Magufuli ameachwa njia panda


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 23 March 2011

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala
DK. John Magufuli

DK. John Magufuli, mmoja wa mawaziri mashuhuri katika serikali ya Rais Jakaya Kikwete, ameachwa njia panda. Taarifa zilizovuja mwishoni mwa wiki iliyopita, zilisema Dk. Magufuli amejiuzulu nafasi yake.

Muda mfupi baada ya vyombo vya habari kuripoti kile kilichoitwa, “barua ya Magufuli kwa Rais Jakaya Kikwete,” serikali ilitoa tamko kukanusha kuwa “Magufuli hajajiuzulu na wala hakuwa na nia ya kufanya hivyo na kwamba alikuwa akiendelea na kazi zake kama kawaida akiwa na imani kubwa na rais Kikwete.”

Hata hivyo, serikali haikusema kuwa Magufuli hajaandika barua ya kujiuzulu. Ilichosema hajajiuzulu. Sote tunajua kuwa wakati serikali inatoa tamko lake hilo, ni kweli Magufuli alikuwa bado hajajiuzulu.

Lakini hata kama Magufuli hajajiuzulu, bado hana jinsi nyingine isipokuwa kufanya hivyo. Kwa jinsi waziri mkuu Pinda alivyoingilia kati utendaji kazi wa Magufuli, mwanasiasa huyo hawezi kuendelea na nafasi yake aliyonayo sasa, na bado akaamini kuwa ataendelea kuheshimika mbele ya wananchi.

Kwanza, Pinda ametoa kauli yake mbele ya mkutano wa hadhara, jambo ambalo ni kinyume na utawala bora na kanuni ya utumishi wa serikali. Pili, ametoa kauli hiyo Chato, ambako ndiko walipo wapigakura wa Magufuli.

Kadiri anavyochelewa kujiuzulu ndivyo anavyopoteza uaminifu wake mbele ya wananchi waliokuwa wametokea kumuamini kuwa ni kiongozi anayeongozwa na kanuni na maslahi ya taifa na siyo utamu wa madaraka. 

Hata kabla ya kuteuliwa kushika tena nafasi hii, tayari Magufuli alijitofautisha na wenzake kwa kusimamia sheria bila ya kuangalia sura za watu, dini, rangi, au hata chama chake. Anakumbukwa alivyoshika nafasi hiyo kwa mara ya kwanza, hasa katika suala zima la kusimamia nidhamu ya matumizi katika fedha za ujenzi wa barabara.

Hata alipoteuliwa kuwa waziri wa uvuvi, bado Magufuli aliendelea kuaminika; hadi sasa hakuna anayezungumzia gharama kubwa za kuhifadhi samaki zinazobebwa na taifa kwa kuwa wengi wanaamini kutenda yote hayo kwa maslahi ya taifa lake.

Sasa alipoanza kuja na “bomoa bomoa” nyingine hasa baada ya kutoa angalizo 13 Januari 2011, kiongozi huyu alianza kuzigusa mioyo ya watu kwa kuwa ilikuwa ni imani ya wengi, kwamba sasa jiji la Dar es Salaam litaanza kupewa sura inayostahili na barabara zitaanza kusimamiwa ipasavyo.

Lakini wapi! Pinda amempiga “stop.” Amesitisha ubomoaji wa nyumba zilizopo katika hifadhi ya barabara. Anasema kazi ya Magufuli – bomoa hapa, jenga pale – imekuwa ikisababisha malalamiko “yasiyokuwa ya lazima” na kwamba jambo hilo litarudishwa serikalini ili lijadiliwe upya na kutafutiwa ufumbuzi mwafaka.

Kwa maneno mengine, Pinda amezuia upanuzi wa barabara na hivyo amemzuia Magufuli kufanya kazi zake. Lakini Pinda amekiri kwamba  Magufuli alikuwa anatekeleza wajibu wake chini ya sheria ya barabara ya mwaka 1937.

Yote haya yanamfanya Magufuli asiwe na mahali pazuri pa kusimamia isipokuwa kujiuzuli. Tukikubali hoja zilizotolewa na Pinda kule Chato na baadaye tamko lililojaribu kufafanua alichofanya, tunajikuta na hali ngumu ya kuamini umakini wa serikali.

Kwanza, kama kweli Magufuli katika kuagiza bomoa bomoa alikuwa anatumia sheria ambayo haipaswi kusimamiwa kwa sababu ni “ya zamani” na yeye akakubali kutoisimamia kwa sababu ni ya zamani, basi hastahili kuendelea kuwa waziri.

Hata Pinda mwenyewe anajikuta anapoteza nafasi ya kuaminiwa kuendelea kuwa waziri mkuu. Sheria haiachi kuwa sheria kwa sababu umepita muda! Sheria inafutika kuwa sheria endapo tu imefutwa na Bunge au vipengele vyake vimetangazwa na mahakama kuwa ni kinyume na katiba.

Sasa, kama Pinda atakubali kusitisha bomoa bomoa hii kwa sababu ya “sheria ya zamani” ina maana ya kuwa hasimamii sheria tena isipokuwa anaangalia ni sheria gani ya muda wa karibuni.

Pili, kwa kauli ya Pinda, inaonekana maamuzi haya mazito hayakupitia katika baraza la mawaziri wala kupata baraka za baraza hilo. Kama ni kweli, basi hapa kuna tatizo kubwa la umakini serikalini.

Hii ni kwa sababu, suala la ujenzi wa barabara na upanuzi wake, limeingizwa katika ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo Magufuli anaitekeleza. Je, Magufuli anawezaje kujenga barabara mpya au kupanua za kale, bia kuondoa wavamizi wa barabara hizo? 

Tatu, wote wawili (Pinda na Magufuli) hawawezi wakawa sahihi na wote wakabakia kama mawaziri wa Kikwete. Mmoja wao ni lazima ajiuzulu. Baba wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere alifafanua vizuri juu ya kanuni hii ya kiuongozi wa kisiasa katika kitabu chake cha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania.

Nyerere alikuwa anaelezea ni kwa jinsi gani waziri hawezi kumshauri kitu rais na kisha rais akatekeleza ushauri wa waziri wake, kisha waziri akarudi tena na kumshauri juu ya kitu kile kile lakini kinyume na ushauri wa awali halafu mtu huyo akabakia kuwa waziri.

Alikuwa anazungumzia juu ya waziri mkuu Malecela kuhusu suala la Tanganyika ambapo mwanzoni Malecela alishauri kutupwa kwa hoja ya Tanganyika. Rais Alli Hassani Mwinyi wakati huo akakubali.

Lakini baadaye baada ya kupewa shinikizo na wabunge waliojiita G55 – wakiwamo baadhi ya viongozi waliopo madarakani sasa – akatoa ushauri tofauti kwa rais.

Mwalimi akasema, “waziri mkuu huwezi ukamshauri rais wako kupinga, halafu baada ya siku chache, wewe huyohuyo umshauri rais huyo huyo kukubali hoja hiyo, ambayo juzi tu ulimshauri na kuipinga, na yeye akakubaliana na ushauri wako; na bado ukaendelea kubaki na wadhifa wako.”

Alisema, “Ama ushauri wako wa awali haukuwa sahihi, na wajibu wako ni kujiuzulu; au ulikuwa sahihi, lakini ukashindwa kuutetea na wajibu wako ni kujiuzulu. Huwezi kuendelea kuongoza serikali. Ama umwachie waziri mkuu mwingine anayeweza kutetea msimamo wa awali; au umwachie mwingine anayeweza kumpa rais ushauri huu wa pili. Wewe huyo huyo huwezi kushindwa kuutetea ushauri wako wa awali, halafu umshauri rais akubali ushauri ulio kinyume cha ushauri wa kwanza, na utazamiwe kuwa huo sasa utautetea.”

Magufuli aidha alikuwa sahihi kubomoa majengo yaliyojengwa kinyume cha sheria au hakuwa sahihi; ama Pinda alikuwa sahihi au hakuwa sahihi; kwa vile wote wawili hawawezi kuwa sahihi basi ambaye hayuko sahihi ni lazima ajiuzulu.

Hawezi kusema alikuwa sahihi kwenye alilolisimamia na baadaye akabadilika na kuwa sahihi sasa halafu asilipie gharama ya kutokuwa sahihi mwanzoni!

Pendekezo langu ni kuwa Magufuli ndiye ambaye anastahili kujiuzulu. Anatakiwa kuandika barua kwa rais na kumwambia amruhusu kuendelea na utekelezaji wa agizo lake la 13 Januari 2011 kwa sababu ni la kisheria na kwamba ni sahihi kimaadili na ni sahihi kwa maslahi ya taifa.

Kama rais hatokuwa tayari kumruhusu kuendelea na uamuzi huo, basi amvue madaraka vinginevyo yeye mwenyewe ajiuzulu. Rais Kikwete akiona kuwa Pinda anawakilisha maslahi na hisia za viongozi wengine wa CCM na serikali basi anatakiwa kumkatalia Magufulu ombi hilo na kumfukuza kazi Pinda kwa kushindwa kuwa na uwajibikaji wa pamoja.

Lakini, kinyume chake ni kweli. Endapo rais atamkubalia Magufuli kuendelea na zoezi lake kwa lugha yoyote tamu, basi Pinda ni lazima yeye ajiuzulu kwa kufuata kanuni hiyo ya Nyerere. Tatizo ni je, Kikwete ana ujasiri wa kupoteza mmoja wa mawaziri wake maarufu kwa sababu ya kufuata kanuni ya uongozi? Historia itamhukumu.

mwanakijiji@jamiiforums.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: