Mafuriko yatatuzindua?


editor's picture

Na editor - Imechapwa 28 December 2011

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

GHARIKA ya mafuriko iliyotokea jijini Dar es Salaam hivi karibuni imeacha mafunzo mengi.

Kwa namna serikali ilivyotekeleza jukumu la kusaidia watu walioathirika na mafuriko hayo yaliyosababishwa na mvua za siku mbili mfululizo, inathibitisha kuwa bado viongozi wetu hawajatambua wajibu wao wakati wa majanga.

Ingawa mkoani Dar es Salaam walitangaza haraka vituo vya waathirika kukimbilia maeneo ya hifadhi kupata msaada, huduma zilichelewa mno kuwafikia.

Kwa siku mbili hakukuwa na vifaa vya kujihifadhi vituoni. Hakukuwa na huduma za chakula kama ilivyotarajiwa. Inasikitisha baadhi ya vituo, waathirika walichangishwa fedha za kununua sukari kwa ajili ya chai.

Katika kituo cha Mchikichini, wilayani Ilala, hadi Ijumaa, siku tatu baada ya mafuriko kutokea, waathirika walikuwa hawajapatiwa magodoro, ingawa wasamaria walitoa magodoro mengi kwa ajili hiyo.

Gazeti hili lilipigiwa simu na muathirika mmoja saa 5 usiku siku hiyo akiomba atumwe mwandishi na mpigapicha kushuhudia waathirika walivyokuwa wakivunja mlango wa vyumba ambamo magodoro yalifungiwa tangu yalipofikishwa mchana.

Kusema kweli, watu wengi walisalimika vifo kwa kudra tu ya Mwenyezi Mungu.

Kwanza, serikali imezidi kukaa uchi kwa kukosa vifaa vya uokoaji. Jitihada za taasisi zake hazikuonekana, isipokuwa pale wapiganaji wa Jeshi la Ulinzi walipoharakia kwenye baadhi ya maeneo yaliyo karibu nao.

Ilitarajiwa serikali haraka ipeleke askari kwenye maeneo yaliyokumbwa na mafuriko ili kusaidiana na wananchi katika kazi ya kuokoa waathirika. Askari hawakuwepo na wale wachache waliokutwa hawakuwa na vifaa.

Kilichoonekana zaidi ni hatua za zimamoto za kutoa lawama kwa wananchi waliofikwa na mafuriko wakisimangwa kuwa wamejitakia kwa kuendelea kushikilia kuishi mabondeni, kama vile watu wote walioathirika wanaishi mabondeni.

Baadhi ya maeneo ambako maji yalifika ni ya juu lakini kule mamlaka za serikali kuruhusu ujenzi wa majengo ya kibiashara kwenye njia za maji, kulisababisha kuzuia maji kupita mkondo wake na hivyo kupanda kwenye nyumba za juu.

Hapa wa kulaumiwa ni waliojenga au wale watumishi wa umma waliowaruhusu kujenga?

Ndio maana tunasikitika kusikia serikali ikiamuru kubomolewa kwa makazi ya mabondeni. Ubomoaji utafanyika vipi kabla ya kila nyumba kusajiliwa na wenyewe kupatiwa nyumba nyingine?

Ni jambo baya kumvunjia mtu nyumba yake bila ya kwanza kumpatia sehemu mbadala ya kuishi. Hata akipatiwa kiwanja, wapi atapata fedha za kujenga haraka ili ahamie na familia yake wakati amepoteza kila kitu kutokana na mafuriko?

Haya ni mambo ya kutiwa akilini kabla ya uamuzi mzito kuchukuliwa kama mpaka leo waathirika wa milipuko ya mabomu Mbagala na Gongolamboto hawajapatiwa viwanja.

0
No votes yet