Maghembe anasubiri nini elimu


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 23 June 2009

Printer-friendly version
Profesa Jumanne Maghembe

KWA miaka mingi sasa nimekuwa napata tabu sana kutambua mtu mwenye sifa inayostahili kuwa Waziri wa Elimu. Nasema wizara ya elimu bila kujali inapewa jina gani kwani kumekuwa na utaratibu wa kubadili majina ya wizara hii mara kwa mara.

Kuna wakati iliitwa Wizara ya Elimu na Utamaduni ikishughulikia elimu ya chini huku elimu ya juu ikiwa chini ya Wizara, Sayansi, Tekinolojia na Elimu ya Juu. Mara ikaja Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa elimu ya chini na elimu ya juu ikiwa inaendelea kuwa wizara ya Sayansi, Tekinolojia na Elimu ya Juu.

Mara zote, mabadiliko haya ya majina ya wizara yanafanyika kwa nia moja tu, kutaka kupata njia sahihi ya kushughulikia majukumu ya elimu kwa ufanisi.

Lakini kadri tathmini inavyokwenda imekuwa ni vigumu mno kutambua kama kweli majina haya yamesaidia kutatua kero za kimsingi za sekta ya elimu na hasa wadau wake wakubwa yaani walimu na wanafunzi.

Kwa mfano, hadi sasa ukizungumza ajira ya walimu unaweza kuchanganyikiwa. Kuna walimu wanaajiriwa na wizara ya Tawala wa Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI); wapo wanaojariwa kupitia Tume ya Walimu na wapo wanaoajiriwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, huku ajira zao zikiombewa kibali Utumishi. Wapo walioajiriwa kwa mikataba. Kwa hakika, kuna kila aina ya mgongano. Ni mkorogo juu ya mkorogo.

Katika mpangilio kama huo, mara nyingi imekuwa ni vigumu mno kujua kwa mfano, serikali imeajiri walimu wangapi? Wako wapi? Wanalipwa nini na nani?

Ndiyo maana nilianza hapo juu kwa kuuliza swali ni mtu wa sifa za namna gani anatakiwa kuwa Waziri wa Elimu nchini?

Ninauliza swali hili kwa sababu ni jambo la bahati mbaya kwamba watawala wetu hawajakaa na kuwaza na hatimaye kupata jibu la swali gumu kwamba walimu wawekwe kwenye mfumo upi wa ajira.

Hivi karibuni serikali ilipendekeza kwamba walimu wote wa shule za sekondari kama walivyo wa shule za msingi ajira zao zihamishwiwe halmashauri husika, kama za wilaya, miji, manispaa na majiji.

Nia ya mabadiliko hayo inaelezwa ni kuongeza ufanisi katika kuwahudumia walimu kwa kuwa wako karibu zaidi na halmashauri kuliko makao makuu ya wizara.

Ingawa kuna maelezo mengi yamekuwa yanatolewa kwa nyakati na mahali tofauti na watawala kuhusu ajira za walimu, jambo moja lipo bayana. Kwamba kwa miaka mingi mno udhaifu umeruhusiwa kutawala mfumo mzima wa ajira ya walimu.

Ni kwa maana hiyo, leo hii tunaona walimu wakiwa ni kundi pekee katika watumishi wa serikali ambao wanaishi maisha ya dhiki huku haki zao za msingi zikikanyangwa kila kukicha.

Mathalani, tuchukulie sakata la sasa la malimbikizo ya madai mbalimbali ya walimu, kama posho za likizo, mishahara, nyongeza ya mishahara na nyinginezo.

Walimu wamekuwa wakidai madai haya  wakijaribu kutumia kila aina ya njia halali, lakini mara zote wamekabiliana na mambo mawili; moja, vitisho vya nguvu za dola, mbili kauli za uongo na ulaghai kutoka kwa watawala.

Mwaka jana walimu walimu walitaka kugoma kushinikiza kulipwa malimbikizo ya stahiki zao.

Lakini mawaziri, Hawa Ghasia (Ofisi ya Rais Utumishi) na Profesa Jumanne Maghembe (Elimu na Mafunzo ya Ufundi), si tu walitambua kwamba walikuwa wamezidiwa kete na walimu, hivyo kukimbilia mahakamani kuomba kusimamishwa kwa mgomo huo, bali pia walitumia mbinu zisizokubalika katika nchi inayoheshimu utawala wa sheria.

Serikali ilikimbilia mahakamani mwishoni mwa wiki na kupata zuio la mahakama jioni Ijumaa siku waliojua kwamba walimu wasingeweza kuwa na njia ya kupangua zuio hilo. Lakini pia zuio la mahakama lilitolewa huku muda wa kazi ukiwa umemalizika.

Kwa maana hiyo, bila kujali hisia, haki na mahangaiko ya walimu, watawala walivuruga mgomo wao halali ambao ulikuwa umefuata taratibu zote kisheria. Walifanya hivyo wakati wanajua kwamba wao (watawala) ndio wamewafikisha walimu hapo.

Kwa ujumla walimu walikuwa wanadai zaidi ya Sh. 16 bilioni kama malimbikizo mbalimbali, ingawa baadaye baadhi walilipwa madai yao, huku wakiwa wamepunjwa mno.

Kuna zaidi ya Sh. 4.4 bilioni za halali kabisa ambazo hazikulipwa, hizi ni pamoja na mishahara kwa walimu wapya ambao wamefanya kazi kwa takribani mwaka mmoja sasa bila mshahara.

Mwezi uliopita Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) kilitangaza kwamba wangefanya mgomo kama serikali isingewalipa madai yao yanayofikia Sh. 4.4 bilioni.

Haraka haraka Profesa Maghembe akawahi kuzungumza na vyombo vya habari na kuahidi kwamba walimu wangelipwa madai yao ifikapo 15 Juni 2009.

Kwa staili ile ile ya hadaa, ilipofika tarehe 15 Juni 2009, si tu walimu hawakulipwa, bali hata hayo mahesabu yanayodaiwa hayakuwa tayari.

Waziri Maghembe aliibuka na kudai kwamba kamati ya kuhakiki madai ya walimu ndiyo kwanza ilikuwa imekamilisha kazi ya kuzungukia mikoa na kwamba sasa ilikuwa ikae kitako na kukokotoa madai hayo.

Visingizio vya Waziri Maghembe havikuishia hapo tu. Bali alikwenda mbali zaidi na kueleza kwamba walituma watu kwenda mikoani kuzungmza na mwalimu mmoja mmoja kati ya hao waliokuwa wanadai.

Kwa maneno mengine, waziri Maghembe anataka kusadikisha umma kwamba eti siku hizi wako makini sana katika kusimamia fedha za umma kiasi cha kufuatilia mdai mmoja mmoja na kuzungumza naye ana kwa ana.

Kama huu ungekuwa ndio utendaji wa serikali hakika habari ya miradi hewa na matumzi ya fedha yasiyoliongana na kazi iliyofanywa, ingekuwa ni historia.

Lakini haya yote yana maana gani? Kwamba walimu wanakorogwa kwa sababu ya utii wao. Hatua ya baadhi ya viongozi kuwapuuza walimu, ni wazi inaisababishia hasara taifa.

Hii ina maana kwamba kazi nyeti ya kutengeza taifa, kupika watalaam, imeachwa mikononi mwa watu wasioithamini kazi ya walimu. Hivyo kazi tuliotarajia ifanyike, haiwezi kufanyika kwa kiwango kinachotarajiwa.

Hali hii ndiyo inanifanya niamini kwamba bado kuna kazi ya kumpata Waziri wa Elimu mwenye kutambua nafasi ya elimu katika uhai wa taifa. Bila elimu madhubutu taifa hili litaendelea kubaki hapo lilipo, kama si kurejea nyuma zaidi.

0
No votes yet