwa utakuwa umefutika.

Aidha, Spika wa Bunge la Jamhuri, Samwel Sitta amesema suala la wizi wa fedha kutoka akaunti ya madeni ya nje (EPA) ya BoT, halitapelekwa mbele ya Mkutano wa 11 wa Bunge kama alivyokuwa ameahidi.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Sitta alisema suala la EPA sasa limo mikononi mwa Kamati ya Rais iliyokabidhiwa jukumu la kuwatafuta wahusika na kuwezesha urejeshaji wa mabilioni yaliyokwapuliwa.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, watuhumiwa wanajiandaa kukabiliana na serikali kwa kuonyesha jinsi fedha zilivyotumika na nani hasa walinufaika.

"Sikiliza bwana mdogo, kuna wenye barua zinazoelekeza fedha zichukuliwe na wapi zipelekwe. Kuna wenye vimemo vinavyoelekeza nani apewe kiasi gani na kwa kazi ipi. Hakuna atakayekubali kufa peke yake; watayasema tu," ameeleza mtoa taarifa wa MwanaHALISI.

Akizungumza kwa kujiamini, mtoa taarifa huyo alitoa mfano wa fedha za kampuni moja zilizotumika kununua nyumba ya "mtoto wa kigogo" wa serikalini.

"Nakuapia, huyu ana kimemo. Kinaelekeza hata nyumba ya kununua na mahali ilipo. Sasa kwa nini huyo asulubiwe peke yake. Watatajwa hata wale ambao serikali itajuta kwa nini iliwapeleka mahakamani," ameeleza.

Taarifa zinasema kuna wenye makampuni yaliyokwapua mabilioni ya shilingi ambao waliombwa wagharimie masomo ya watoto wa baadhi ya viongozi; tena nchi za nje.

Kuna wanaodai kuchangia shughuli za Chama Cha Mapinduzi (CCM), tena kwa mamilioni ya shilingi, na wana ushahidi wa nani aliomba, nani aliombwa, nani alipeleka, nani alipokea na jinsi zilivyotumika.

"Memo" ni vikaratasi vidogo vya ujumbe rasmi na wa haraka, badala ya barua, kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine au kundi au asasi nyingine.

Kwa sasa kuna taarifa zilizoenea jijini Dar es Salaam kwamba mmoja wa viongozi wa juu nchini, alipewa Sh. 200 milioni kwa shughuli za kisiasa katika CCM lakini kiasi hicho hakikufikishwa ofisini.

"Nakwambia kila kampuni ilichota kiasi fulani kugharimia shughuli za wakubwa au za kisiasa. Waliozipokea na vimemo vyote vipo; kwa hiyo la mgambo likilia watatajana na wameapa kutokuwa na aibu," kimeeleza chanzo cha habari.

Kwa mfano, kuna taarifa ambazo hazijathibitishwa kwamba wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu, kiongozi mmoja wa CCM alipewa Sh. 200 milioni azipeleke ofisi ya chama Mkoa wa Mwanza.

Kinachoshangaza wengi hadi sasa ni kwamba zilifikishwa Sh. 80 milioni lakini wagombea ubunge waliokuwa walengwa, waliambiwa zimeletwa Sh. 20 milioni.

"Sasa hili unaweza kulielezeaje? Kila utakayembana atamtaja mwenzake na utakuta wengine ni viongozi wa chama na serikali," kimeeleza chanzo chetu.

Angalau katika miji miwili nchini – Kigoma na Moshi- kuna vituo vya kuuza mafuta ya petroli na dizeli. Wananchi wamekuwa wakishuhudia magari ya chama na serikali yakipewa mafuta bure.

Taarifa hizi ambazo zinahitaji uchunguzi zaidi zinasema vituo hivyo vimejengwa wakati au mara tu baada ya uchaguzi mkuu na wahusika wanatoa "asante" kwa waliowawezesha.

Inadaiwa kuwa fedha za ujenzi wa vituo hivyo ni sehemu ya mabilioni yaliyokwapuliwa BoT.

"Hii ndiyo maana nasema uwezekano wa watuhumiwa kupelekwa mahakamani ni mdogo sana, au wakipelekwa kutakuwa na kazi kubwa ya kuchambua nani asalimishwe na nani atoswe," amesema.

Ni ugumu huohuo unaoikabili serikali kuhusu kumshitaki Dk. Daudi Ballali, yule aliyekuwa gavana wa BoT.

Kurejea kwake nchini au kutoka kwake mafichoni, kunaweza kuiweka serikali pabaya kwani anadaiwa kuwa na maelekezo yote kabla ya kuruhusu uchotaji wa mabilioni ya fedha hizo.

Makampuni 22 yalithibitika kuchota kifisadi Sh. 133 bilioni kutoka akaunti ya EPA katika mwaka wa fedha wa 2005/06. Inadaiwa baadhi ya fedha hizo zilitumika katika kampeni za CCM za uchaguzi mkuu.

Mwaka huu, 8 Januari, Katibu Mkuu Kiongozi (Ikulu), Philemon Luhanjo, alitangaza kuwa kiasi hicho cha fedha kiliibwa na makampuni 22 yakitumia nyaraka za kughushi.

Hii ilikuwa baada ya ukaguzi wa kitaalam wa hesabu za akaunti hiyo uliofanywa na maodita wa Ernst & Young.

Rais Jakaya Kikwete, baada ya kupokea ripoti ya maodita aliyokabidhiwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Ulotu, alitangaza kumfukuza kazi aliyekuwa Dk. Ballali na kuunda kamati ya kurejesha mabilioni yaliyoibwa.

Kamati hiyo inayoongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, inahusisha pia Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Edward Hoseah.

Hata hivyo, kuna taarifa kwamba Idara ya Usalama wa Taifa (Tanzania Intelligence Service - TIS) imejumuishwa, na kwamba magari yake yanatumiwa kwa ufuatiliaji wa wahusika.

Mwanyika amekana kuwepo kwa maofisa wa TIS ndani ya Kamati ya Rais ambao wanamiliki makampuni yaliyo kwenye orodha ya mafisadi.

"Tunajua hali ni ngumu sana kwa serikali, bali Rais Kikwete anastahili kuuma jino na kusema lije na liwalo, hata kama naye atatajwa, ili kurejesha mamlaka yake na ya wananchi ambayo yamemomonyolewa na mafisadi," anasema mhadhiri wa Chuo Kikuu ambaye ni mmoja wa mashabiki wakuu wa CCM. Aliomba kutotajwa jina..

Makampuni yanasakwa ili yarejeshe fedha zilizoibwa ni Kagoda Agriculture Limited, Malegesi Law Chambers; Money Planners & Consultants; Kiloloma and Bros Enterprises; Mibale Farm; Ndovu Soap Limited.

Mengine ni Njake Enterprises Limited; Navycut Tabacco (T) Limited; Becon International Limited; Bina Resort Limited; Changanyikeni Residential Complex Limited na Njake Hotels and Tours Limited.

Wakwapuzi wengine ni Bora Hotel and Apartment Limited; Liquidity Services Limited; V.B. & Associate Company Limited; Maltan Mining Company Limited; Venus Hotels Limited; B. V. Holding Limited; Kernel Limited, G & T International Limited, Excellent Services Limited na Clayton Marketing Limited.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: