Magufuli hakustahili baraza jipya


Nyaronyo Kicheere's picture

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 09 May 2012

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki
Dk. John Pombe Magufuli

MIONGONI mwa mawaziri machachari walioteka hata nyoyo za wananchi ni Waziri wa Ujenzi, Dk. John Pombe Magufuli.

Waziri Magufuli ni mtu anayejifunza kwa haraka kazi na mazingira ya kila wizara anayopangiwa. Hii ndiyo sababu amekuwa bingwa wa kukariri vituo vya daladala, treni, viwanja vya ndege, na hata mifugo na samaki katika wizara alizowahi kusimamia.

Kukariri barabara za lami na za changarawe, zilijengwa lini na nani na kwa gharama gani ndipo kumempa sifa na umashuhuri, lakini yanayofanyika katika wizara yake yanatisha.

Hata hivyo, rais makini, anayefuatilia utendaji kazi wa mawaziri katika kila wizara, angemwajibisha siku nyingi Dk. Magufuli kwa kushindwa kuzuia wizi, ubadhirifu au kutoa maagizo yaliyolisababishia taifa hasara kubwa.

Katika baraza hilo jipya ambalo aliyeteua anatuaminisha kwamba ni zuri kuliko lile la akina William Ngeleja, Omar Nundu, Mustapha Mkullo, Haji Mponda, Cyril Chami, Ezekiel Maige itabidi tujiulize kwa kigezo gani?

Kama ni ubadhirifu, wizi na udanganyifu Wizara ya Ujenzi ni nambari moja. Hii ndiyo wizara iliyonunua ile meli au boti maarufu pale Magogoni iitwayo MV Magendo ingawaje ubavuni imeandikwa RESCUE, yaani UOKOZI.

Boti hii ilinunuliwa enzi zile Magufuli akiwa Waziri wa Ujenzi chini serikali ya awamu ya tatu iliyoongozwa na Rais Benjamin Mkapa. Hadi leo boti ile iliyonunuliwa kwa fedha za kigeni haijafanya kazi.

Ilipofika kwenye fukwe za Tanganyika boti hiyo ikawa inatumika kuchota na kufyonza mafuta kwenye meli na boti zingine bandarini na kuyauza kwa wavuvi, ndiyo maana ikaitwa MV Magendo.

Baada ya muda kidogo boti hiyo ikapwelezwa kwenye mchanga ambako hadi leo haifanyi kazi ya kuokoa kama tulivyotangaziwa siku ya uzinduzi kwenye kivuko cha kuelekea Kigamboni.

Bahati mbaya si wafanyakazi wa wakala wa vivuko au serikali wanaohoji aliyehusika kuagiza boti mbovu isiyofanya kazi wala kudai wahusika waitengeneze boti hiyo ili iweze kuwadumia wananchi.

Si hivyo tu, hakuna hata mfanyakazi mmoja kuanzia watendaji serikalini hadi wakala wa vivuko aliyepewa adhabu. Hata Waziri Magufuli hakuwajibishwa kwa hilo na sasa yumo kwenye baraza jipya.

Ubadhirifu mwingine uliofumbiwa macho katika wizara hiyo ni juu ya uagizaji, ununuzi na ufungaji mitambo ya kukatia tiketi kwenye kivuko cha kigamboni ambayo haikuwahi kufanya kazi tangu inunuliwe miaka yapata sita au saba iliyopita.

Sisi tunaokaa Kigamboni tunakumbuka vizuri sana jinsi serikali ilivyotutangazia kuwa wafanyakazi Kivukoni ni wezi sana na kwamba wanaiba mapato hivyo ikasema imekuja na mbinu mpya ya kukomesha wizi huo wa mapato – ikanunua wa mitambo ya kukatia tiketi.

Mitambo iliagizwa kwa pesa za kigeni, ikafungwa pale Kivukoni upande wa Magogoni na kusababisha milango miwili ya wapita kwa miguu kufungwa kwa miaka yote sita sasa.

Mitambo haitumiki, haitengenezwi na wala haiondolewi licha ya kusababisha kero ya msongamano kwa wasafiri kulazimika kupita mlango mmoja uliobaki.

Japokuwa hakuna ushahidi wa Magufuli kuhusika moja kwa maoja katika ununuzi wa boti mbovu na mitambo chakavu ya kukatia tiketi, alipaswa kuwashtaki wahusika au yeye mwenyewe kuwajibishwa kutokana na makosa ya waliochini yake. Magufuli hakuwajibishwa.

Lakini hakuna atakayebisha Magufuli alivyohusika kupigia debe uuzwaji wa nyumba za serikali bila kujali gharama ya maeneo nyumba hizo zilipokuwa zimejengwa.

Mbaya zaidi baadhi ya watu waliouziwa nyumba hizo hawakustahili kwani hawakuwa watumishi wa serikali. Kwa nini Magufuli hakuwajibishwa?

Wauzaji nyumba walitoa kigezo kwamba anayestahili kuuziwa nyumba hizo lazima awe mfanyakazi tu wa serikali ya muungano. Kigezo hicho hakikuzingatiwa.

Hii si mara ya kwanza habari hizi kuandikwa. Wakati zilipoandikwa magazetini yapata miaka minne iliyopita si Magufuli aliyejali wala mamlaka iliyomteua. Mpaka leo hajawajibishwa.

Dk. Magufuli pia aliagiza kuvunjwa kituo cha mafuta jijini Mwanza na kuliingiza taifa katika mgogoro mkubwa ambao uliishia mahakamani na serikali ikatakiwa kulipa mamilioni ya shilingi. Magaufuli hakuwajibishwa.

Kituo cha mafuta kimejengwa ndani ya mipaka ya jiji la Mwanza kwa vibali vya uongozi wa jiji. Lakini badala ya Magufuli kufuata taratibu za kisheria za kuchukua eneo la mtu binafsi alitumia mabavu na jazba huku akidai anatekeleza sheria.

Dk. Magufuli pia alilazimisha kuvunjwa nyumba katika barabara ya Morogoro pale Ubungo na Kimara mwaka 1997 na kuliingiza taifa katika mgogoro na raia wake na kuisababishia serikali hasara ya Sh. 65 milioni. Magufuli hakuwajibishwa.

Kwa bahati nzuri kwa upande wa serikali wakazi wa Ubungo - Kimara walikuwa mbumbumbu hawakwenda mahakamani kudai fidia ya mamilioni ya shilingi baada ya kuelewa vibaya hukumu ya maombi yaliyowasilishwa na wakili wao Profesa Mgongo Fimbo ndiyo maana hawakwenda mahakamani kudai.

Mmoja wa raia hao ambaye alilielewa vizuri shauri hilo Bw. Ebeneza Massawe, alikwenda mahakamani na kushinda kesi. Alilipwa na serikali Sh. 65 milioni.

Je, wote waliovunjiwa nyumba zao Ubungo na Kimara wapatao zaidi ya 350 wangefika mahakamani kudai fidia, serikali ingelipa kiasi gani?

Ikiwa mawaziri sita waliotemwa, Rais Jakaya Kikwete amesema ni uwajibikaji wa kisiasa, kwa rekodi hii ya usimamizi wa Dk. Magufuli alipaswa kuwajibishwa kwa kuondolewa kwenye baraza la mawaziri mara moja kwa sababu hatufai.

nkicheere@gmail.com; 0787788727/0718582755
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: