Mafuta yanavyohangaisha utawala Z’bar


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 06 July 2011

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

KATIKA mazingira ya mfungamano wa kiutendaji uliopo ndani ya Jamhuri ya Muungano imekuwa vigumu Zanzibar kujizongoa na kile kinachoonekana kama mnyororo ili kujitegemea kiuchumi.

Ukweli huu unajengwa na ushirikiano uliotokana na kuunganishwa dola mbili zilizokuwa huru kabla – Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika – kwa mkataba uliasainiwa 26 Aprili 1964.

Sasa mfungamano huu, unajichimbia katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, inayojumuisha nchi tano wanachama baada ya Burundi na Rwanda kujiunga pale Kenya, Uganda na Tanzania zilipoasisi ushirikiano huo.

Kwa kuwa Tanzania ni muungano wa nchi mbili, Zanzibar inaingia kwenye jumuiya kwa mgongo wa Tanzania.

Jambo jipya limejitokeza. Baraza la Wawakilishi, chombo cha kutunga sheria mfano wa Bunge, limeambiwa itakuwa vema Zanzibar itambuliwe na kama mwanachama mshiriki – Associate member.

Nini? Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, Ismail Jussa Ladhu wa Mji Mkongwe, kupitia Chama cha Wananchi (CUF), anashauri serikali kuomba Sekretarieti ya Jumuiya irekebishe itifaki ya ushirikiano ili Zanzibar ijisemee yenyewe.

Jussa ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF, anaipa nguvu hoja yake kwa kusema wakati itifaki ya jumuiya ya Afrika Mashariki inaunganisha nchi wanachama kwa mambo 17, kwa Jamhuri ya Muungano ni mambo manne tu ndiyo mambo yanayoshughulikiwa kimuungano.

Nini maana yake? Kwamba Zanzibar inayotambuliwa na jumuiya kama mshirika katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inanyimwa haki ya kimsingi ya kushughulikia mambo yale 13 yasiyokuwa katika muungano wake na Tanzania Bara.

CUF kinashirikiana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kuongoza serikali chini ya mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Nini matokeo ya mfungamano huo wa mambo yasiyokuwa ya muungano katika jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo Zanzibar imeingia chini ya mgongo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?

Kwamba Zanzibar haiwezi kusimamia masuala hayo 13 kwa uhuru na kama vile inavyoona inafaa kuyasimamia. Huku ni kunyimwa uhuru wake wa kimsingi kama nchi.

Ndipo Jussa anapoishauri SUK iwasiliane na Sekretarieti ya Jumuiya kuitaka irekebishe itifaki na hivyo kuipa uhuru Zanzibar wa kuamua itakavyosimamia yenyewe mambo hayo kwa maslahi ya Wazanzibari.

Baadhi ya mambo yanayobainishwa katika itifaki ya jumuiya ambayo hayamo katika Orodha ya Mambo ya Muungano kama inavyobainishwa katika Makubaliano ya Muungano – Aricles of Union – ni Kazi, Utalii, Mazingira na HIV/AIDS.

Ikumbukwe kuwa Makubaliano ya Muungano ndiyo msingi wa mambo ambayo dola mbili huru, Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika, zilikubaliana kushirikiana kimuungano.

Mambo yaliyomo kwenye orodha hiyo yanasomwa katika Ibara ya 102 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Vile Zanzibar inavyochukuliwa katika jumuiya ilikuwa moja ya hoja zilizotawala mjadala wa bajeti ya kwanza ya SUK kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012.

Hiyo ni moja ya changamoto nyingi kwa serikali ya Dk. Ali Mohamed Shein, ambaye kwa miaka minane kuanzia Julai 2002, aliitumikia Serikali ya Muungano kama makamu wa rais, alipoteuliwa kuziba pengo la Dk. Omar Ali Juma (Mwenyezi Mungu amrehemu) aliyefariki 2 Julai 2002.

Na changamoto hii inachimbuka mifupani mwa muungano wa Tanzania ambao kwa Zanzibar unaendelea kuonekana kikwazo cha maendeleo yake.

Sitakosea nikisema wananchi na viongozi wakuu wa serikali Zanzibar wanaamini chini ya mfungamano wa kimuungano, Zanzibar itabaki nyuma kwani “imebanwa na haitoki bila ya ridhaa ya Dar es Salaam.”

Wazanzibari wanakumbuka walivyopigwa “changa la macho” na Tanzania. Mwaka 1993, Zanzibar ilipotangaza rasmi kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislam (OIC), haraka ilitakiwa kutoka.

Wakuu wake walitishwa kuadhibiwa wasipoitoa Zanzibar kwenye jumuiya hiyo.

Serikali ya muungano iliahidi kwamba itafikiria kujiunga baada ya kutafiti muundo wa jumuiya hiyo kwa kuwa Zanzibar haipaswi kufanya hivyo kisheria.

Tangu hapo kila ikiulizwa inatapatapa. Imezidisha kigugumizi kila swali kuhusu suala hilo linapoulizwa, iwe ndani au nje ya bunge.

Lakini, zipo taarifa kuwa wakuu wameapa Tanzania haitajiunga OIC, mjumuiko unaofadhili miradi ya maendeleo kwa nchi wanachama, zikiwemo zile zenye watu wachache Waislam. Msumbiji na Uganda ni mfano wake.

Hatua ya Serikali ya Muungano kuilazimisha Zanzibar, ilikuwa mzaha. Kilichokuja baadaye, kule Tanzania kukaa kimya na sasa kuthibitisha haiko tayari kujiunga OIC, ndiko kunawaumiza Wazanzibari.

Kwamba kumbe muungano ni kiinimacho. Kwamba kwa yale ambayo Zanzibar inaamini yataisaidia kuendelea, inazuiwa na inatishwa isithubutu, lakini Tanzania Bara yenye raslimali nyingi inazozitumia bila ya kuifikiria Zanzibar, ina uhuru wa kujitanua.

Ni mtizamo huu uliochochea wawakilishi kuibana serikali ndani ya mjadala wa bajeti, isimame imara na kuzingatia matakwa ya wananchi badala ya kuhofia kuandamwa na wakuu wa Dar.

Ndivyo hoja ya kutaka SUK iharakishe uanzishaji wa shirika lake la maendeleo ya mafuta na gesi – Zanzibar Petroleum and Gas Development Corporation, ZP&GC – ili kushughulikia uchimbaji wa mafuta yaliyowahi kuthibitishwa kuwa yapo chini ya ardhi ya Zanzibar tangu miaka ya 1950.

Kabla ya kumaliza muda wa uongozi wake, Amani Abeid Karume kutokana na azimio la baraza lilojadili suala hilo, alianzisha utaratibu kuwezesha mafuta na gesi kuondolewa kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano.

Ingawa kauli za kisiasa zinabeza, ripoti ya kitaalamu inathibitisha Zanzibar kauwa na mafuta kutokana na utafiti uliofanywa mara mbili ikiwemo mpaka miaka ya 1980.

Maeneo yaliyogundulika dalili za mafuta ni Tundaua, kwenye mwambao wa magharibi mwa kisiwa cha Pemba, na Kama, mwambao wa magharibi mwa kisiwa cha Unguja. Kama ni kilomita 12 tu hivi kutoka bandari ya Malindi, mjini Zanzibar.

Karibu kila mwakilishi aliyejadili bajeti aliyowasilisha Waziri wa Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo, Omar Yussuf Mzee, alihimiza hatua zilizobaki za kuhakikisha mafuta yanakuwa suala la kushughulikiwa na Zanzibar yenyewe.

Ndipo Jussa alipovunja mfupa kwa kuamini itachukua miaka mingi Dar kuridhia jambo hilo, aliposema SUK iandae rasimu ya marekebisho na kuipeleka bungeni.

Utaratibu wa kikatiba na kanuni za bunge zinaelekeza kuwa jambo lolote linalogusa muungano linapohitaji uamuzi, lazima liridhiwe na theluthi mbili ya wabunge wa Zanzibar na pia kwa wabunge wa Bara.

Jussa hana wasiwasi theluthi mbili itapatikana kwa wabunge wa Zanzibar, bali anahofia kwa wabunge wa Bara. Ikitokea ikakwama, anashauri Zanzibar iamue peke yake.

Kwamba suala hilo litakuwa limekosa muafaka na kwa hivyo itakuwa haki kwa Zanzibar kushughulikia mafuta na gesi inavyoona inajenga maslahi ya watu wake.

Kweli, huu ni mtihani kwa Dk. Shein. Pengine ndio maana Waziri Mzee na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi (CCM), waliposema kwa lugha nyepesi hatua zitachukuliwa bila ya “jazba.”

Mawaziri wakiwemo watokao CCM waliunga mkono hoja za Jussa kutaka mafuta yabaki katika himaya ya Zanzibar ili itumie mapato yake kujenga uchumi na watu wake.

Kama mambo haya mawili yatashughulikiwa kwa maslahi ya Zanzibar ni kitu cha kusubiri; angalau kwa sasa serikali inajua ikilala, itaamshwa tu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: