Magaidi kushambulia tena Kenya


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 25 April 2012

Printer-friendly version

UBALOZI wa Marekani nchini umetoa onyo jipya juu ya uwezekano wa mahoteli pamoja na majengo maarufu ya serikali jijini hapa kushambuliwa na magaidi.

Hata hivyo, ubalozi huo umesema haujui saa wala siku ya kufanyika kwa shambulio hilo, lakini una taarifa kuwa mikakati yao liko katika hatua za mwisho.

Taarifa ya onyo kutoka ubalozi huo ikikariri vyanzo vya kuaminika vya kiintelejensia, imewataka Wamarekani waishio nchini Kenya kuwa macho juu ya usalama wao.

"Ubalozi unawaarifu Wamarekani waishio nchini au wanaokuja kwa matembezi Nairobi kwamba umepata taarifa juu ya uwezekano wa kufanyika shambulizi katika mahoteli na majengo maarufu ya serikali ya Kenya,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

"Muda wa shambulio haujulikani, lakini ubalozi una kila sababu ya kuamini kwamba mipango ya shambulio hilo iko hatua za mwisho.  Ubalozi unawataka Wamarekani kuwa waangalifu katika maeneo yao na kuwa macho na usalama binafsi,” taarifa ilisisitiza.

Onyo hilo limekuja katika kipindi ambacho maofisa usalama wa Kenya wamekuwa wakitafakari namna ya kukabiliana na mashambulizi ya magruneti dhidi ya nchi hii na ambayo yanahusishwa na kikundi cha Kiislamu cha Al-Shabaab cha Somalia.

Mtu mmoja aliuawa na wengine 33 walijeruhiwa mwezi uliopita milipuko mwili ilipolipuka katika jiji la Mombasa.

Waziri mkuu, Raila alishutumu kikundi cha Al-Shabaab kuhusika na mashambulizi hayo.

0
No votes yet