Magufuli kabebeshwa zigo


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 11 January 2012

Printer-friendly version

KIONGOZI akitumia lugha nzuri husifiwa sana kwa ushawishi; lakini akitumia lugha inayokera, hakopeshwi, huzomewa.

Hata akiomba radhi, kile alichokisema kama ni utekelezaji wa sera za chama chake au maagizo ya bosi wake, basi ndio kimetoka hicho.

Hivyo wakazi wa Kigamboni wanaolia na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli kwa kauli yake mbovu isiyo na ushawishi, wajue ametumwa kuzidisha mzigo wa gharama za maisha kama isemavyo sera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Ieleweke uongozi wa nchi hukabidhiwa mtu mmoja tu – Rais, kupitia uchaguzi mkuu. Ataunda serikali na kwa nguvu ya Katiba, atateua mawaziri kutoka wabunge.

Mawaziri ni wasaidizi wake na hutekeleza sera za chama au fikra au maagizo yake. Sasa, wa Kigamboni wanaomlalamikia Magufuli, wajue anatekeleza alichotumwa.

Fuatilia. Alipokuwa Waziri wa Ujenzi (2000–2005) chini ya Benjamin Mkapa, Magufuli alijenga barabara kweli lakini aliudhi.

Alisimamia uuzaji wa nyumba za serikali kwa viongozi. Wananchi walilalamika lakini walipuuzwa maana alikuwa anatekeleza maagizo tu.

Kwa kile kilichoonekana kipya kinyemi, Magufuli alizuia boti ya kampuni ya Fast Ferries kusafirishwa kwa barabara kutoka Dar es Salaam hadi Ziwa Victoria – Mwanza.

Dk. Magufuli alisema boti ilikuwa pana na nzito; ingeharibu barabara na kuvunja madaraja ambayo yamejengwa kwa fedha nyingi. Alitaka ichanguliwe ili isafirishwe vipandevipande ikajengwe upya Mwanza.

Mfanyabiashara Azim Dewji aliyepewa kazi ya kusafirisha boti ile akalazimika kutumia gharama kubwa kwa barabara za Kenya hadi Mwanza. Hadi leo, Kenya haijalalamika kama kwa kupitisha boti ile, barabara zilititia.

Dk. Magufuli alikataa barabara kuwekewa matuta kama njia ya kupunguza ajali. Alisema barabara kuu haziwi na matuta na alishangiliwa bungeni.

Rais Jakaya Kikwete aliposhika urais 2005, aliona Magufuli angekuwa kikwazo kwa anayoyataka.

Akamteua Andrew Chenge kusimamia barabara. Matuta yakajengwa hata katika barabara kuu. Pia Rais alitangaza mpango wa kurejesha serikalini baadhi ya nyumba zilizouzwa kipindi cha Mkapa na Magufuli akisisitiza “nyumba zilizokuwa maeneo nyeti hazikustahili kuuzwa.”

Mpaka hapo inatosha kujua Dk. Magufuli anajituma au anatumwa.

Baada ya kukamilisha mipango hiyo miwili, ndipo Rais akamrejeshea dhamana ya kusimamia ujenzi wa barabara. Akajisikia kama samaki mdogo kwenye bwawa kubwa. Akajituma kutangaza bomoa bomoa, bila fidia, nyumba zote zilizojengwa karibu na barabara.

Wee! Mtoto wa Mkulima, Mizengo Pinda akampiga ‘stop’. Akamwambia hajatumwa kutia watu umaskini; akamrejesha darasa elekezi: wasiostahili fidia ni wale waliozifuata barabara, lakini waliokutwa na barabara lazima walipwe fidia.

Kasi ya Dk. Magufuli ilipungua na ikadaiwa alitaka kuutema uwaziri na miposho yake. Rais pia akamwambia awe anaangalia historia.

Je, hili la Kigamboni amejituma au ametumwa? Iko hivi. Miezi sita tangu Bajeti ya Serikali iwasilishwe bungeni, serikali inakabiliwa na nakisi ya Sh. 800 bilioni.

Inahaha. Imekata baadhi ya ahadi kwa asilimia 50, imepanga vivuko vichangie walau nusu ya hizo.

Tayari Kigamboni kwa siku wanakusanya Sh. 18 milioni, ongezeko la Sh. 9 milioni. Hivyo Kigamboni peke yake (9m x siku 30 = 270m x miezi 6 = 162 bilioni) itachangia Sh. 162 bilioni. Hii ndiyo sababu Kikwete na Pinda wamenyamaza.

0658 383 979, jmwangul@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: